23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

NMB, eGovernment Z’bar zasaini makubaliano Makusanyo Mapato

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

BENKI ya NMB na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kupitia Wakala wa Serikali Mtandao ‘eGovernment Zanzibar’, wamesaini makubaliano ya ushirikiano, yatakayowezesha mifumo ya NMB kuingiliana na ile ya ZanMalipo, hivyo kuwezesha taasisi za SMZ, kukusanya mapato kupitia matawi na mifumo ya kidijitali ya benki hiyo.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna na Mkurugenzi Mtendaji wa Serikali Mtandao Zanzibar, Said Seif Said wakibadirishana mikataba baada ya kutiliana saini ya makubaliano ya ushirikiano wa ukusanyaji mapato na malipo ya Serikali kwa njia ya Kidigtali wakati wa hafla iliyofanyika Zanzibar. Kulia anayeshuhudia ni Mwanasheria wa Benki ya NMB, Lilian Komwihangiro na kushoto ni Mwanasheria wa Ofisi ya Serikali Mtandao Zanzibar, Safia Hija Abass

Hafla ya kusaini makubaliano hayo imefanyika Zanzibar Jumatano Machi 16, ambapo NMB imesema imejipanga kuimarisha ushirikiano huo ambao utakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi visiwani humo, na kwamba inaamini utakuwa wa karibu zaidi, endelevu na wenye manufaa kwa SMZ na taasisi zake lakini pia utakaoleta maendeleo chanya.

Akizungumza kabla ya kusaini makubaliano hayo ya mwaka mmoja yenye kipengele kinachoruhusu mazungumzo na kuyarefusha, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, aliipongeza SMZ chini ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa mageuzi chanya ya kiuchumi yanayochakatwa na kusimamiwa na serikali yake kwa ustawi wa Taifa.

Zaipuna alibainisha kuwa makubaliano hayo ni chachu kwa taasisi yake kubuni suluhushi mbalimbali za Wazanzibar na Taifa ujumla, na kwamba maendeleo ya kidijitali kwa ulimwengu wa sasa hayaepukiki, hivyo ushirikiano wao huo utakuwa na mchango chanya katika kuharakisha ukuzaji uchumi na kurahisisha utendaji wa Serikali.

“Makubaliano haya ni kielelezo tosha kuwa Serikali ya Zanzibar na NMB sasa tunaenda kushirikiana kuboresha huduma za ukusanyaji mapato na malipo, sambamba na kuwezesha mifumo yetu kuingiliana na ile ya ZanMalipo, hivyo kuwezesha Taasisi za SMZ kukusanya mapato kupitia matawi ya NMB na mifumo ya kidijitali ya benki yetu.

“Kupitia makubaliano haya, NMB na eGovenment Zanzibar, tunaenda kutengenezea Kituo cha Pamoja cha Malipo Kidijitali ‘One Stop Center,’ cha Shirika la Bandari Zanzibar, ambacho kitampa mlipaji wa huduma mbalimbali ‘control number’ moja kwa ajili ya kufanyia malipo mbalimbili bandarini, badala ya namba tofauti tofauti.

“Suluhisho hizi mbili zinazooambatana na makubaliano haya, zinaenda kuboresha utoaji huduma kwa wananchi, lakini pia kuongeza ufanisi katika ukusanyaji mapato na kuondoa kero ya muda mrefu wanaotumia wananchi kufanya huduma za malipo,” alisisitiza Zaipuna mbele ya wanahabari katika Ukumbi wa Wizara ya Katiba na Sheria.

Alibainisha kuwa, SMZ kupitia eGovenment na NMB, wanaenda kujenga ushirikiano utakaokuwa chachu ya ukuaji wa uchumi na kwamba matarajio yao ni kuwa na ushirikiano endelevu, wa karibu zaidi, wenye manufaa kwa SMZ na taasisi zake, utakaoleta maendeleo chanya ya Serikali, Taifa na wananchi kwa ujumla.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna na Mkurugenzi Mtendaji wa Serikali Mtandao Zanzibar, Said Seif Said wakionyesha mikataba baada ya kutiliana saini ya makubaliano ya ushirikiano wa ukusanyaji mapato na malipo ya Serikali kwa njia ya Kidigtali wakati wa hafla iliyofanyika Zanzibar. Kulia anyeshudia ni Mwanasheria wa Benki ya NMB, Lilian Komwihangiro na kushoto ni Mwanasheria wa Ofisi ya Serikali Mtandao Zanzibar, Safia Hija Abass

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa eGovernment Zanzibar, Said Seif Said, aliishukuru NMB kwa kusaini makubaliano ya ushirikiano huo, ambao aliutaja kama muarobaini wa changamoto mbalimbali za kimalipo wanazokutana nazo wananchi wa Zanzibar, unaoenda pia kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali.

“Sisi eGovernment tunaamini kwamba ushirikiano huu ni chanya, utakaobeba tija kwa Serikali, hususani hiyo ‘One Stop Center’ ambayo itajikita katika kurahisisha mifumo ya malipo bandarini ambako tutatumia mifumo ya kidijitali kuongeza ufanisi  kwenye makusanyo mbalimbali.

“Tunatarajia huu utakuwa ni mwanzo tu, tunategemea kufanya mengi makubwa kwa pamoja baina yetu na NMB. Bandarini ni sehemu ambako kumekuwa na changamoto za muda mrefu katika masuala mazima ya makusanyo, lakini kupitia makubaliano haya tunaamini yataondoa na kumaliza changamoto zote hizo,” alisisitiza Seif.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles