Serikali yatangaza msako wa majambazi

0
807

majaliwaNa MAREGESI PAUL

-DODOMA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amasema majambazi walioua polisi na raia katika maeneo mbalimbali nchini, watasakwa na kukamatwa ili wafikishwe katika vyombo vya sheria.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa msimamo huo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (CCM), wakati wa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu.

Katika swali lake, Ngonyani ambaye ni maarufu kwa jina la Profesa Maji Marefu, alitaka kujua Serikali inachukua hatua gani dhidi ya majambazi wanaoua polisi na raia wema katika maeneo mbalimbali nchini.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, hivi karibuni majambazi wameua wananchi na polisi wasiokuwa na hatia. Sasa nataka kujua, je Serikali inachukua hatua gani juu ya wahalifu hao,” alihoji.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Majaliwa alikiri uwepo wa majambazi hao na kusema hatua zinachukuliwa dhidi yao ili wananchi waishi salama.

“Ni kweli kuna Watanzania wameuawa Tanga, Mwanza, Vikindu na kwingineko tena wakiwamo askari wetu. Kwa hiyo, natoa pole kwa waliopoteza ndugu zao na Serikali inasikitishwa na vitendo na inawatoa hofu Watanzania wote.

“Kwa hiyo, tutawasaka waharifu hao popote walipo na kuwakamata kwani vyombo vya dola viko macho saa zote.

“Ulinzi utazidi kuimarishwa na nchi itaendelea kuwa salama ila wananchi wazidi kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa pindi wanapowaona watu wasiowafahamu katika maeneo yao,” alisema Waziri Mkuu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here