27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Profesa Muhongo aweka msimamo

sospeter-muhongoNa TERESIA MHAGAMA, RUVUMA

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameendelea kusisitiza kuwa, Serikali haitatoa vibali kwa viwanda nchini kwa ajili ya kununua madini ya jasi na makaa ya mawe  nje ya nchi.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe katika Mgodi wa Ngaka, ulioko Kata ya Ruanda, mkoani Ruvuma, unaomilikiwa na Kampuni ya Tancoal, Profesa Muhongo alisema Serikali haitatoa vibali hivyo kwa kuwa ina hifadhi kubwa ya madini.

Wakati wa ziara hiyo, Profesa Muhongo aliongozana na watendaji mbalimbali wa viwanda vya saruji vinavyotumia makaa ya mawe, Chama cha Wamiliki wa Malori (Tatoa), wazalishaji wa makaa ya mawe, watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na viongozi kutoka Mkoa wa Ruvuma.

“Baadhi ya viwanda vya saruji vimelalamika kuwa, kuna upungufu wa makaa ya mawe. Kwa kulitambua hilo, ndiyo maana wadau wote tuko hapa ili kujiridhisha kama kweli kuna upungufu wa makaa ya mawe au la,” alisema Profesa Muhongo.

Akijibu suala la upungufu wa makaa hayo ya mawe, Meneja wa Tancoal, David Kamenya, alisema katika mgodi huo wa Ngaka, madini hayo yapo ya kutosha na kwamba kuna hifadhi ya tani milioni 400 ambazo uchimbaji wake utafanyika kwa miaka 40.

Pamoja na hayo, Kamenya alisema mgodi wake una vifaa vya kutosha vya kuchimba madini hayo ili kukidhi mahitaji ya wateja.

“Hapa tuna vitendea kazi vya kutosha kwani kwa siku tunaweza kuzalisha tani 1200 hadi 1500 za makaa ya mawe kulingana na mahitaji ingawa tuna uwezo wa kuzalisha hadi tani 3,000 kwa siku.

“Kuhusu ubora wa makaa ya mawe, yana ubora unaotakiwa sawa na makaa ya mawe ambayo viwanda mbalimbali nchini vimekuwa vikiagiza kutoka Afrika Kusini,” alisema Kamenya.

Katika ziara hiyo, viongozi wa kampuni za saruji za Tanga, Rhino na Lake, zilikiri uwepo wa hifadhi ya madini hayo ya kutosha, lakini kinachowakwamisha ni kutokuwa na magari ya kutosha kwa ajili ya usafirishaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles