27 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi kuanza kufanya doria kwa helkopta

Nora Damian -Dar es salaam

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema kuanzia leo litaanza kutumia helkopta kufanya doria maeneo mbalimbali ya jiji kuhakikisha mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) unafanyika kwa amani.

Hadi sasa jeshi hilo linavishikilia vyombo vya moto 126 zikiwamo pikipiki 87, bajaji 13 na magari 26 yenye ving’ora na taa zenye kuleta usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema wamejipanga vizuri kuweka mazingira rafiki na salama kwa ujio wa viongozi mbalimbali wa kimataifa.

“Tunaendelea kushirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama kuhakikisha jiji letu ambalo limepata heshima ya kusimamia ugeni huu, linakuwa salama na wageni wanapokewa kuanzia uwanja wa ndege hadi watakakofikia wakiwa wanasindikizwa.

“Bila amani mambo hayawezi kwenda vizuri, ndiyo maana tunafanya kazi usiku na mchana, tunataka wageni ambao wamekuwa wakisikia Tanzania ni kisiwa cha amani waje wathibitishe wenyewe,” alisema Mambosasa.

Alisema ili kuimarisha ulinzi katika mkutano huo, askari 300 wameongezwa na kusambazwa maeneo mbalimbali ya jiji ambako wamekuwa wakifanya doria za polisi wa miguu, pikipiki, mbwa na farasi.

Kuhusu vyombo vya moto vilivyokamatwa, alisema wahusika wanashikiliwa na taratibu nyingine za sheria zinafuata kwa kuwafikisha mahakamani.

“Katika hili Watanzania wasije kunisumbua habari ya huruma huruma kuomba waachiwe, hatuna nia mbaya, lakini haya ni maelekezo halali, hivyo ni lazima yafuatwe na yana nia njema.

“Anayetaka kwenda kinyume tutamrudisha kundini, tunataka kila mmoja ajivunie kutii sheria za nchi bila kusubiri kushurutishwa,” alisema.

Alifafanua kuwa kabla ya kuzuia pikipiki kuingia katikati ya jiji wakati wa mkutano huo, walifanya utafiti na kubaini kundi hilo ni korofi kwani limekuwa haliheshimu alama na sheria za usalama barabarani.

Katika hatua nyingine, Kamanda Mambosasa alisema barabara kadhaa za jiji zitafungwa kutokana na mkutano huo, lakini ni zile ambazo kutakuwa na ulazima wa kufanya hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles