31.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 5, 2022

Contact us: [email protected]

‘Viongozi Afrika hawapendi kuwajibishwa’

ulimwengubc1Na ELIYA MBONEA

-ARUSHA

MWANDISHI wa habari mkongwe nchini, Generali Ulimwengu, amewakosoa wakuu wa nchi za Afrika akisema kuwa hawapendi kuambiwa wafuate Katiba, sheria wala utaratibu wa kuendesha nchi zao.

Alisema viongozi hao wakiamka asubuhi hupenda kufanya au kusema wanayotaka yafanyike, bila kujali yatanyima haki au kupoteza maisha ya watu wengine.

Hayo aliyasema mjini hapa kwenye mafunzo ya wahariri na waandishi wa habari wa nchi za Afrika yaliyoandaliwa na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) yenye makao makuu yake mjini Arusha.

Akizungumza baada ya kufunguliwa kwa mafunzo hayo na Rais wa AfCHPR, Jaji Sylvain Ore, aliyechaguliwa hivi karibuni, Ulimwengu alisema viongozi hao hawapendi suala lolote linalowataka wafuate sheria, Katiba na kanuni.

“Wakuu wa dola za Afrika hawataki kuwajibishwa. Hata ungesema ufute Mahakama ya Kimataifa ya ICC (The Hegue Uholanzi), kisha umlete Mwendesha Mashitaka Fatou Bensouda Mahakama ya Afrika ukiamini ni mwenzetu bado hawatakubali kuwajibishwa,” alisema Ulimwengu.

Alisema kwa miongo mingi nchi za Afrika tangu zilipopata uhuru, haki za watu zimekuwa zikikanyagwa, kupondwapondwa na kudharauliwa hatua iliyoibua mjadala wa kushughulikia watu, asasi au Serikali zinazovunja, kupokonya, kunyang’anya au kunyima haki za binadamu.

“Kumekuwa na mijadala mipana kwamba wapelekwe Mahakama ya ICC kushitakiwa au washughulikiwe hapa Afrika kwenye mahakama yetu?” alihoji Ulimwengu na kuongeza:

“Mara nyingi tunasema wenyewe kwamba hakuna sababu ya kwenda katika mahakama zilizoanzishwa na wazungu wakati tuna wataalamu wanaoweza kufanya kazi hizo.

“Sasa Mahakama ya Afrika ni jawabu la maswali haya kwamba inao majaji wa kiafrika wanaoweza kusikiliza kesi za Waafrika dhidi ya watawala wao pale wanapohisi wamefanyiwa jambo ambalo si la haki,” alisema Ulimwengu.

Hata hivyo, Ulimwengu alisikitishwa na viongozi hao waliopitisha na kuridhia kuanzishwa kwa mahakama hiyo kwa kushindwa kuipatia nguvu inayotakiwa kwa kutoa matamko yanayotakiwa ili kuwasukuma watu wa nchi za Afrika wawe na uwezo wa kwenda mbele ya Mahakama kuwasilisha malalamiko dhidi ya Serikali za nchi zao.

“Kwa hiyo ni jukumu lenu wanahabari kutoa taswira na kuionyesha mahakama hii ipo na inatakiwa kutumiwa. Na viongozi waipe nguvu ifanye kazi ili waache kulalamika wanapopelekwa ICC wakidai wanaonewa,” alisema.

Mwanahabari huyo alitolea mfano wa marehemu Mchungaji Christopher Mtikila, alivyoshinda kesi ya mgombea binafsi lakini bado Serikali ilimwekea kizingiti.

Mwandishi mwingine mkongwe, Salim Said Salim aliwataka viongozi wa Afrika kutambua kuwa wakati wa kutoa amri ili kuongoza nchi umemalizika.

“Tatizo la viongozi wa Afrika wanatawala kwa amri, jamani wakati wa kutoa amri umeisha, amri zimebakia kwenye Biblia na Qurani,” alisema Salim.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,586FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles