25.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 6, 2022

Contact us: [email protected]

Mapya yaibuka kutoweka kwa Rais wa Malawi

mutharika

RAIS wa Malawi, Peter Mutharika, ametoweka na hajulikani alipo.

Mara ya mwisho alionekana hadharani Septemba 16, mwaka huu alipohudhuria Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) uliofanyika katika Jiji la New York nchini Marekani.

Licha ya mkutano huo kumalizika Septemba 26, mwaka huu lakini hajarejea nchini mwake Malawi wala haijulikani yuko wapi na anafanya nini na imewasababisha maelfu ya wananchi wa Taifa hilo kuhoji usalama wa rais wao, huku taarifa za Serikali yake zikisema kuwa hana tatizo lolote na atarejea haraka leo Jumapili.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana kwa njia ya simu kuhusu kutoweka kwa Rais Mutharika mwenye umri wa miaka 76, ofisa mmoja wa juu aliyewahi kufanya kazi miaka ya hivi karibuni katika Ubalozi wa Tanzania uliopo nchini Malawi ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema kwa taarifa alizonazo ni kwamba baada ya kumaliza kuhudhuria mkutano huo inadaiwa kuwa alifanyiwa upasuaji wa kansa ya koo.

“Nimepewa taarifa za Rais Mutharika na marafiki zangu waliopo serikalini pale nchini Malawi, japo inasemekana ni uvumi tu lakini huwezi kuupuuza,” alisema na kuongeza:

“Kwa sababu inadaiwa alikuwa anasumbuliwa na saratani ya koo na ukichunguza unaweza kusema pengine ni kweli kwa sababu siku zote Rais Mutharika akitoa hotuba yake kwa wananchi alikuwa anaongea kwa muda wa kati ya dakika 10 au 12 na si zaidi ya hapo. “Uvumi huo unadai kuwa baada ya mkutano wa UN kumalizika inasemekana alifanyiwa upasuaji wa koo, upasuaji huo umefanywa siri na Serikali iko kimya mno na watu wa Malawi wanapoendelea kuhoji Serikali inawaambia itawakamata. Unajua Malawi bado kuna ile hali ya Ukamuzu Banda.”

Ofisa huyo mwandamizi aliendelea kusema kuwa hali hiyo imezidi kuleta sintofahamu na inadaiwa imesababisha Kamati Kuu ya Chama cha Democratic Progressive (DPP) kutaka kubadilisha Katiba ya nchi hiyo ili Makamu wa Rais, Saulos Chilima, asimrithi Rais Mutharika kama atafariki dunia.

“Wazee wa chama tawala cha DPP wanadaiwa kutaka kuanzisha zengwe ili makamu wa rais asimrithi Rais Mutharika, kama zengwe la wakati ule alilofanyiwa Joyce Banda ili asimrithi Rais Bingu Mutharika alivyofariki dunia.

“Ndivyo wanavyotaka kumfanyia makamu wa sasa ambaye ni kijana na mchapakazi kweli kweli ambaye anaungwa mkono na watu wengi. Wazee hao hawamtaki kijana huyo, kwanza wanasema hatoki katika kabila la Mutharika kwa sababu yeye ni Mchewa. “Kwa kweli hilo jambo hata mimi nashangaa kwamba kwanini wafanye hivyo sasa hivi, makamu huyo ni kijana mdogo na Rais Mutharika alimteua kutoka katika shirika moja la simu la nchi hiyo.”

Taarifa za Rais Mutharika kutoweka zimezua taharuki kwa muda wa mwezi mzima sasa nchini humo, lakini hakukuwa na taarifa zozote kwa wananchi wa Malawi, jambo lililosababisha kuanzishwa kampeni maalumu ya ‘BringBackMutharika’ yenye lengo la kutaka taarifa sahihi juu ya afya yake.

Katika hatua nyingine, taarifa zenye utata ziliibuka na kusababisha maelfu kuamini kuwa Rais Mutharika huenda hayupo duniani. Baadhi ya vyombo vya habari vikiwamo Redio ya Power FM ya Afrika Kusini ilidai kuwa na taarifa za kifo. Si redio hiyo peke yake bali magazeti mbalimbali na mitandao yalitoa taarifa za kutatanisha huku Serikali ya Malawi ikishindwa kueleza ukweli.

Hata hivyo, maelfu ya wananchi wa Malawi hawajaridhishwa na majibu ya Serikali yaliyotolewa na Wizara ya Habari.

 WASHINGTON POST

Juzi, gazeti la Washington Post la Marekani liliandika katika mtandao wake taarifa za kutoweka kwa Rais Mutharika kueleza hajulikani alipokuwa mara ya mwisho hivyo kuzua hofu ya kifo chake.

“Wananchi wa Malawi wanamkosa rais wao, hajulikani alipo na wengi wanaamini huenda amefariki dunia. Lakini Serikali imeshindwa kukidhi haja ya wananchi kueleza ni mahali gani alipo, anafanya nini na kama mgonjwa au la, licha ya kuaminika kuwa yuko nchini hapa (Marekani) akipatiwa matibabu kutokana na kusumbuliwa na maradhi.

“Licha ya wiki hii msemaji wa Serikali kutoa taarifa ya kukanusha kuwa si mgonjwa, hivyo ana afya njema. Tangazo la pili la Serikali linatarajiwa kutolewa Jumapili (leo) ikiwa na maana Rais Mutharika alikuwa nje ya nchi kwa muda wa mwezi mmoja.”

HUFFINGTON POST

Oktoba 13, mwaka huu gazeti la Huffington Post liliandika: “Malawi wamtafuta rais wao, hawajui mahali alipo.”

Gazeti hilo lilisema kuwa hofu imetanda nchini humo huku wananchi wakijaribu kutafuta mahali alipo kiongozi wao.

 THE ECONOMIST

Kwa upande wake, Oktoba 11, mwaka huu Gazeti la The Economist liliandika kichwa cha habari cha ‘Rais wa Malawi atoweka.’

Gazeti hilo liliandika na kuongeza kuwa: “Viongozi kutoka Bara la Afrika kukimbilia matibabu katika nchi za Magharibi si jambo la kushangaza, hivyo kutoonekana kwao hadharani linaweza kulingana na wanavyokwenda kufuata matibabu katika hospitali nzuri na huduma maridadi. Hisia hizo ndizo zimechangia wananchi wa Malawi kuamini rais wao ni mgonjwa.

“Rais huyo aliwasili mjini New York Septemba 16, hajasikika tena tangu kumalizika mkutano wa UN mnamo Septemba 26, hivyo watu wanaamini amefariki dunia, lakini Serikali haisemi.”

Pia liliongeza kuwa wananchi wanahofia hilo kutokana na uzoefu walioupata katika kifo cha Rais wa zamani wa nchi hiyo, Profesa Bingu ambaye ni kaka yake Rais Mutharika. Wananchi wanakumbuka mwaka 2012, Profesa Bingu alifariki dunia baada ya kupata matibabu mara kadhaa bila mafanikio.

Oktoba 9, mwaka huu Serikali ya Malawi ilikanusha taarifa za kifo kwa kusema:

“Rais Mutharika yuko katika afya njema, anaendelea vema na majukumu yake nchini Marekani.”

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Malawi, Boniface Dulani, aliliambia The Economist kuwa haijalishi Mutharika awe mgonjwa au vinginevyo au yuko mapumzikoni na watoto wake watatu wanaoishi nchini Marekani, lakini ni lazima Serikali izingatie uwazi juu ya hali yake badala ya majivuno ya kimamlaka.

“Nchi yetu (Malawi) ina kiongozi mwenye umri mkubwa sana, lakini si sisi pekee bali Algeria wanaye Rais wao, Abdelaziz Bouteflika mwenye umri wa miaka 79. “Huyo anatembelea kiti, anaugua ugonjwa wa kiharusi tangu mwaka 2013. Paul Biya, Rais wa Cameroon ana miaka 83, alitumia muda mwingi akipewa matibabu nchini Uswisi. Rais wa Zimbabwe (Robert Mugabe) ana umri wa miaka 92, alidhaniwa kufariki alipokuwa huko Dubai, hata aliporejea aliwatania waandishi wa habari kuwa; ‘Ni kweli nilikufa, ila kila wakati narudishwa kuongoza,” alisema Dulani.

NYASA TIMES

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Malawi, Idriss Nassah, aliripotiwa mfululizo na gazeti la Nyasa Times mnamo Oktoba 11, 12, 13 na 14, mwaka huu akihoji Rais Mutharika yuko wapi?

“Niliandika barua kwa Katibu Mkuu wa UN na kwa Rais Barack Obama wa Marekani. Nilimwandikia pia Rais wa Rwanda (Paul Kagame), Uganda (Yoweri Museveni), Afrika Kusini (Jacob Zuma) na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (Dk. Dlamini Zuma) kuwaomba pengine walifahamu mahali alipo Rais Mutharika na kutaka watuambie walipokutana na Mutharika walipanga jambo gani wakiwa mkutanoni mjini New York.

“Pia niliandika barua kwa Meya na Mkuu wa Polisi wa New York, mahali ambako Mutharika alikuwapo kwa mara ya mwisho. Lengo lilikuwa kufahamu nini kilichotokea kwake au kama kulikuwa na lolote lilitokea hivyo wakaamuru ahifadhiwe. Nimefanya mahojiano na BBC, Sauti ya Amerika na Redio Power FM ya Afrika Kusini kuelezea wasiwasi wa wananchi kumkosa rais wao kwa muda wa mwezi mmoja.”

Kwa mujibu wa Msemaji wa Rais Mutharika, Mgeme Kalilani, Mutharika alikuwa akihudhuria shughuli za kiserikali. Hata hivyo, Gazeti la The New York Times liliripoti kuwa Bunge la Malawi liliitaka Serikali kueleza ukweli juu ya hali ya Rais Mutharika kwa kuwa anatumia gharama kubwa nchini Marekani na wananchi wanatakiwa kufahamu.

Akijibu swali hilo aliloulizwa na gazeti hilo, Msemaji wa Wizara ya Habari nchini Malawi, Malison Ndau, alisema: “Rais Mutharika anaendelea vema, hana tatizo la kiafya. Tuache kusambaza tetesi zisizo na maana yoyote. Tutawachukulia hatua wote wanaoeneza taarifa potofu.”

MUTHARIKA HAAMINIKI

Licha ya kutoweka nchini mwake kwa muda wa mwezi mmoja, ripoti zinasema kuwa wananchi wake hawamwamini Rais Mutharika. Kwa mujibu wa Ripoti ya Afrobarometer ya mwaka 2014, wananchi wa Malawi wana kiwango kidogo cha imani kwa Rais Mutharika pamoja na vyombo vya Serikali yake. Inaelezwa huenda ikawa moja ya sababu ya Rais Mutharika kutotoa taarifa zozote juu ya kutoweka kwake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,606FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles