25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Prof. Mkumbo: Mkopo wa Dola Bilioni 2.5 hauna masharti ya Rasilimali

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Serikali imeweka wazi kuwa mkopo wa Dola Bilioni 2.5 ambao Tanzania imepata kutoka Korea ya Kusini hauna masharti ya kuweka rehani rasilimali za nchi.

Hayo yamebainishwa leo Juni 6, 2024 Ikulu jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amebainisha kuwa taarifa zinazosambaa mtandaoni kuhusu kupeana bahari na madini si za kweli.

Amesema mkopo huo utakuwa na faida kubwa kwa nchi na siyo mkopo wa kwanza kutoka Korea kwani walikopa bilioni 1 mwaka jana, na sasa jumla ni bilioni 2.5. Mkopo huo ni wa miaka 40 na riba ya asilimia 0.01, na malipo yataanza mwaka wa 26.

“Kukopa ni muhimu kwani ni moja ya nyenzo za kujenga uchumi wetu na uwezo wa serikali kutoa huduma kwa wananchi. Muhimu ni kuelewa masharti ya mkopo na matumizi yake,” amesema Profesa Mkumbo.

Amesema mkopo huo utaelekezwa kwenye sekta za uzalishaji, siyo kununua magari au kulipa mishahara.

Katika ziara hiyo, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alijifunza mbinu mbalimbali za kuvutia uwekezaji kutoka Korea, huku Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, akisema walijifunza mengi kuhusu maendeleo ya sekta ya habari na teknolojia ya miundombinu kutoka Korea, huku akigusia kuwa mchakato wa Tanzania kuwa na setelaiti yake unaendelea vizuri na utaboresha huduma za mawasiliano.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, amesema Tanzania inahitaji kujifunza kutoka Korea ili kuzalisha bidhaa za viwango vya juu na kuingia katika masoko ya kimataifa.

Upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, amesisitiza juu ya umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kutafuta mitaji, masoko na maarifa ya maendeleo.

“Tunapozungumza na nchi nyingine, tunatekeleza sera ya nchi ya mambo ya nje. Dunia ya sasa inahitaji ushirikiano na ushindani na viongozi wanapaswa kutafuta washirika wa kushirikiana nao,” amesema Makamba na kuongeza kuwa kutokujifungia ndani ya mipaka ni muhimu kwa maendeleo ya ndani na ya kimataifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles