24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

JINAMIZI LENYE SURA MBILI LINAMKABA RAIS OBAMA

untitled-1KUNA usemi wa mazoea kuwa usingizi ni zoezi la kifo kwani kulala ni sawa na nusu kifo, kwa kuwa huyatambui yanayokuzunguka labda utakachokiona ni ndoto au maono kama umejaliwa karama hiyo.

Lakini pia usingizini kuna mengi zikiwemo ndoto za jinamizi au kuwangiwa na walozi kutegemea na unavyoamini, lakini kuna usingizi usiofumbwa macho kwa matamanio ya kutimia ulichoshindwa kukitimiza licha ya kudhamiria awali.

Anayekabwa na jinamizi huweweseka kwa sauti zisizoeleweka na jinamizi la kisiasa humuwewesesha Rais kupitia hotuba au matamko, hata kama hana uwezo wa kubadili hali iliyopo kwa kuchelewa kutimiza sera zake wakati muda umeshamtupa mkono. Hicho ndicho kinachomkabili Rais Barack Obama wa Marekani anayemaliza rasmi muda wake majuma matatu na ushei yajayo.

Jinamizi lililomwinamia Rais Obama lina sura mbili zinazojibadilisha kwa kumkenulia meno na kuogofya mustakabali anaoiachia Marekani, anajaribu kufumbua mdomo kulikemea akiwa katika usingizi wa kisiasa lakini anashindwa kutamka maneno yoyote.

Kutokana na sura ya atakayekabidhiwa madaraka Rais mteule Donald Trump kuvaa sura ya hasimu wake, Vladimir Putin wa Urusi, ambaye hata jina lake linatisha kwani ukikosea kulitamka unaweza kusema ‘Rasputin’ jina la Mtawa mtata katika historia ya Urusi aliyeitwa Grigori Yefimovich, aliyetumia miujiza kuvuruga utawala wa taifa hilo.

Kama miujiza ya Rais Putin kupitia Trump inavyomvuruga Obama aliyetamani kuiacha Marekani isiyotikiswa na mahasimu wake lakini ameshindwa kukamilisha mipango mingi aliyoiandaa.

Kwa bahati mbaya atakayemkabidhi madaraka ameshadhihirisha mtazamo mbadala wa sera na kulegeza msimamo dhidi ya Urusi, kwa kuwaachia wafanye wanavyotaka nchini Syria kwenye vita isiyo na macho isiyoisha, jimbo la Krimea lililomegwa nchini Ukraine.

Lakini pia kushindwa kumaliza mzozo wa Iraq hususani mjini Mosul, bila kusahau aliyoyasababisha Obama barani Afrika hasa nchini Libya kulipogeuka chanzo cha uzalishaji wahamiaji haramu wanaokimbilia Ulaya.

Kuapishwa kwa Rais wa 45 wa Marekani, Donald Trump, Januari 20, 2017 kutakakoashiria kuanza kwa muhula wake wa kwanza wa miaka minne akiwa na Makamu wake, Mike Pence, ni jinamizi ambalo Rais Obama asingependa kuliona likimkaba zaidi akiwa nje ya madaraka hivyo hataweza kupiga kelele za kuweweseka kupitia hotuba na matamko.

Kinachomuwewesesha Obama aliyefanya ziara kwenye nchi marafiki wa Marekani ili kutuliza kihoro cha kuchaguliwa Trump, ndicho kinachowawewesesha Wamarekani wasiomtaka Trump lakini nao hawana uwezo wa kuzuia jinamizi hilo labda wabadilishe mfumo wa kuchagua Rais, ambao ni mchakato mrefu usio na uhakika wa kukamilika hata ndani ya miaka minne ya awamu ya kwanza ya Rais Trump.

Kwa utaratibu wa Marekani baada ya kushinda uchaguzi, Trump aliidhinishwa rasmi siku tisa zilizopita na wajumbe wanaopiga kura turufu ambao ni jopo la Maseneta na wawakilishi wa Congress. Kuapishwa kwa Rais husimamiwa na kamati mbili za wawakilishi wa Bunge na kamati ya uapishaji wanaosimamiwa na kamati ya sheria na utawala ya Maseneta na mazoezi ya maandalizi ya uapishwaji yalishaanza tangu Novemba kwa kusimikwa jukwaa rasmi la kiapo na mazoezi ya gwaride.

Kuna tofauti kubwa ya siasa za Marekani hata kuhusu wasimamizi wa kuapishwa Rais, mathalani ungetarajia kamati ya maandalizi kugubikwa na wanasiasa lakini kamati hiyo inayohusika pia na shamrashamra tangu yakiwemo maandamano ya treni, gwaride, maonesho ya muziki, dhifa na sala mahususi inasimamiwa na Mwenyekiti wake, Thomas J. Barrack, wakala wa uthamini majengo ambaye ni CEO wa kampuni kubwa ya uwekezaji rasilimali.

Wajumbe wake ni Sheldon Adelson mmiliki wa Casino za Palazzo na Venetian, Steven Wynn, mfanyabiashara anayemiliki Casino, Harold Hamm, mwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi, Diane Hendrics mwanamama mfanyabiashara, Joe Craft, mwekezaji wa sekta ya makaa ya mawe na Woody Johson mmiliki wa timu ya kandanda la Marekani ya New York Jets.

Hao ni baadhi ya wajumbe wanaopanga mikakati ya upatikanaji dola milioni 70 zitakazotumika katika sherehe za uapishwaji wa Rais Trump, ambaye ujio wake ni jinamizi si tu kwa Rais Obama lakini pia Wapalestina waliotamaushwa na dhamira yake kuuhamishia ubalozi wa Marekani nchini Israel katika jiji la Jerusalem wanalodai kupokwa na Wayahudi.

Tayari Rais Mteule Trump ameshateua baadhi ya mawaziri akijumuisha ‘watata’ wenzake wasiotabirika akiwemo Ben Carson, Tabibu aliyejiondoa katika kinyang’anyiro cha kugombea urais baada ya kubaini hatafanikiwa dhidi ya Trump, aliyemteua kuwa Waziri wa makazi na maendeleo ya miji.

Kinachosababisha mkanganyiko zaidi wa kihoro cha Trump ni uteuzi wa wasaidizi wake muhimu akiwemo Balozi wa Marekani nchini Israel, David Friedman, ambaye ni wakili wa ufilisi anayeunga mkono utanuzi wa Israel jijini Jerusalem na kufifisha uwezekano wa kuundwa kwa taifa la Palestina.

Ufumbuzi uliohangaikiwa na Marekani tangu wakati wa Rais Bill Clinton ili kupata suluhu ya kudumu ya mzozo huo kwa kuwa na mataifa mawili yanayotangamana kwa amani.

Ni jinamizi litakaloigubika dunia kutokana na mwelekeo wa Serikali mpya ya Marekani utakavyokuwa baada ya kushika hatamu za madaraka Januari 20 mwakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles