33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

ODINGA AJIAPISHA URAISI KENYA

  • Kalonzo, Watangula, Mudavadi waingia mitini

Nairobi -KENYA

BAADA ya wiki kadhaa za wasiwasi, hofu na mashaka miongoni mwa wafuasi wa upinzani wa National Super Alliance (NASA), hatimaye kiongozi wao Raila Odinga, jana aliapishwa kuwa ‘Rais wa Wananchi’ wa Kenya.

Tukio hilo lililofanyika kwenye Bustani ya Uhuru mjini Nairobi, baada ya awali kuahirishwa wakati wa Sikukuu ya Jamhuri Desemba 12, 2017 na kuwakasirisha wafuasi wa Odinga kiasi cha kumuita mwoga.

Mbele ya maelfu ya wafuasi wake, Odinga aliapishwa na Mbunge wa Ruaraka, Tom  Kajwang pamoja na aliyekuwa mgombea wa kujitegemea wa ugavana wa Nairobi, Miguna Miguna ambaye pia ni wakili.

Aliapishwa akiwa amevaa nguo nyeupe na kofia nyeusi kwa kushika Biblia ya rangi ya kijani katika mkono wake wa kulia.

“Mimi Raila Odinga, naapa kwamba nitalilinda Taifa kama Rais wa Wananchi, nitakuwa mwaminifu. Mungu nisaidie,” aliapa kwa memeno hayo Odinga.

Baada ya kiapo hicho aliweka saini katika nyaraka zilizotumika kumuapisha katika tukio ambalo halikuzidi dakika 10.

Hata hivyo, Odinga aliapa bila uwapo wa naibu wake Kalonzo Musyoka, ambaye ni kiongozi wa Chama cha Wiper Democratic Movement (WDM).

Vinara wengine wa NASA ambao hawakuonekana kwenye shughuli hiyo ni Musalia Mudavadi wa Chama cha Amani National Congress (ANC) na Seneta wa Bungoma, Moses Wetangula wa Ford Kenya.

Muungano huo wa upinzani umekuwa ukishikilia kutowatambua Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais, William Ruto.

NASA inapinga uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26, 2017 kwa madai kuwa matakwa yao hayakutimizwa huku ikisisitiza Odinga alishinda uchaguzi wa Agosti 26, 2017.

Akizungumza muda mfupi baada ya kula kiapo, Odinga aliwashukuru wafuasi wake kwa kujitokeza kwa wingi.

“Mamia ya maelfu ya raia wa Kenya wamehudhuria sherehe hii ili kusema kwamba wamechoshwa na wizi wa kura.

“Hii ni hatua ya kwanza katika kukabiliana na wizi wa kura. Nawashukuru raia wa Kenya kwa subira na ujasiri wao. Tukio hili linaashiria mwisho wa ukosefu wa haki katika chaguzi za Kenya,” alisema.

Akimzungumzia naibu wake aliyapaswa kuapishwa pamoja naye, alisema Kalonzo ataapishwa baadaye lakini hakueleza ni kwa nini hakuhudhiria.

Haijulikani atakachofanya Odinga baada ya kuapishwa ikizingatiwa Kenya ina Rais na Naibu wake.

Hali ilivyokuwa uwanjani

Wafuasi wa Odinga kutoka maeneo mbalimbali yikiwamo Mombasa, Kisumu na Machakos  walianza kufurika katika uwanja huo kabla ya saa mbili asubuhi.

Kwa kile kilichoonekana kama hofu ya uwezekano wa kutokea machafuko, shughuli za usafiri na biashara mijini hazikuwa nyingi ikilinganishwa na siku za kawaida.

Katika Barabara ya Uhuru inayopakana na bustani hilo, baadhi ya vijana walichukua kazi ya askari trafiki kuelekeza magari kwa vile hakukuwa na polisi yeyote.

Hatua hiyo ni kinyume na msimamo wa awali wa serikali iliyokuwa imewaamuru polisi kulinda bustani hiyo na kuhakikisha hakuna shughuli zozote zinazoendelea kwenye eneo hilo.

Awali majira ya jana asubuhi, askari wa kutuliza ghasia (GSU) waliokuwa wameweka kambi eneo la Uhuru Park waliamriwa kuondoka.

Serikali ya Kaunti ya Nairobi ilikuwa imepiga marufuku hafla yoyote kufanyika katika bustani hiyo kwa madai kuwa ilipanga kuikarabati.

Kadhalika, Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nairobi, Japheth Koome mwishoni mwa wiki alitangaza kuwa maafisa wa polisi hawataruhusu hafla hiyo ya Nasa kufanyika Nairobi kwa sababu ingezua ghasia.

Baada ya kutokuwepo kwa kizuizi chochote wafuasi wa Odinga walikuwa wamafurika uwanja mzima majira ya saa nne asubuhi  huku mabasi ya abiria yakiendelea kusomba wengine.

Wengi walionekana wenye furaha huku wakiimba nyimbo za kuusifu muungano wa NASSA.

Awali kulikuwa na sintofahamu baada ya kufikia saa 8.30 mchana bila ya kuonekana kwa viongozi wa NASA isipokuwa kikundi cha wabunge na maseneta.

NASA ilikuwa imetangaza kuwa tukio hilo lingekamilika kufikia saa 7 mchana. Mwelekeo huo ulikuwa umeibua matumaini kwa Jubilee kuwa tukio hilo halipo huku wale wa NASA wakiwa na wasiwasi.

Kalonzo awachefua NASA

Kukosekana kwa Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula kwenye hafla hiyo kulionekana kuwadhaisha baadhi ya wafuasi wao.

“Tumefadhaishwa na kutojitokeza kwa vinara hasa Kalonzo. Hata hivyo tunashukuru hatimaye ‘Baba’ amelishwa kiapo na kuwa ‘rais wa wananchi’,” alisema Maurice Mukhwana aliyekuwa amesafiri kutoka Kakamega.

Mfuasi mwingine wa NASA, Jared Omondi kutoka Migori alisema;  “Nimesikitishwa sana na vitendo vya vinara wengine hasa Musyoka kwa kumwangusha Baba (Odinga). Kamwe sitawaamini kama viongozi.”

Wakati upinzani ulipoahirisha hafla ya kuapishwa Odinga, Desemba 12 mwaka jana ilieleza kuwa ni kwa sababu ya kusubiriwa kwa Kalonzo aliyekuwa Ujerumani akimuuguza mkewe.

Kalonzo alaani vyombo vya habari kufungiwa

Saa chache kabla ya tukio hilo la kuapishwa kwa Odinga, Kalonzo alilaani Mamlaka ya Mawasiliano (CA) kwa kufunga matangazo ya televisheni wakati Wakenya walikuwa wakisubiri haki yao kushuhudia tukio hilo,

Kalonzo aliongeza kuwa dunia ilikuwa ikitarajia tukio la Uhuru Park na kwamba alikuwa njiani kwenda kujadiliana na vinara wenzake namna ya kukabiliana na kitendo kilichofanywa na Mamlaka ya Mawasiliano (CA).

“Hatuelewi mshtuko huu hivyo tunajadiliana bado na tutawafahamisha. Tunatarajia kulijadili suala hili kwa sababu dunia inalisubiri. Huwezi kulifanikisha ipasavyo kukiwa na mfungo mzima namna hii.

“Hivyo, ndio basi nasema ni lazima tuangalie mambo haya, tunazumgumza, tunajaribu kuelewana kwa sababu CA imefanya vibaya kufunga mawasiliano, hatujui kama sasa watazima na simu zetu na hivyo kusababisha kuchelewa chelewa,” alisema Kalonzo.

NASA ilipuuza maonyo

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Githu Muigai aliwaonya viongozi wa NASA kuwa kuwaapisha viongozi wao ni kitendo cha uhaini ambacho adhabu yake ni kifo.

Lakini NASA ilipuuza onyo la Muigai ikisisitiza kuwa kipao hicho ni kwa mujibu wa sheria.

Baadaye, Odinga alikaririwa kuwa yuko tayari kufa iwapo kuapa kunalipa katika mapambano ya upatikanaji wa haki za chaguzi.

Alisisitiza kuwa ni lazima aapishwe na aliyashutumu mataifa ya kigeni kwa kumtishia kufuta nyaraka zake za kusafiria.

Odinga abadili akaunti ya Twitter

Katika hatua nyingine, muda mfupi baada ya kuapishwa, wasaidizi wake waliibadili akaunti yake ya Twitter na kusomeka,  Hii ni akaunti rasmi ya Mheshimiwa Raila Amolo Odinga, Rais wa Jamhuri ya Kenya.’

Akaunti ya Rais Uhuru Kenyatta haina madoidoi mengi zaidi ya kusomeka, ‘Rais wa Jamhuri ya Kenya.’

Akaunti hiyo ya Odinga inatarajia kuibua maswali juu ya tafsiri yake na matumizi yake kama rais kama ilivyo kwa uhalali wa kitendo chake cha kuapa ilhali kuna Rais mwingine madarakani.

Aandika ujumbe Twitter

Odinga pia aliandika ujumbe kuwashukuru watu wa Kenya kwa mamlaka waliyoipatia NASA na kwa Imani waliyoionyesha.

“Mlikuja kutoka kona zote za jamhuri kushuhudia kuapishwa kwangu na ilipendeza kuwaona mkiwa mmejitokeza kwa mamilioni,” aliandika ujumbe huo jana jioni.

Vituo vya Runinga vyafungiwa matangazo

Jana, saa nne asubuhi Mamlaka ya Mawasiliano (CA) ilivizima vituo vya tekevisheni vya vya  NTV, Citizen TV na KTN News.

Odinga kabla ya kuelekea uwanja wa Uhuru kuapishwa alisema hakutarajia kufungiwa kwa vyombo vya habari.

Alisema hali hiyo inasikitisha na inaonesha kuwa kufikia kiwango cha Uganda.

Mbunge wa Suba, John Mbadi naye alishutumu vikali hatua ya Mamlaka ya Mawasiliano (CA) kuzima runinga ya Citizen, pamoja na vituo vyake vya runinga na redio vilivyo chini ya Shirika la Habari la Royal Media Services (RMS).

RMS inamiliki vituo kadhaa vya redio, ikiwamo Redio Citizen, Ramogi FM, Muga FM, na hurusha habari na matangazo kwa lugha asili ya Kikuyu.

Kadhalika, hatua hiyo imeathiri runinga ya NTV inayomilikiwa na Nation Media Group (NMG) ambapo watazamaji hawakuweza kufuatilia habari na matangazo yake kupitia mfumo huru kama vile Signet, ADN na BAMBA.

Viongozi walioshiriki

Baadhi ya viongozin wa NASA walioonekana katika tukio hilo ni pamoja na Mwakilishi wa Wanawake Homa Bay, Gladys Wanga, Mbunge wa Rangwe Lilian Gogo, Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang’, Elisha Odhiambo (Gem) na Kiongozi wa walio Wachache Bungeni John Mbadi (Suba South).

Baadaye Mbunge wa Ruaraka, TJ Kajwang aliwasili akiwa amevalia joho la wanasheria na wig kichwani na kusisimua umati, ambao uliamini ndiye atakayesimamia kiapo cha Odinga na Kalonzo.

Kajwang alifuatiwa na Mwakilishi wa wanawake wa Kisumu, Rosa Buyu na Miguna Miguna, Gavana wa Mombasa Hassan Joho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles