24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Pluijm asema ni fainali

hans-van-der-pluijm-kocha-wa-yanga_n6yuvorbr0jr1mq58mnv76j3oNA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Van der Pluijm, amesema anauchukulia mchezo wao wa kesho dhidi ya Tanzania Prisons kama fainali kwani unahitaji nguvu, umakini mkubwa, kujiamini ili kutimiza mafanikio ya ushindi.

Yanga inashikilia nafasi ya kwanza katika msimamo wa ligi hiyo, huku ikiwa imepoteza mchezo mmoja katika michezo 16 ambayo imecheza hadi sasa ikifanikiwa kuwa na pointi 39.

Hata hivyo, Yanga imefanikiwa kubaki nafasi hiyo baada ya Azam iliyoko nafasi ya pili ambayo ina mchezo mmoja mkononi kwa kuwa imecheza michezo 15 kuwa nje kwa ziara ya michezo ya kirafiki na ina pointi 39. Tanzania Prisons yenye pointi 27 inahitaji pointi tatu hizi ili kufikisha pointi 30 na kujiweka vizuri katika msimamo wa ligi.

Akizungumza na MTANZANIA, Pluijm alisema wanatambua si rahisi kupata ushindi katika uwanja huo wa Sokoine, ila watajitahidi kuweza kuondoka na pointi tatu katika mchezo huo.

Kikosi cha Pluijm kinakabiliwa na majeruhi ambayo yameathiri safu yake imara ya ulinzi baada ya kuumia nahodha wa timu hiyo na beki wa kati, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Haji Mwinyi na ile kadi nyekundu aliyoipata Kelvin Yondani katika mchezo dhidi ya Coastal Union wikiendi iliyopita.

Kocha huyo raia wa Uholanzi alisema pamoja na kupata pigo kwenye safu ya ulinzi kutokana na majeruhi hao, hawezi kumchezesha beki mkongwe, Cannavaro ambaye tayari ametolewa hogo (POP), kwani bado hajapona vizuri majeraha yake ya mguu, akifanya hivyo upo uwezekano wa kuendelea kumkosa katika mechi nyingine muhimu zinazofuata.

Alisema kwa sasa Cannavaro hawezi kucheza anaendelea na programu maalumu ya mazoezi ambayo ameanzia kwenye gym na baada ya kuridhika na maendeleo ya afya yake atamruhusu kujiunga na wenzake mazoezini.

Akimzungumzia beki Yondani ambaye alionyeshwa kadi nyekundu katika mchezo uliopita, Pluijm alikiri kuwa ni pigo kubwa ndani ya kikosi chake hasa kwa kipindi hiki ambacho wanakabiliwa na mechi ngumu mbele yao.

Alisema Yondani alitakiwa kucheza kwa utulivu na umakini wa hali ya juu kuliko kufanya jambo ambalo linaweza kuigharimu timu, hakupaswa kupaniki na changamoto alizokuwa akizipata kutokana na ushindani uliokuwepo kati yao.

“Tayari tumesahihisha makosa yetu, hivyo sifikirii kushindwa tena, pia tunatambua mzunguko huu wa pili kila mchezo kwetu ni zaidi ya fainali.

“Tunatarajia kucheza dhidi ya Prisons ya Mbeya, tayari tumeshawasili na tumeanza kufanya mazoezi asubuhi na jioni ili kujiweka tayari na mchezo, kwa sasa hatuangalii tuna pigo gani bali tunaangalia ushindi,” alisema.

Pluijm alieleza kipigo dhidi ya Coastal Union kimewafanya kuimarika zaidi, baada ya kufahamu makosa yao na kuwa tayari kuyasahihisha.

“Kila mchezo ni lazima tushinde na tutaufanya kama fainali ili kufikia lengo la kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara,” alieleza Pluijm.

Hata hivyo, mchezo huo umeonekana kuwa na hisia kubwa kwa mashabiki wa Yanga, ambao wamejipanga kuhakikisha timu hiyo inaondoka na ushindi.

Akizungumzia mchezo huo, shabiki Saleh Kupaza, alisema mchezo dhidi ya Yanga na Prisons ni mgumu kwani timu zote zimekuwa zikizihitaji pointi hizo tatu katika kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi.

“Mchezo wa Jumatano (kesho) ni mgumu kwani kila timu inahitaji pointi hizi tatu muhimu, ukiangalia ratiba ya Prisons ni ngumu kwani wakimaliza kibarua na Yanga, wanatarajia kukutana tena na mahasimu wao Mbeya City siku ya Jumamosi,” alisema.

Yanga wamewasili Mbeya juzi jioni na kuweka kambi ndani ya Jeshi la Wananchi 44KJ, Mbalizi nje kidogo ya mji na wanatarajiwa kufanya mazoezi katika Uwanja wa Sokoine jana jioni, huku Prisons wakiendelea kujifua ndani ya Uwanja wa Shule ya Sekondari Sangu.

Prisons imelazimika kuutumia uwanja wa shule hiyo kwa muda baada ya kupisha ukarabati wa kiwanja chao kilichopo ndani ya Jeshi la Magereza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles