25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kodi ya Mapato huzingatia kumbukumbu sahihi

Kamishina Jenerali Kodi  alphayo-kidataNA KOKU DAVID-DAR ES SALAAM

KODI ya Mapato ni kodi inayotozwa kwa  mtu mwenye mapato yatokanayo na vyanzo mbalimbali vilivyoainishwa kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mapato yanayotozwa kodi ni yale yatokanayo na biashara, ajira na uwekezaji katika rasilimali kama  vile nyumba, viwanja, mashamba pamoja na hisa.

Pia kuna mapato yanayotozwa kodi ya zuio kamilifu kwa viwango maalumu kama vile malipo ya gawio kutoka kwenye kampuni ambayo ni mkazi wa Tanzania, riba itokanayo na benki ikiwa ni pamoja na malipo yatokanayo na matumizi ya maliasili.

Katika sheria hiyo, mapato yanayotozwa kodi kutokana na biashara yanajulikana kama faida au ziada itokanayo na biashara kwa mwaka wa mapato.

Mapato ya biashara yanajumuisha faida inayotokana na mauzo ya rasilimali za biashara kama vile kuuza bidhaa za duka la rejareja au jumla.

Endapo mtu au kampuni yoyote inataka kuanzisha biashara ni lazima taratibu za kodi zizingatiwe na kufuatwa.

Kwa biashara binafsi, hatua ya kwanza ni ya usajili kwa ajili ya kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) na kwa upande wa usajili wa biashara ya makampuni, inatakiwa wapate cheti cha usajili kutoka Brela ili biashara iweze kufanyika pasipo na usumbufu wowote.

Ni muhimu kwa mlipakodi kukumbuka namba yake ya utambulisho kila anapokwenda katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa shughuli mbalimbali za ukadiriaji na kulipa kodi kutokana na kuwa namba hiyo inarahisisha kupatikana kwa jalada lake la kodi.

Baada ya kupata TIN, mfanyabiashara (binafsi au kampuni) anatakiwa afuate taratibu zote za maombi ya leseni kwa kujaza fomu ya maombi inayopatikana katika ofisi ya biashara ya jiji, manispaa, mji au ofisi ya halmashauri ya wilaya au wizara ya viwanda na biashara.

Baada ya taratibu zote kukamilika, mfanyabiashara huyo atalipa kodi kulingana na mapato atakayokuwa akipata katika biashara zake na kwamba viwango vya kodi kwa wafanyabiashara vimegawanyika katika sehemu tatu.

Sehemu ya kwanza ni viwango vinavyowahusu wafanyabiashara binafsi na wadogo ambao mauzo yao hayazidi Sh milioni 20 kwa mwaka na sehemu ya pili ni kwa wafanyabiashara binafsi ambao wengine viwango vya kodi watakayotakiwa kulipa hutegemea faida inayopatikana kulingana na kumbukumbu za biashara na hesabu za mizania zilizokaguliwa.

Sehemu ya tatu ni kwa makampuni, mashirika, klabu, ushirika na taasisi nyingine ambazo kiwango maalumu hutozwa kwenye faida.

Kwa upande wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya mwaka 2014, kodi hii hutozwa kwa mlaji kwenye bidhaa na huduma zinazozalishwa hapa nchini na pia kwenye bidhaa au huduma zinazoingia Tanzania Bara kutoka nje ya nchi.

Pia hutozwa kuanzia ngazi ya uzalishaji wa bidhaa, uuzaji wa jumla, rejareja mpaka bidhaa inapomfikia mlaji wa mwisho.

Mfanyabiashara anayetakiwa kujisajili na VAT na kupata cheti cha usajili anapokuwa amefikia kiwango cha mauzo ya Sh milioni 100 ya bidhaa zinazotozwa VAT kwa mwaka na kwamba kiwango kinachotumika sasa ni cha asilimia 18.

Lakini ikumbukwe kuwa kutokana na sababu mbalimbali za kijamii, Tanzania haina utaratibu wa kutoza VAT kwenye kila kitu hivyo kuna baadhi ya bidhaa husamehewa kodi kabisa na nyingine hutozwa kwa kiwango cha asilimia sifuri.

Sheria zote za kodi zinasisitiza suala la utunzaji wa kumbukumbu sahihi za biashara kupitia mfumo wa utoaji wa risiti kwa kutumia mashine ya kodi kielektroniki (EFD).

Pamoja na kwamba ni matakwa ya kisheria, pia utunzaji wa kumbukumbu una faida kwa mfanyabiashara kwani utamsaidia kujua maendeleo ya biashara iwapo kuna faida, haja ya kuboresha zaidi, kudhibiti wafanyakazi ambao si waaminifu kwenye biashara, kufanya makadirio ya kodi ambayo ni sahihi, ikiwa ni pamoja na kutumika kama njia ya kushughulikia malalamiko ya kodi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles