MBUNGE wa Misungwi, Charles Kitwanga (CCM) maarufu kama Mawematatu, amechangisha Sh milioni 28 na mifuko 226 ya saruji katika ujenzi wa shule ya sekondari ya kKata ya Gulumungu.
Katika harambee hiyo iliyofanyika katika Kijiji cha Nyamahinza, Leticia Luboja (75) alijitokeza kumunga mkono kwa kuchangia mifuko mitano ya saruji.
Kitwanga alimuomba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Misungwi kuwakamata na kuwafikisha mahakamani haraka mwenyeviti wa Kijiji cha Gulumungu, na wenyeviti wa vitongoji saba akidai wanakwamisha shughuli za maendeleo ikiwamo ujenzi wa sekondari hiyo.
Alisema anatambua Serikali haina fedha za kutosha kukamilisha kila kitu hivyo aliwaomba wananchi kujitokeza kuchangia miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na elimu.
“Sote tunafahamu changamoto za sekta ya elimu watoto kusomea katika mazingira yasiyo rafiki nitaendelea kuzungumza na marafiki zangu.
“Fedha hazitoshi, lakini kwa nguvu zetu zitatosha sasa nawaomba wale wenye nafasi na uwezo wa kuchangia mfanye hivyo na ukiitwa kuchimba msingi usiache kufanya hivyo,” alisema Kitwanga.
Kitwanga alisema yeye na marafiki zake waliomuunga mkono katika ujenzi huo wamechangia Sh milioni 11.7 na kati ya hizo Sh milioni 5.7 ni fedha tasilimu na ahadi zikiwa ni Sh milioni sita.
Alisema walioahidi ni kampuni mbalimbali wakiwamo rafiki zake na kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi imetoa mifuko 68 ya saruji ambayo itasaidia kukamilisha ujenzi huo.
Wananchi wa kata hiyo kwa pamoja walichangia Sh milioni 6,794,000 na kupitia Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) Sh milioni 3.7.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Misungwi, Anthony Bahebe alisema kazi ya kujenga shule haiishi kwa siku moja.
Alisema bila wananchi kusimama na kushikamana hakuna mtu wa kuwasaidia bali umoja wao utasaidia kukamilisha ujenzi huo.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Misungwi, Eliud Mwaiteleke alimshukuru Kitwanga kwa jitihada zake katika kuleta maendeleo jimboni humo.
Vilevile aliwashukuru wananchi kwa kujitolea na kuiunga mkono halmashauri ili kufikia maendeleo katika nyanja zote.