BEIJING, CHINA
OFISA wa zamani wa ngazi ya juu China, Wei Pengyuan, yupo hatarini kuhukumiwa kunyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kuficha dola za Marekani milioni 30 nyumbani kwake. Hukumu yake imeahirishwa.
Wei Pengyuan alikuwa ofisa mkuu aliyesimamia biashara ya makaa ya mawe China.
Mahakama mjini Baoding, kaskazini mwa China, imesema Wei alipokea rushwa alipokuwa akiidhinisha miradi ya makaa ya mawe.
Maofisa wa serikali walisema mashine nne za kuhesabu fedha ziliharibika walipokuwa wanajaribu kuhesabu fedha zilizopatikana nyumbani kwa ofisa huyo.
Maelfu ya maofisa wa serikali wameadhibiwa katika kampeni kubwa ya kukabiliana na ulaji rushwa China.
Kampeni hiyo ambayo inaungwa mkono na Rais Xi Jinping imesababisha kuadhibishwa kwa baadhi ya wapinzani wa siasa wa Rais Xi.