Na Ramadhan Hassan, Dodoma
WAZIRI wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali imetenga Sh bilion 2.2 kwa ajili ya kuandaa mbegu za alizeti ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa mafuta nchini ambapo amedai mbegu hizo zitauzwa kwa Sh 3,500 kwa kilo.
Akizungumza leo Oktoba 23,2021 jijini Dodoma wakati akizindua zoezi la ugawaji mbegu bora za alizeti zinazozalishwa na wakala wa Taifa wa uzalishaji na uendelezaji wa mbegu za kilimo (ASA), Waziri Mkenda amesema Serikali imejipanga kuondoa tatizo la uhaba wa mafuta nchini kwa kutoa mbegu nyingi kwa wakulima.
Waziri Mkenda amesema wamekuwa wakikabiliana na changamoto ya bei ya mafuta kupanda mara kwa mara ambapo amedai Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha mbegu za alizeti zenye ubora zinapatikana ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Amesema baada ya uchambuzi wameona kwamba sekta binafsi iendelee kuingiza mbegu za alizeti lakini changamoto imekuwa ni bei kuwa kubwa.
Waziri Mkenda amesema Serikali imetenga sh bilioni 2.2 kwa ajili ya kuandaa mbegu za alizeti ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa mafuta .
Amesema watatoa tani 1,600 ambapo amedai wanataka kufikia tani 2,000 na baadae mpaka tani 5,000 huku akidai  bei kwa  Kilo moja itakuwa ni Sh 3,500.
“Mbegu hizi zitakuwa zinapatikana katika halmashauri na kwa bei rahisi ili kuokoa fedha zinazotumika kwa ajili ya kununua mafuta, “alisema Profesa Mkenda.
Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha mwakani hawaagizi tena mbegu nchini nakwamba wameteua mikoa mitatu ambayo italima alizeti chini ya usimamizi mzuri ili yaweze kuzalisha mbegu za alizeti.
Amefafanua zaidi kuwa Mikoa hiyo na wilaya zake wamegawana ekari kwa ajili ya kulima zao hilo katika mikoa hiyo.Â
Profesa Mkenda pia aligawa  mbegu kwa wakuu wa wilaya ambapo zitapelekwa katika halmashauri kwa ajili ya kwenda kuwauzia wananchi ambao ni wakulima.Â
Vilevile amesema wameongeza fedha za mafunzo kwa maafisa ugani na mabwana shamba ili waweze kuwapa maelekezo mazuri wakulima.Â
Kwa upande wake,Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Fatma Mganga Amesema wametenga ekari 800,000 kwa mkoa wa Dodoma ambapo kila Wilaya itapata ekari zake kwa ajili ya kupanda mbegu hizo.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Bahi ambae alimwakilisha Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka,Mwanahamisi Mkunda alimhakikishia Waziri wa Kilimo kuwa mbegu hizo zitatunzwa vizuri na wakulima wote watazipata Â
Naye, Mwenyekiti wa Wakulima Nchini akizungumza kwa niaba ya wakulima, Stephen Marriale ameishukuru serikali kwa kupunguza bei za alizeti pamoja na kuwajali wakulima wa zao hilo.