24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ofisa Benki ya NBC na wenzake sita kortini kwa utakatishaji fedha

Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam

Ofisa wa Benki ya NBC tawi la Mnazi Mmoja, Silvina Karugaba (46) na wenzake sita wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka 11 ikiwemo la utakatishaji wa Sh bilioni 4.7.

Ofisa wa Benk ya NBC tawi la Mnazi Mmoja Silvina Karugaba[46] na Wenzake sita wamefishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Wakikaliwa na Mashitaka 11 ikiwemo la utakatishaji wa sh bilion 4,7.

Mbali na Karugaba ambaye ni Mkazi wa Wazo, washitakiwa wengine ni Mkurugenzi Uendeshaji wa Kampuni ya Peertech, Baraka Madafu (39) Mkazi wa Goba, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Mark Mposo (40), Mkazi wa Kijitonyama, Meneja wa Fedha, Lusekelo Mbwele (39), Meneja Opereseheni, Leena Joseph (39) Mkazi wa Salasala na Mkaguzi wa Ndani wa kampuni hiyo,  Bernard Mndolwa (47) Mkazi wa Mwenge.

Akisoma mashitaka hayo Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Cassian Matembezi kuwa washitakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Desemba 4,2018 na Desemba 31,2020.

Wakili Simon alidai katika mashitaka ya kwanza kuwa kati ya Desemba 4,2018 na Desemba 31,2020 maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, washitakiwa kwa pamoja waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kufanya udanganyifu na kujipatia Sh 4,786,800,000 kutoka Benki ya NBC.

Alidai Februari 6,2019 maeneo ya Masaki, washitakiwa kwa pamoja na kwa lengo la kufanya udanganyifu walighushi nyaraka ya uongo kuonesha watu 60 ni wanufaika na ni waajiriwa wa Kampuni ya Peertech wakati wakijua sio kweli.

Pia alidai Februari 6, 2019 maeneo hayo ya Masaki washitakiwa hao kwa pamoja waliwasilisha katika benki ya NBC nyaraka ya uongo kuonesha watu hao 60 waliotajwa kwenye nyaraka hiyo kuwa ni waajiriwa wa kampuni hiyo na ni wanufaika wa mikopo wakati wakijua sio kweli.

Katika mashitaka ya nne, Wakili Simon alidai Agosti 30, 2019 maeneo hayo washitakiwa kwa pamoja walitengeneza nyaraka ya uongo kuonesha watu 11 waliotajwa kwenye makubaliano ni wanufaika na waajiriwa wa kampuni hiyo wakati wakijua sio kweli.

Inadaiwa Februari 30,2019 washitakiwa hao waliwasilisha nyaraka hiyo ya uongo katika benki ya NBC kuonyesha kuwa watu 11 ni waajiriwa jambo ambalo sio la kweli.

Simon alidai Februari 13, 2020 maeneo ya Masaki washitakiwa hao walighushi nyaraka za uongo kuonesha watu 20 ni wanufaika wa mkopo na kwamba ni waajiriwa wa kampuni ya Peertech wakati wakijua sio kweli.

Inadaiwa tarehe hiyo na maeneo hayo, washitakiwa waliwasilisha nyaraka hiyo ya uongo kwa benki ya NBC.

Wakili Kadushi alidai katika mashitaka ya nane kuwa washitakiwa kwa pamoja Februari 13,2020 maeneo ya Masaki Ilala, walitengeneza nyaraka uongo kuonesha kuwa wanahisa wa kampuni walipitisha azimio kwamba watu 20 watambulishwe katika benki ya NBC kama wafanyakazi wa kudumu jambo ambalo sio kweli.

Pia alidai kwa makusudi washitakiwa hao waliwasilisha nyaraka hiyo katika benki ya NBC kitendo ambacho ni kinyume na sheria.

Katika mashitaka ya 10, inadaiwa Desemba 4,2018 na Desemba 31,2020 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, kwa njia ya udanganyifu walijipatia Sh 4,786,800,000 kwa kuwasilisha nyaraka za uongo kuonesha watu 78 ni wafanyakazi wa kudumu kampuni ya Peertech na kwamba wamedhaminiwa kuchukua mkopo kupitia mkataba wa kampuni hiyo.

Katika mashitaka ya utakatishaji fedha, inadaiwa katika tarehe hizo kwamba washitakiwa wote walijipatia Sh 4,786,800,000 huku wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya kughushi na kujihusisha na genge la uhalifu.

Upande wa mashitaka walidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kukamilisha upelelezi.

Hakimu Matembele aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 12, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Katika hatua nyingine, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilidai kuwa  katika kipindi cha kati ya mwaka 2018 hadi 2020, kwa kutumia orodha ya majina ya watumishi hewa, Kampuni ya Peertech iliingia makubaliano na Benki za NBC, ABC na ABSA zote za jijini Dar Es Salaam, na kuweza kujipatia fedha kiasi cha Sh bilioni nane (8) kwa njia za kughushi.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo, alisema  orodha ya watumishi iliyowasilishwa katika benki hizo na kampuni ya Peertech kwa ajili ya kupatiwa mikopo, hawajawahi kuajiriwa wala kufanya kazi katika Kampuni ya Peertech Company Limited.

Alisema ili watuhumiwa waweze kufanikisha nia yao ovu, walitengeneza na kughushi mikataba, salary slips pamoja na vitambulisho vya kazi na kuziwasilisha nyaraka hizo katika benki hizo.

Vile vile, uchunguzi wa Takukuru umebaini kuwa, ili kufanikisha upatikanaji wa mikopo hiyo ya kughushi, Kampuni hii ya Peertech iliwasilisha nyaraka za kughushi kutoka benki za NMB, CRDB, GT Bank pamoja na BOA   zote za jijini Dar es Salaam.

Pia ilibainika katika uchunguzi huo ni kuwa, Kampuni ya Peertech iliwasilisha kadi za wapiga kura na vitambulisho vya Uraia ambavyo ni vya kughushi.

Kwamba, kati ya mwaka 2019 na 2020, kampuni hii kupitia waajiriwa wao waliotambulika kama Mohamed Kombo, Leena Francis pamoja na Benard Mndolwa  ambao walikuwa ndio watia saini  katika nyaraka za mikopo, iliwasilisha nyaraka za wafanyakazi 78 katika benki za NBC, wafanyakazi 40 katika benki ya ABC na wafanyakazi 22 katika benki ya ABSA kuonyesha kwamba watumishi hao ni waajiriwa wa kampuni ya Peertech Company Ltd huku wakijua si kweli.


Ilibainika pia kwamba, kutokana na kuwasilisha maombi hayo ya mikopo, jumla ya mikopo ya Sh bilioni 4.7, ilipatikana kutoka NBC, Sh bilioni 1.9 ilipatikana kutoka benki ya ABC na  mikopo ya Sh bilioni 1.3 ilipatikana kutoka benki ya ABSA na mikopo hiyo ilitolewa kwa wafanyakazi hewa 140 wa kampuni hiyo. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles