Johanes Respichius Na Teophil Mbunda (EHICO)
– Dar es Salaam
NA WAANDISHI WETU
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema linafanya operesheni ya kuwakamata wamiliki wa nyumba za kulala wageni wanaofanya biashara kinyume cha sheria.
Taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Kanda hiyo, Simon Sirro, ilisema wamebaini baadhi ya nyumba za kulala wageni zinatumika kuhifadhi magenge ya majambazi na wahalifu wengine.
Alisema nyumba hizo zimekuwa zikitumiwa na wanawake na wanaume wanaofanya biashara ya kuuza miili yao maarufu ‘dadapoa’ na ‘kakapoa’.
“Ni wajibu wa Polisi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye nyumba za kulala wageni, hoteli, migahawa, vilabu vya vileo, kumbi za starehe zinazokesha na zisizokesha na watakaobainika kuvunja sheria hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisema.
Katika hatua hiyo, Kamishna Sirro aliwatahadharisha wafanyabiashara wa nyumba hizo kufuata utaratibu wa kupokea wageni kwa kuandika majina yao kwenye vitabu, namba za vitambulisho vyao na sehemu wanapotoka na pale watakapomtilia shaka mteja yeyote watoe taarifa kituo chochote cha polisi.
Aidha wenyeviti wa Serikali za mitaa na wajumbe wa nyumba kumi wametakiwa kuwajibika na kuwatambua wageni wote wanaoingia kwenye himaya zao na kuwachukulia hatua stahiki kwa lengo la kuimarisha ulinzi ndani ya jiji la Dar es Salaam.
Hata hivyo Kamanda huyo aliwataka wageni wanaotoka mikoani kupuuza taarifa zilizoenea katika mitandao ya kijamii kuwa polisi wanawakamata watu wanaolala kwenye nyumba za kulala wageni mchana kwa kosa la uzembe na uzururaji.
“Taarifa hizo si za kweli na watu wanaotoka mikoani nawaomba waendelee na shughuli zao kama kawaida na wapuuzie taarifa hizo, “alisema Kamishna Sirro.