31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

ATC KWENDA SAFARI KENYA MWAKA KESHO

Ndege aina ATC Bombardier Q 400
Ndege aina ATC Bombardier Q 400

NA HARRIETH MANDARI-DAR ES SALAAM 

IMEELEZWA kuwa kufikia mwakani, ndege mpya za Shirika la ndege nchini (ATC) zitaanza safari za kwenda nchini Kenya, ambapo zitasaidia kurahisisha usafiri na pia kuinua Sekta ya Utalii.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa Tume ya pamoja ya Mashirikiano kati ya nchi ya Tanzania na Kenya, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, Benson Ogutu, alisema vile vile kwa Upande wa Kenya ndege za Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways), nazo pia zitaanza safari zake nchini Tanzania.

“Mkutano huu ambao unajadili umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano mzuri kati ya nchi hizi mbili ambazo ni majirani,  hasa katika sekta zote muhimu zikiwamo usafirishaji, biashara, maji, usalama, na mengineyo mengi kwa nia ya kuinua uchumi wa nchi hizi na  kuimarisha ushirikiano kwa manufaa ya nchi zote mbili,” alisema.

Njia hizo za ndege za Kenya Airways zitahusisha  jumla ya ndege nane zinazomilikiwa na shirika hilo la ndege  ambapo Ogutu alisema zitakuwa zikisafirisha abiria hasa watalii ambao hapo awali walilazimika kufanya safari mara mbili.

“Uhusiano kati ya nchi hizi mbili  ni wa kihistoria ambapo umekuwa wa  amani na mshikamano, lakini tumeona ipo haja ya kuuimarisha zaidi hasa katika  sekta mbalimbali ili kuleta ufanisi zaidi na hivyo kuinua uchumi kwa pande zote mbili kupitia ushirikiano huu,” aliongeza.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samuel Shelukindo,  alisema  kufuatia safari hizo za ndege, Tanzania inategemea kuinua sekta mbalimbali hasa ya utalii ambapo watalii wengi wanaotaka  kutembelea mbuga za wanyama wamekuwa wakiishia  nchini  Kenya.

“Tunategemea baada ya mkutano huu, tutaweza kuzijadili changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikizikumba nchi hizi mbili katika sekta zote muhimu na kutafuta suluhu na hivyo kuweza kunufaika na ushirikiano huu tunaojitahidi kuuimarisha,” alisema.

Akaongeza kuwa si tu watalii wataweza kutumia njia ya usafiri wa ndege hizo, bali hata wagonjwa ambapo kwa sasa kumekuwa na wagonjwa wengi wanaotoka nchi mbalimbali kuja nchini Tanzania kupata tiba,hivyo watakuwa wamerahisishiwa usafiri wa haraka na wa uhakika.

Anasema mkutano huo ilikuwa ufanyike mapema mwaka jana lakini kutokana na matukio makuu muhimu yakiwamo Uchaguzi Mkuu na marekebisho ya Katiba, ilipendekezwa  kusogezwa  mbele kwa mkutano huo muhimu.

Jumla ya ndege ambazo zinamilikiwa na ATC ni tatu kwa sasa, ukijumlisha  na ile iliyokuwapo kabla hazijawasili hizo mpya mbili. Shirika hilo la ATC lilianzishwa mwaka 1977 baada ya kuvunjika kwa lililokuwa Shirika la Ndege la Afrika Mashariki na kufuatia pia kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati huo na halijatengemaa kiuchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles