Na RAYMOND MINJA -IRINGA |
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) mkoani hapa, umetoa msaada wa shuka 300 zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 4.5 kwa Halmashauri na Manispaa ya Iringa kusaidia upungufu uliokuwapo.
Msaada huo ulikabidhiwa jana na Meneja wa NSSF Mkoa wa Iringa, Josephat Komba ambaye alisema kuwa wameutoa ikiwa ni utekelezaji wa maombi yaliyotolewa na halmashauri hizo kwao.
“NSSF kama mfuko wa hifadhi ya jamii, unalo jukumu la kuendelea kuunga mkono jitihada za halmashauri nchini katika kutoa huduma za afya, ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa ili wananchi wake waweze kupata huduma bora,” alisema.
Komba alisema NSSF itaendelea kuwa karibu na jamii ya Watanzania kwani hatua ya waajiri kuwaunganisha wafanyakazi wao na mfuko huo, ni kutaka kuona maisha yao yanaendelea kuboreshwa zaidi, hivyo jukumu lao ni kuendelea kuunga mkono uboreshaji wa huduma za afya.
“NSSF imekuwa ikisaidia katika huduma mbalimbali za kijamii pamoja na kusaidia halmashauri, ila pia tumekuwa tukisaidia huduma ya matibabu kwa wanachama wetu bure pamoja na familia zao,” alisisitiza.
Komba aliongeza kuwa Hospitali ya Manispaa ya Iringa, Frelimo iliomba msaada wa kupatiwa shuka 200 na Halmashauri ya Iringa iliomba shuka100.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Omary Mkangama, aliipongeza NSSF kwa msaada huo katika Hospitali ya Frelimo na kuomba ushirikiano huo kuendelea zaidi.