WANNE KIZIMBANI KWA WIZI WA NG’OMBE

0
889

Na MALIMA LUBASHA- SERENGETI


ngombeWAKAZI wanne wa Vijiji vya Misseke na Nyamakendo wilayani Serengeti, mkoani Mara, wamekamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za wizi wa ng’ombe.

Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Jacob Sanga, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Serengeti, Ismael Ngaile, aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Marwa Girimwa (48), John Makuru (18), Makuru  Goreri (36) wakazi wa Kijiji cha Misseke na Mwita Nyaisuka (28), mkazi wa Kijiji cha Nyamakendo, Kata ya Machochwe, Tarafa ya Rogoro.

Ilidaiwa na mwendesha mashtaka kwamba, kati ya Agosti 20 na Septemba mosi, 2015, kwa muda tofauti, washtakiwa walifanya biashara ya kuuziana ng’ombe ambao baadaye walibainika kuwa walikuwa ni mali ya wizi waliokamatwa kwa mshtakiwa wa nne,  Mwita Nyaisuka.

Baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili, walikana kuhusika na wizi huo ambapo upande wa mashtaka na uliwauliza maswali kila mmoja alivyonunua ng’ombe, alama zilizowekwa na kama wana vibali walivyoandikiana wakati wa kuuziana mifugo hiyo, kila mmoja alisema hana uthibitisho wowote.

Katika kuanza kujitetea mshtakiwa wa kwanza, Girimwa, aliiambia mahakama kuwa Agosti 20, mwaka 2015, alinunua ng’ombe watatu aliouziwa na John Makuru kwa thamani ya Sh 600,000 na hawakuandikiana wala kupata kibali kwamba hiyo ni mali yake.

Naye mshtakiwa wa pili, John alisema Machi 9, 2015 aliuza ng’ombe hao watatu kati ya watano aliolipwa na mshtakiwa wa tatu kama malipo yake ya mshahara kwa kufanya kazi ya kumchungia ng’ombe tangu 2011 hadi Januari 2016.

Alidai kila mwaka hulipwa ng’ombe mmoja na kukiri kupokea mifugo inayonunuliwa na tajiri wake, Goreri ambaye ni mfanyabiashara wa mifugo.

Aidha, mshtakiwa wa tatu, Makuru Goreri, alijitetea kuwa Februari 20, 2015, alinunua ng’omb 20 katika  mnada wa Mugumu kwa thamani ya Sh milioni nne, huku  kila mmoja  akiuziwa  kati ya Sh 200,000 na 300,000, ambapo kesho yake aliwapeleka Kijiji cha Misseke na kumkabidhi mama yake mzazi pamoja na mchungaji wake ambaye ni mshtakiwa wa pili.

Naye mshtakiwa wa nne, Nyaisuka, alisema Septemba 1, 2015 alikwenda mnada wa Mugumu na kufanikiwa kununua ng’ombe watano aliouziwa na mshtakiwa wa kwanza kwa thamani ya Sh milioni 1.5 na kulipa ushuru wa halmashauri wa Sh 25,000 ambaye alikamatwa nao waliodaiwa walikuwa ni mali ya wizi.

Hakimu Ngaile alipotaka kujiridhisha dhidi ya tuhuma hizo, alimtaka kila mmoja kwa mujibu wa sheria kuonyesha kama waliandikiana na wale waliowauzia ng’ombe hao na kama walikuwa na kibali kilichothibitishwa na kiongozi wa Serikali baada ya kujiridhisha na kuweka muhuri wa Serikali.

Maelezo ya washtakiwa kukosa vielelezo  hivyo, Hakimu Ngaile aliwaonya washtakiwa na watendaji wa vijiji na kuwataka kabla ya kuandika kibali ajiridhishe kwa macho kuona kinachouzwa ni halali ya mhusika na uthibitisho wa nembo ya Serikali.

Pia alitoa ushauri kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya kutoa elimu kwa maofisa watendaji wa vijiji namna ya kutoa vibali kwa watu wanaokwenda kuuza mifugo mnadani wasikamatwe na mali za wizi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here