Na Mwandishi Wetu, Mbeya
MABAO mawili ya Saido Ntibazonkiza na Fiston Mayele, yametosha kuipa Yanga alama tatu muhimu baada ya kuifunga Mbeya Kwanza mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa leo Novemba 30,2021 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Ntibazonkiza ndiye alianza kuwainua mashabiki wa Yanga dakika ya 18 kwa mpira wa adhabu baada ya Feisal Salum ‘’Fei Toto’kufanyiwa madhabi na mabeki wa Mbeya Kwanza, huku Mayele akifunga dakika ya 27 akipata pasi nzuri Fei Toto.
Ushindi huo umeifanya Yanga kuvunja rekodi ya Mbeya Kwanza ya kutopoteza mechi hata moja tangu imeanza ligi hiyo, huku Wanajangwani hao wakiendelea kujikita kileleni wakifikisha alama 19.
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasredine Nabi, amesema baada ya kutoka sare na Namungo katika mchezo uliopita alichukua jukumu la kurekebisha makosa.
Mchezo ujao Yanga inakutana na Simba Desemba 11,2021 lakini kocha huo amesema atauzungumzia baada ya mapumziko ya siku chache.
“Sasa hivi tunazungumzia ushindi wetu wa Mbeya Kwanza, najua mchezo ujao na Simba, nitauzungumzia baadae sio sasa,” amesema.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Mbeya Kwanza, Hererimana Haruna, amesema wachezaji wake walikosa umakini, pia waamuzi hawakuwatendea haki.
Katika mchezo mwingine, Biashara United imelazimishwa sare ya bao 1-1 na Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Karume, Mara.