Ramadhan Hassan -Dodoma
JESHI la Polisi jijini Dodoma, limekamata magari 17 yakiwa yanatumia kadi na file za magari mengine yaliyopata ajali.
Jeshi hilo limesema yapo magari wahusika wamekata chassis na kuunga kwenye magari mengini huku mengine wakiongeza na kubadilisha baadhi ya namba au kubandika vibati vya magari mengine.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alisema magari hayo yamekamatwa katika msako uliofanywa Mei 19 hadi 22 mwaka huu kwa ushirikiano wa Jeshi la Polisi kutoka mikoa mitano ambayo ni jirani na Jiji la Dodoma.
Kamanda Muroto alisema magari hayo yamekutwa na makosa ya kutumia kadi na file za magari mengine yaliyopata ajali.
“Pia wameyakata chassis kwa kufuta baadhi au kuongeza au kubadilisha baadhi ya namba au kubandika vibati vya magari mengine,”alisema Kamanda Muroto
Pia alisema kati ya magari hayo, gari namba T,864 CQA Toyota IST ilikuwa na chassis namba iliyokatwa na kuungwa na kibati kingine, pamoja na vioo kufutwa na kuandikwa namba nyingine.
“Gari hii ni ya wizi limebambikizwa namba na Card ya gari lingine,”alisema Kamanda Muroto.
Pia alisema wanalishikilia gari namba lenye namba za usajili T.680 BWU aina ya Toyota Prado lenye Chassis Namba RZJI 200626277 na Engine namba 3RZ3204070 lakini inatumia usajili wa Card na file la gari lingine.
Pia, alisema wanalishikilia gari namba T 237 DSJ aina ya Subaru ambalo ni Transit (IT) lilokuwa likisafirishwa kwenda Uganda na Dereva alipakia abiria wawili Misugusugu Pwani ambao walikuwa wakienda Kahama Shinyanga.
“Lakini matoke yake dereva alitishiwa silaha na kuporwa gari huku wakimwacha wamemfunga kamba na kutupwa porini eneo la Pandambili wilayani Kongwa.
Kamanda Murroto alisema wamefanya ufuatiliaji kwa kushirikiana na wenzao wa Pwani na kufanikiwa kulikamata huko Kiwanga Bagamoyo Pwani likiwa na namba bandia na watuhumiwa sita wamekamatwa.
“Pia tunalishikilia gari T.578 DBU Toyota Axio yenye Chassis namba VZT240-5016540 Engine no INZ16540, gari imebatizwa namba za gari lingine na linatumia nyaraka zisizo zake ni za gari la wizi,”alisema.
Kamanda Muroto alisema gari lingine ambalo limekamatwa lina namba za usajili T.380 AGP Toyota Chaser lililotelekezwa.