Gabriel Mushi, Dodoma
Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), ameliomba Bunge kuunda tume maalumu kuchunguza miradi ya maji nchi nzima kwa kuwa kuna ubadhirifu zaidi ya uliokuwa kwenye mchanga wa dhahabu (makinikia).
Pia amesema baadhi ya miradi ya maji katika jimbo la Chemba amepewa Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) hali inayothibitisha namna gani kulivyo na ubadhirifu.
Nkamia ametoa kauli hiyo leo bungeni jijini Dodoma wakati akichangia majadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji na kuongeza kuwa licha ya kutoa maombi mwaka jana kuhusu kuundwa kwa tume hiyo sasa anarejea kuliomba Bunge litekeleze ombi lake kwa kuwa hatua alizoanza kuchukua na Rais John Magufuli dhidi ya ubadhirifu huo wa miradi hazitoshi.
“Tusimuachie rais peke yake, Bunge lina nafasi kama mhimili na wakati tume inaundwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ijiandae kupanua magereza. Miradi mingi kwa sisi wabunge tuliotoka vijijini imekuwa ‘dili’ tu.
“Kwa mfano pale Chemba kuna miradi mitatu, mmoja wapo amepewa Ofisa wa Takukuru, mimi nimekutana naye ‘site’ ndiye mkandarasi aliyepewa mradi. Kule Kiremba kuu mradi huo nao umechezewa tu halafu humu ndani tunaonekana hovyo,” amesema.