27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

POLEPOLE: NINAJUA WATANZANIA WANACHOKITAKA KUHUSU KATIBA MPYA

Na ELIZABETH HOMBO


 

pole* Asema ndiyo maana hakuunga mkono serikali mbili

YAPO maswali mengi yaliyoibuka miongoni mwa jamii yetu baada ya mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole, kuteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Maswali hayo msingi wake mkubwa ni namna Polepole alivyokuwa mstari wa mbele kutoa maelezo, ufafanuzi na kukabiliana kwa hoja na wapinzani wa rasimu ya Katiba mpya.

MTANZANIA limefanya mahojiano ya ana kwa ana na Polepole, ambaye pamoja na mambo mengine, amejibu maswali hayo na amezungumzia namna CCM ilivyojipanga katika mambo mengi.

MTANZANIA: Ulipoteuliwa tu kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM ulisema tunarudi kwenye msingi, hebu tuelezee.

POLEPOLE: CCM ni chama kikongwe katika historia ya Tanzania, lakini Bara la Afrika kwa ujumla. CCM kina historia ndefu ya ukombozi wa Bara la Afrika, ukombozi wa Watanzania ambao ulifanyika chini ya vyama mama, yaani TANU na ASP.

Mageuzi ndani ya CCM imekuwa ni agenda hasa katika uongozi wa awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM.

MTANZANIA: Dhana ya mageuzi msingi wake nini?

POLEPOLE: Dhana ya mapinduzi katika miongo minne ni kwamba, CCM imepitia nyakati mbalimbali na ambazo nyingi zina changamoto kubwa ambazo zilipima umadhubuti wa chama kuendelea kuwa chama cha siasa ambacho kimepewa heshima na kupewa dhamana ya kuongoza.

Sasa yapo mambo mengi ambayo tumejifunza katika miongo hii minne na tumetengeneza taarifa nyingi, maarifa mengi ambayo imefikia pahala uongozi wa CCM chini ya JPM kwamba CCM kwa hali ilipofika ni lazima ijitazame upya, kijipange upya, kijirekebishe, kijitengeneze na kifanye mageuzi makubwa ambayo msingi wake mkubwa ni kuirudisha katika misingi ambayo kwayo kilianzishwa.

CCM tofauti na vyama vingine, kinayo misingi ambayo kwayo kilianzishwa tangu mwaka 1977. CCM ni imani na kinayo imani kinayoiamini na wanachama wa CCM wanapaswa kuwa wanachama wa imani.

Imani ya CCM malengo yake na haki za wajibu za wanachama sambasamba na ahadi pamoja na miongozo iliyotolewa kwa nyakati tofautofauti. Inatengeneza ujumla wa misingi ambayo CCM kinaisimamia.

Misingi hii bado ina maana kubwa, ina mantiki hata leo. Zoezi hili la kufanya mageuzi ndani ya CCM pale popote ambapo tulijikwaa, tukaenda nje ya mistari ya kuanzishwa kwa misingi ya CCM sasa tunairejesha kwa asilimia zote ili chama hiki kiishi misingi hii, itikadi yake ambayo kwayo kilianzishwa.

Lakini kusudi lingine kubwa ni kuhakikisha kwamba uhalisia kwamba CCM ni chama cha wanachama, chama cha watu kinapaswa kujinasibu na kujihusisha na shida za watu.

CCM kinapaswa kuwa kimbilio la watu wanyonge wengi wa taifa letu, kinapaswa kuwa sauti kwa wale wasio na sauti, kimbilio kwa wale wasiokuwa na nguvu.

CCM ambacho katika awamu hii kimepewa dhamana ya kuisimamia Serikali kinapaswa kuishauri, kuisimamia na kuikumbusha kuweka mazingira mazuri zaidi kwa wale wenye uwezo wa kuzalisha na kuendesha shughuli zao wazifanye kwa kufuata sheria na Serikali iwe na dhamana ya kuwawekea mazingira mazuri ili wao waendelee kufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria.

Kwa hiyo, mageuzi katika CCM yanalenga katika maeneo matatu, nasema tu kwa mfano; eneo la kwanza ni la kimfumo, kiutawala na mageuzi ya kiuongozi.

Kimfumo; tunazungumzia ujumla wa namna ambavyo CCM kinakwenda na kutenda katika shughuli zake mbalimbali namna ambavyo kinafanya uamuzi katika ngazi mbalimbali. Kinapokea maoni, hoja na changamoto za wananchi.

Namna ambayo kinaisimamia kwa ufanisi mkubwa Serikali. Tunapozungumzia mfumo; tunazungumzia mienendo, kanuni, taratibu, desturi njema ndani ya CCM ambazo zinawezesha utekelezaji wa sera, mipango na shughuli mbalimbali ambazo kwayo CCM kilianzishwa na kufanya shughuli zake kama chama cha siasa.

Tunaposema mageuzi ya kimfumo, tunamaanisha kuboresha kabisa mifumo ya ndani na ya kitaasisi, mifumo ambayo inalenga kukipatia chama chetu taasisi imara, madhubuti inayojisimamia, yenye mifumo ambayo inaweza kuhakikisha kwamba mali na rasilimali mbalimbali za CCM zinatumika kwa masilahi mapana kwa CCM, wanachama na umma wa Watanzania.

Eneo lingine ambalo tunalifanyia mageuzi ni la utawala; katika eneo hili, tunatazamia na tunaendelea kutafakari na tumefanya hivi katika vikao vikuu vya chama chetu kwamba ifike pahala utendaji wetu lazima ujikite katika weledi wa hali ya juu.

Lazima upimwe kwa matokeo, utaarifiwe na mipango mikakati sera za muda mrefu ambazo zitatusaidia kusimamia ipasavyo utekelezaji wa mpango wetu wa kati ambao unaitaarifu pia ilani ya CCM ya miaka mitano.

Kwa hiyo, unapokuwa na taratibu nzuri za kiutawala tutaweza kutumia rasilimali zetu chache, ambazo tunazizalisha wenyewe lakini pia tutaweza kuitumia ruzuku tunayoipata ambayo bado kwa ukubwa wa chama chetu haitoshelezi mahitaji yetu.

Lakini kile kidogo tutakitumia kwa umakini mkubwa, tutakuwa na nidhamu ya matumizi, tutakuwa na mifumo madhubuti ambayo tutahakikisha kwamba kidogo kile tunachokipata kinatumika kwa manufaa makubwa ya CCM kama taasisi, wanachama na Watanzania kwa ujumla.

Eneo la tatu ni mageuzi ya kiuongozi; uongozi ambao unaondoka kuwa uongozi tu unaoongoza na una wafuasi kwenda kuwa na aina ya uongozi ambao unawatumikia wanachama na umma wa Watanzania ambao unasikiliza kero na shida za wananchi.

Uongozi unaoishauri Serikali, unaisimamia na kuikumbusha Serikali kutenda sawa sawa na ahadi ambazo CCM kilizitoa wakati wa mchakato wa uchaguzi 2015, kwa hiyo uongozi wa kuwatumikia wanachama na Watanzania.

Viongozi wetu wa kitaifa wanaweza kufahamu kwa hakika mahitaji, matakwa, maoni ya wanachama katika ngazi ya msingi. Tunajitahidi katika eneo hili la uongozi, kuhakikisha hawawi viongozi mangimeza, viongozi wa kujifungia ofisini, viongozi wa kuongea na wenzao tu, tunataka wawe viongozi ambao wanaweza kuwa na mikutano kuhusiana na wanachama wetu wa msingi.

Kwa sababu tunapokuwa na utaratibu mzuri ambao viongozi wa kitaifa kwa mfano; wanafahamu kwa hakika nini changamoto za wanachama wa CCM, kwa kufanya hivyo tutapata kuelewa changamoto za Watanzania.

Na sisi kwa sababu ndio tuna dhamana ya Serikali tutatumia hiyo kama fursa kuielekeza Serikali kutatua changamoto hizo kwa wakati na mkakati. Kwa hiyo mageuzi ya CCM ni kupeleka chama kwa wanachama na wananchi.

Unapozungumzia mfumo namna tunavyokaa kwenye vikao vyetu na kufanya maamuzi, nikupe mfano; uamuzi mkubwa na wa kihistoria tuliufanya katika kikao cha mwisho cha Halmashauri Kuu.

Halmashauri Kuu ilikuwa na wajumbe 388, katika kikao kile wanachama kwa sauti moja wameamua kujipunguza hadi kufikia 158, mantiki ikiwa moja, kikao hiki kinasimamia utekelezaji wa shughuli kwa maana ya Kamati Kuu na sekretarieti ni kikao ambacho ni cha juu na kinatoa maelekezo.

MTANZANIA: Je, malengo yenu ni nini ya kupunguza idadi hiyo ya wajumbe?

POLEPOLE: Kupunguza idadi uwakilishi unakuwa mpana. Serikali ya awamu ya tano imejikita katika kubana matumizi, inapendeza sana Serikali hii inapokea maelekezo kutoka CCM, chama kimeona na kimeakisi dhamira ile imeelekeza Serikali kubana matumizi na kutumia rasilimali chache kwa manufaa ya wengi.

Kwa hiyo, tukasema si tu kupunguza, lakini pia twende mbali zaidi kwa kupunguza idadi hii tutakuwa tumepunguza fedha nyingi ambayo tutaitumia katika maeneo mengine ya maendeleo.

Kupunguzwa kwa vikao kumekwenda sambasamba na idadi ya vikao kwa mwaka. Halmashauri Kuu ilikuwa inakaa kila baada ya miezi minne, lakini sasa ni kila baada ya miezi sita, tafsiri yake ni nini?

Kikao kikubwa kama hiki kinatakiwa kikae, kitoe maelekezo makubwa ya kitaifa, muda mzuri wa kuyapima kutoka siku maelekezo yametolewa mpaka siku tunaona utekelezaji na kufikia hatua ya kuyapima, tukasema tuipe miezi sita, ni muda mzuri.

Kwamba baada ya miezi sita wajumbe wa CCM warudi kwa wananchi huku chini wafuatilie, kuangalia na kuzingatia utekelezaji wa shughuli mbalimbali, kwa hiyo wanapokuja kwenye kikao wanakuwa wana mrejesho mpana juu ya yale tuliyoazimia katika kikao kilichopita.

Marekebisho haya yamefanyika NEC na Kamati Kuu ambapo wajumbe wake wamepungua kutoka 30 mpaka 24. Hii itatuongezea tija.

Mageuzi haya ya CCM kuishi imani kwa vitendo kwa viongozi na wanachama. Kukirudisha chama kwa wananchi, mtu anapotaka dhamana ya uongozi aelewe si pesa, mali, si utajiri wake, si umaskini wake bali hoja zake, imani yake, maono yake na kusudio lake na akatueleze kwa hoja zenye mashiko na sababu  anataka kututoa wapi na kutupeleka wapi na si nini anacho na nini hana.

MTANZANIA: Imekuwa ni kawaida kwamba ukitaka uongozi ndani ya CCM lazima uwe na uwezo wa fedha, mmejipanga vipi kuondoa dhana hii iliyojengeka na  Watanzania wategemee nini?

POLEPOLE: Wananchi wategemee mambo makubwa katika mageuzi haya; kwanza ni namna ambavyo tunapata uongozi ndani CCM.

Kipindi hiki wote wanaopenda kupata dhamana tunapenda wapate kwa sifa, vigezo, imani yao kwa CCM na maelezo yao thabiti yaliyojaa hoja, kwanini wanataka dhamana, hivyo tunapoelekea 2020 CCM kimejipanga vilivyo, watoa na wapokea rushwa hawatakuwa na nafasi tena ndani ya CCM.

MTANZANIA: Ulipata kuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mpya na ulikuwa na msimamo wa serikali tatu ambao ulipingwa na chama chako, je, utawashawishi viongozi wakuu, hasa Rais Magufuli ili wabadili msimamo au wewe utabadili ili uendane nao?

POLEPOLE: CCM ya sasa imeamua kuwasilikiza wananchi.

MTANZANIA: Kwa maana hiyo mtairejesha ile rasimu ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini Jaji Joseph Warioba?

POLEPOLE: Ujue ninapenda kuwafikirisha watu kwamba ninaposema CCM imeamua kuwasikiliza wananchi tafsiri yake ni nini. Ngoja nikueleze; mimi ninajua wananchi wanachokitaka kuhusu Katiba mpya na ndiyo maana mimi sikusema serikali mbili bali nilisema tatu.

CCM sasa inawasikiliza watu…wakati ukifika wa Katiba mpya, CCM hii mpya itasikiliza wananchi walisemaje kuhusu Katiba.

MTANZANIA: Kwa maelezo yako ni kwamba mtairejesha ile rasimu ya Jaji Warioba

POLEPOLE: Haaaaaa!…nimeshaelewa unachokitafuta… acha tusubiri muda ukifika. Lakini nimeshakwambia kwamba hii ni CCM mpya. Tusubiri makubwa mazuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles