Na EVANS MAGEGE
MWENYEKITI wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Penina Mlama, amesema pamoja na utendaji kazi mzuri anaofanya Rais John Magufuli kwa sasa lakini mambo yatakuja kugongana na kumharibikia mbele ya safari kutokana na nchi kukosa msingi madhubuti wa itikadi inayobeba dira ya taifa.
Profesa Penina ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Sanaa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alitoa mtazamo huo katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika katikati ya wiki hii ofisini kwake.
Pamoja na kumsifu Rais Magufuli kufanya kazi kwa uchungu mkubwa kwa maendeleo ya Watanzania, lakini alisema ataangushwa kwa kukosekana msingi ambao utabeba itikadi zitakazolinda sera na juhudi zake za dhati za kuwasaidia wananchi.
“Rais anafanya kazi nzuri sana, nafikiri hata haya mambo tulipoyumba hapo nyuma inamuuma sana kwa hiyo anataka kuyaweka sawa na anayo nia nzuri, mambo aliyokwisha kuyafanya ni mazuri lakini mimi ninaamini kuwa bado kunahitajika sera ili hatua hizi nzuri anazochukuwa zijikite katika msingi fulani.”
Katika hilo alimshauri Rais Magufuli kuchagua moja, ujamaa au ubepari pamoja na itikadi zake.
“Kwa hiyo tukae chini tutafakari kwamba huku chini mambo yameharibika sasa tuamue tunakwenda wapi, kwenye ujamaa au ubebari? Lakini kama ataamua kwenda bila msingi wowote haya mazuri anayoyatenda kwa sasa yatagongana na kuharibika tu,” alisema.
Pamoja na hilo, Profesa huyo alisema lazima chama tawala pamoja na Serikali imsaidie Rais Magufuli kuamua juu ya dira ya taifa.
Alisema lengo la kufanya hivyo litamrahisishia Rais kuchukua hatua zinazobebwa na aina ya itikadi ya msingi iliyochaguliwa.
“Kwa sasa hivi namwona Rais anahangaika kujaribu kurekebisha mambo bila kubebwa na msukumo wa kiitikadi au wa kifalsafa, sasa binafsi nafikiri kutakuwa na ugumu na mambo yatagongana tu lakini haya ni mawazo yangu mimi,” alisema Prof. Penina.
Mtazamo huo wa Profesa Penina ulitokana na maelezo yake juu ya Azimio la Zanzibar ambalo amelitafsiri kuwa lilizika miiko ya uongozi na kuzaa sura mpya ya itikadi za kibepari ambazo ni kinyume na misingi iliyokuwapo ya mwelekeo wa nchi.
“Jambo la kusikitisha ni kwamba, baada ya Azimio la Zanzibar, si chama tawala, wala si Serikali waliokuja na tamko la kusema sasa tunaachana na ujamaa na mpaka leo sidhani kama wameshasema kwamba sisi sasa ni mabepari, kwa hiyo tumechukuwa ubepari au mwelekeo wa kibepari lakini kitaifa hatujatangaza rasmi.
“Utashangaa kuwasikia viongozi wanasema sisi bado ni wajamaa, sasa kama sisi ni wajamaa itikadi yetu ni ipi? Kama tumeamua kwenda nchi ya ubepari basi tuseme kuwa sisi ni mabepari na itikadi yetu katika ubepari wetu ni hii,” alisema Prof. Penina.
Katika muktadha huo, alisema kitendo cha utawala wa awamu ya pili, tatu na nne kushindwa kuweka itikadi inayoendana na Azimio la Zanzibar kumesababisha nchi kukosa mwelekeo hivyo kumekuwa na mvurugano wa mambo ndani ya tawala hizo.
“Unajua walishindwa kuhimili nguvu ya ubepari kwa sababu hawakutaka kuuweka wazi, alivyokuja kutawala kwa mfano Jakaya Kikwete (Rais wa awamu ya nne) ndio kabisa. Alianza Rais Mwinyi ambaye aliingiza mambo yake ya kurekebisha muundo lakini bado watu walikuwa wameshikilia itikadi za utawala wa Mwalimu Nyerere moyoni, akaja Rais Mkapa (Benjamin Mkapa Rais wa awamu ya tatu) akapigilia sasa huyu aliyeondoka juzi….kusema ukweli nafikiri tatizo la awamu ya nne haikuwa tu ubepari kuwa umeachiwa huru lakini ulikuwa ni utawala sijui ni uongozi yaani mambo mengi sana yaliachiwa.
“Kwa sababu unaweza ukawa ni ubepari lakini tatizo ni utawala. Kwa mfano ubepari hausemi watu wasilipe kodi, hakuna watu ambao wanalipa kodi kama mabepari. Marekani usipolipa kodi unafungwa tena si mwaka mmoja ni miaka mitano, haijalishi hata kama wewe ni nani. Hivyo kuna utendaji kazi fulani kwenye ubepari unataka kuchuma sasa na sisi tunaweza tukawa mabepari lakini hatuna utawala wa kibepari, yaani ukawa utawala holela tu, yaani watu hawalipi kodi.
“Sasa ikawa kama tunatekeleza ubepari ambao hauna malengo, ubepari gani watu hawalipi kodi yaani kila mtu anakuja anachukua tu. Labda kwa utawala huu uliopo sasa ambao umeonyesha nia ya dhati katika ukusanyaji wa kodi, lakini tusubiri tuone kwa sababu muda huongea,” alisema Prof. Penina.
Katika hatua nyingine alizungumzia dhana ya mbio za mwenge akisema inatakiwa iandaliwe upya ili kuweza kuendana na fikra za kizazi cha sasa kwa sababu inaonyesha wengi wao hawatambui lengo la mbio hizo.
“Vijana wanataka kufahamu kwanini mbio za Mwenge, kwanini sherehe ziwe ni kuzima Mwenge badala ya kuwasha, wanajiuliza umuhimu ni nini kuzima au kuwasha? Kwa mawazo yangu nadhani dhana hii inatakiwa kuzaliwa upya,”
alisema Profesa Penina.