31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

JPM KWANINI TUNAFIKA HAPA?

magufuliNAKUANDIKA tena Rais wangu, nikijua kuwa yatakufikia. Safari hii ni suala hili la waandishi kuzuiwa kufanya kazi zao. Nilisikia hapo awali waandishi walifungwa muda huko Handeni; tena nasoma habari za mwandishi kufungwa huko Arumeru kwa amri ya Mkuu wa Wilaya. Nikusomee haya;

“… alikuja Ofisa Upelelezi wa Wilaya (OC-CID) na kutoa amri ya kumrudisha ndani Halfan (Lihundi) kwa madai ni amri ya Mkuu wa Wilaya akae ndani hadi saa 48 ziishe na si vinginevyo… alijibiwa kuwa hana kosa ila yuko ndani kwa amri ya Mkuu wa Wilaya…”

Sidhani kama Mheshimiwa Rais hilo la kuwafungia ndani bila kosa waandishi wa habari ni sehemu ya majukumu uliyowapatia wakati wakiapa na kusaini kiapo. Kuwaweka watu bila kosa, kutaka kuonyesha kuwa kuna mkuu wa wilaya… sidhani kama ndicho tulichowatuma katika kutekeleza ahadi ya kututumikia.
Kusimamia shughuli za maendeleo.

Cha ajabu ni kuwa haya yakitokea Waziri wa Ardhi, William Lukuvi, alikuwa wilayani Arumeru kufuatilia migogoro ya ardhi. Nadhani kama kweli alikuwa akifanya kazi yake vizuri isingekuwa muhimu Waziri Lukuvi kufika huko.
Arumeru ni wilaya yenye wafugaji na wakulima wengi na kama ikisimamiwa vizuri ingeweza kuzalisha mazao mengi na kuilisha sehemu kubwa ya mikoa ya Kanda ya Kaskazini.

Nilidhani kwa mkuu wa wilaya anayejua wajibu wake kwanza angeiweka ajenda hii juu katika kazi yake. Na kwa sababu waandishi wa habari ni muhimu katika kufikisha ujumbe sahihi na kwa wakati kwa wananchi, angeweka mkakati wa pamoja na sekta ya habari kuona anawezaje kufanikisha suala hilo maana waandishi wangemsaidia katika hili.

Waandishi wanapokwenda katika jamii wanakumbana na malalamiko mengi. Nimekuwa mwandishi wa habari za vijijini, mara kadhaa unafika kijijini na wananchi wenzako wanapokutambua wewe ni mwandishi wanataka kutoa madukuduku yao nje ya kile ulichofuata. Na unapokuja kufuatilia unagundua kuwa viongozi wanadanganywa, hawafiki kwenye maeneo na waandishi wanapoweka wazi, wanadhaniwa ni wazushi.

Nilifika wilaya fulani mkoani Tanga yenye tatizo kubwa sana la maji. Wananchi wakiwemo viongozi wa kata walinieleza kwa kina kiini cha mradi wa bomba kutofanya kazi. Nikaandika gazetini, Mkuu wa Wilaya alinipigia kulalamika. Nikamwambia kuwa tatizo hilo nalifahamu miaka mingi kabla ya yeye kuteuliwa ukuu wa wilaya na nikamwambia kwa ninavyolifahamu ataliacha halijatatuliwa. Na ndivyo ilivyo, alihamishwa tatizo lilibaki na limeendelea kuwa hadi leo.

Hao ndio wakuu wa wilaya. Wamekuwa ni watu wa kukuiga mheshimiwa Rais. Kwa sababu wao hawana watu wa kuwatumbua wanaona waige staili yako kwa kuacha kufanya mazungumzo na wadau wengine muhimu wa maendeleo, wanataka kugombana nao.

Ningekuwa mkuu wa wilaya nadhani ningeanza na namna gani waandishi wa habari wangenisaidia kujenga mfumo mzuri wa mawasiliano na kuweza kutoa taarifa za kimaendeleo kwa jamii, kufuatilia miradi na mipango ya maendeleo na mimi ningekaa kwa raha mustarehe kwani kila siku ningejua nini kinatokea katika wilaya yangu.

Waandishi wa habari ni sehemu muhimu ya harakati za maendeleo, ndio maana Vkadmir Lenin aliitaja kuwa ni “cog and wheel” ya harakati za kuletea jamii mabadiliko kutoka katika umasikini. Ukitaka kuona kuwa waandishi ni muhimu funga kila chombo japo kwa siku moja.

Utaona jinsi nchi inavyopwaya. Aidha, ukitaka kuona unadanganywa waache waandishi wa habari wasiandike chochote na utegemee taarifa za watendaji wako tu. Siku ukienda huko kwa wananchi utaona tofauti ya kile ulichoandikiwa na kile kilichopo.

Watendaji wa ngazi ya chini wana tabia ya kutosema ukweli kwa kuogopa kutumbuliwa. Waandishi ndipo wanapokuja kuwa watu wa muhimu sana sasa. Watakusaidia kukuambia kuwa kile ulichokipeleka kwa wananchi kimeeleweka; kama sera zako zinatekelezwa na kama kweli fedha za umma zimewafikia walengwa.

Kuwa Arumeru kuna tatizo la maji na waandishi wanasema hayo kutokana na malalamiko ya wananchi si uchochezi. Bali ilitakiwa kuchukuliwa kama mrejesho wa mipango ya maendeleo kuwa hakuna kinachofanyika kuhusiana na huduma hii muhimu. Mkuu wa wilaya alitakiwa kulichukulia kama changamoto na si kama tusi! Ila ni ushahidi pia kuwa alikuwa hajui kinachotokea wilayani mwake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles