23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

PROFESA MAGEMBE TAFAKARI UPYA KAULI YAKO

magembeKAULI mbili kati ya nyingi anazopenda kutumia Rais Dk. John Magufuli, zimekuwa zikinivutia sana. Kauli ya kwanza ni ile ya maendeleo ya Watanzania yataletwa na Watanzania wenyewe na ya pili ni ile ya kusema kila mtu afanye kazi ili kujiletea maendeleo binafsi na ya nchi kwa ujumla.

Kauli hizi mbili kama Watanzania wataziweka mioyoni mwao na kuzifanyia kazi, ni wazi kuwa baada ya muda nchi itafika pazuri.

Hata hivyo, ili kufanikiwa mchango wa Serikali unahitajika kutengeneza mazingira mazuri kwa watu wake ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.

Wakati Rais Magufuli akihimiza watu kufanya kazi, wapo baadhi ya watendaji wake ambao wamekuwa wakienda kinyume na dhana yake ya kuhimiza watu kufanya kazi kwa bidii kwa kuwavunja mioyo wananchi ambao wanajitahidi kutumia fursa mbalimbali kujiletea maendeleo.

Hivi karibuni kumekuwa na msuguano mkali kati ya Wizara ya Mali Asili na Utalii pamoja na wafanyabishara wa viumbe hai (CITES). Msuguano huo, umedumu kwa takribani miezi kumi sasa na wenye mamlaka hawaonyeshi dalili zozote za kutafuta suluhu yenye tija kwa pande zote mbili.

Nikiwa nafuatilia suala hii ilikuwa vigumu kidogo kuelewa kuwa kumbe wadudu ambao tunawaona kama kero na ambao tukikutana nao tunawaua.

Nilipokuja kusoma tangazo la Waziri wa Mali Asili na Utalii, Profesa Jumanne Magembe kwamba Wizara yake imepiga marufuku kusafirisha viumbe hao kwa kuwa haina tija kwa taifa nilizidi kuwa njiapanda.

Baada ya hapo, nilipata shauku ya kujua zaidi. Katika ufuatiliaji wangu niligundua kuwa biashara hii ipo tangu miaka ya 1970 na imekuwa ikifanyika kwa kufuata sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 1974 ambayo ilifanyiwa marekebisho kwa sheria namba 5 ya mwaka 2009.

Tangu kipindi hicho, biashara hii imekuwa ikiwaajiri maelfu ya Watanzania hasa wa vijijini wanaohusika na kuwakamata wanyama hao.

Niliweza kugundua kuwa biashara hii tofauti na biashara nyingine ina mlolongo mrefu sana na hufanyika kwa umakini mkubwa. Mtu anayetaka kufanya biashara hii anatakiwa kupata vibali zaidi ya vitano ikiwa ni pamoja na leseni ya kufanya biashara hiyo, kibali cha kukamata (capture permit), hati ya kumiliki viumbe (ownership permit), hati ya kusafirisha nje (Trophy export certificate) pamoja na leseni ya daktari kuonyesha kuwa viumbe hao wamechanjwa na hawana magonjwa yoyote (veterinary certificate). Ili uweze kusafirisha nje ni lazima uwe na vibali vyote na haiwezekani kuruka hatua yoyote.

Niligundua kuwa tofauti na biashara nyingine, mfanyabiashara anayefanya biashara hii anatakiwa kulipia tozo za kukamata (capture fee) viumbe kabla ya kwenda kuwakamata. Vibali hivi vyote hulipiwa.

Jambo lililonivutia zaidi kufuatilia ni baada ya kugundua kuwa ina tija kubwa kwa Taifa tofauti na alivyosema waziri. Biashara hii kwa mfano kwa mwaka huu ingeingizia nchi fedha za kigeni takribani Dola za Kimarekani 8,890,075 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 17 kama isingekuwa katazo la Waziri Magembe.

Wakati wa sakata hili, Waziri Magembe aliliambia Bunge na Taifa kupitia vyombo vya habari kuwa, Serikali inapata mapato kidogo kutokana na biashara hii.

Tangu kufungiwa kwa biashara hii Machi mwaka huu, watu ambao maisha yao huendeshwa kupitia vipato vinavyotokana na kuuza viumbe hai wamekuwa wakilalamika lakini Waziri Magembe ameapa kuwa hata ‘chawa’ hatatoka nje ya nchi.

Ni jambo la kushangaza na kuhuzunisha kuona waziri amekuwa hataki kutafuta suluhu ya jambo hili. Mara kadhaa wafanyabiashara hawa wamekuwa wakimwomba kuonana naye lakini amekuwa akiwakwepa. Desemba 20 mwaka huu kundi kubwa la wafanyabiashara hao walivamia ofisi za Wizara na kushinikiza kuonana na Waziri ndipo alikubali kufanya mkutano nao.

Badala ya Waziri kuwasaidia wafanyabiashara hawa ambao ni wazawa, anawakandamiza kwa kuwafungia milango ya majadiliano. Mara nyingi busara ni jambo jema zinapotumika katika jambo kama hili. Badala ya waziri kufungia biashara hii angeacha iendelee wakati marekebisho yakiendelea kufanyika.

Najiuliza kama TRA ingetumia njia kama ya Magembe kuamuru maduka kufungwa wakati wa sakata la mashine za kielektroniki au kuamuru migodi ya Acacia kufungwa baada ya kubainika wamekwepa kodi ingekuwaje.

Maamuzi anayoyashikilia waziri kwa mtizamo wangu naona kama ni ya kibabe na hayana tija kwa taifa. Profesa Magembe hajaweza kutoa ushahidi usio na shaka unaoonyesha kuwa kweli biashara hiyo imekuwa ikifanyika kiholela na kukiuka sheria na taratibu jambo ambalo linanifanya nitilie shaka nia yake juu ya biashara hiyo.

Magembe kama kweli angekuwa ni kiongozi mwenye nia ya kuwasaidia Watanzania wanaofanya biashara hii, angekaa nao na kuwaeleza kasoro ni zipi na wafanye nini ili kuzirekebisha badala ya kutoa kauli zenye upotoshaji.

Inawezekana kuwa zipo kasoro pamoja na kwamba mpaka kufikia sasa ni za kinadharia zaidi, lakini kasoro hizo zingeweza kutatuliwa kwa pande hizi mbili kukaa pamoja na kujadiliana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles