Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, amesema sekta ya utalii nchini inakua kwa kasi.
Amesema hiyo inatokana na mazingira ya mapokezi wanayopata watalii katika hoteli mbalimbali na sehemu nyingine zenye vivutio vya utalii.
Hayo aliyasema Dar es Salaam jana baada ya kukabidhi vyeti vya kutambua hadhi za hoteli zilizopo na kuzipa madaraja mpaka nyota tano katika soko la utalii nchini.
Alisema mwaka jana watalii milioni 1.2 waliingia nchini Tanzania huku Kenya ikiwa ni milioni 1.3 na nchi nyingine za Afrika Mashariki zikiwa na watalii wadogo zaidi hivyo kuifanya Tanzania kuendelea kujivunia na kuboresha mazingira zaidi.
Alisema biashara ya hoteli inachangia pato la taifa kwa asilimia 25 hivyo ni muhimu katika kuongeza pato la Taifa kwa kuvuta watalii zaidi nchini.
Akigawa vyeti vyenye hadhi ya nyota tano aliitaja Serena kuwa na nyota tano na vigezo vilivyotumika.
Waziri alisema vimetumika vigezo vya usafi wa mazingira kwa kutotiririsha maji machafu ovyo na huduma nzuri.
Alizitaja hoteli nyingine zilizoshika namba nne kuwa ni Ramada Hotel na Double Tree . Nyota tatu ni Land Mark , Coral beach, Ramada ya Posta, Peninsula na Holday Inn.
Nyota tatu nyingine ni Saphire, Millenium Tower, Regency Park, Tiffany, Slip way, Tanzanite na Golden Tulip hotel.
Baadhi ya hoteli zenye nyota mbili ni Shamool Hoteli ,City style Mbezi Garden .
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania (TCT), Abdulkadir Mohamed, alisema sifa hizo zimezingatia viwango vya Afrika Mashariki.
Aliwataka wamiliki wa hoteli kuendelea kutoa huduma bora zaidi na zaidi kuvutia watalii zaidi.