29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

PAC: OSHA itumike kuainisha viwango vya usalama na afya katika ununuzi serikalini

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeishauri serikali kuutumia Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuainisha viwango vya usalama na afya katika samani na vifaa mbali mbali vya ofisi kabla ya manunuzi kufanyika ili kuepuka kununua samani na vifaa visivyokidhi viwango stahiki.

Mkurugenzi wa Mafunzo, Takwimu na Uhamasishaji wa OSHA, Joshua Matiko akiwasilisha mada ya makundi mbalimbali ya vihatarishi vya maeneo ya kazi na namna ya kuvidhibiti kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) katika Semina maalumu iliyofanyika bungeni jijini Dodoma.

Ushauri huo umetolewa mara baada ya Kamati hiyo kupatiwa semina ya masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi iliyotolewa na wataalam wa OSHA wakiongozwa na Mtendaji Mkuu, Khadija Mwenda.

Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka, amesema kupitia semina hiyo, wameweza kubaini kuwa samani na vifaa mbali mbali visivyozingatia viwango vya usalama na afya vimeendelea kununuliwa katika majengo na ofisi za serikali licha ya kuwepo kwa Taasisi ya OSHA ambayo ingeweza kutoa ushauri juu ya viwango stahiki.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka (Mb) akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya PAC mara baada ya mtendaji Mkuu wa OSHA kuhitimisha mada aliyowasilisha mbele ya Kamati hiyo.

Aidha, Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa OSHA inapaswa kushirikishwa kikamilifu katika miradi ya ujenzi wa majengo ya serikali hususan katika Mji wa Serikali unaoendelea kujengwa katika eneo la Mtumba Jijini Dodoma ili ujenzi huo uweze kuzingatia uwepo wa miundombinu rafiki kwa ajili ya kulinda afya na usalama wa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla.

“Tumeishauri Taasisi yetu ya OSHA kwenda kwenye Taasisi zote za serikali na mashirika ya umma kuwaeleza kuhusiana na umuhimu wa kununua samani na vifaa vinavyozingatia afya na usalama kwa wafanyakazi ili kuepuka hasara inayoweza kusababishwa na ununuzi wa samani na vifaa visivyokidhi viwango stahiki katika kulinda afya na usalama wa watumiaji wake,” ameeleza Mwenyekiti wa Kamati na kuongeza:

“Imekuwa ni muhimu kwa Kamati yetu kuwa na ufahamu wa masuala haya ya usalama na afya kwanza kama wawakilishi wa wananchi ambao tunawajibika kuwapa elimu wananchi wetu huko majimboni. Aidha, elimu tuliyoipata itatuwezesha kuishauri serikali kuhusiana na matumizi mazuri ya fedha za umma hususan katika kuimarisha afya na usalama wa wafanyakazi nchini,” amesema Kaboyoka.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo wameeleza umuhimu wa semina hiyo kwa wanakamati.

“Tumepata fursa ya kupata wasilisho kuhusu kazi, sheria na miongozo ambayo OSHA wamekuwa wakitoa kwenye maeneo ya kazi lakini nikiri kwamba kwa nchi kama yetu inayopambana kukuza uchumi wake, tunawahitaji sana OSHA ili waweze kutoa miongozo ya uzalishaji unaozingatia viwango vya usalama na afya jambo ambalo litawezesha bidhaa zinazozalishwa kuwa katika ubora unaokubalika hata katika masoko ya kimataifa,” amesema Anatropia Theonest, Mjumbe wa Kamati.

Kwa upande wake, Mjumbe Venant Protas, ameipongeza OSHA kwa maboresho ambayo imeendelea kuyafanya katika utendaji wake:

“Mwaka jana OSHA walifika mbele ya Kamati yetu na tukawashauri kufanya maboresho kadhaa ambayo wameyafanyia kazi. Miongoni mwa mambo waliyoyaboresha ni kujiunganisha na kuwa na mawasiliano mazuri na Taasisi nyingine za umma,” amesema.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema Taasisi yake ipo katika nafasi nzuri ya kutekeleza ushauri uliotolewa na Kamati kutokana na serikali kuridhia kujumuishwa kwa masuala ya usalama na afya katika kanuni za utumishi wa umma na kuandaa miongozi ya utekelezaji wake.

“Tunakwenda kufuatilia na kuhakikisha kwamba miongozi ya usimamizi wa masuala ya usalama na afya katika sekta ya umma inasambazwa kwa wahusika wote na kufanyiwa kazi ipasvyo,” amemesema Mwenda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles