Na CHRISTIAN BWAYA
NILIPOANZA mkakati wa kuacha kutia sukari kwenye chai au kahawa, haikuwa kazi nyepesi. Kwa muda mrefu, kitendo cha kujaribu kuacha kilikuwa kama adhabu fulani hivi kwangu. Ningeweza mathalani, kujitahidi kuacha sukari kwa siku kadhaa lakini baadae ningejikuta nikijiambia, ‘acha nitumie sukari leo kwa mara ya mwisho. Kesho nitaendelea na mpango wangu.’
Haikuwa sukari pekee. Kwa kuwa nililenga kupunguza uzito wa mwili, nilijipiga marufuku kunywa soda hasa Coca Cola. Nimeitaja soda hii kwa sababu ilinitesa mno kuiacha. Ugumu wa kuiacha ulitokana na ukweli kwamba, mara kwa mara yalijengeka mazingira ya mimi kujikuta ninarudi kule kule nilikotoka. Ingawa niliamini nilikuwa na nia ya kuachana na vinywaji vyenye sukari, kufanya uamuzi thabiti wa kuacha kwa vitendo ilikuwa shughuli nzito kweli kweli.
Jaribio hili la kuachana na sukari nililinifundisha mambo kadhaa. Kwanza, ingawa nilikuwa na sababu za msingi za kunifanya niche sukari, bado sikuwa na uwezo wa kuacha. Uelewa wa athari ya matumizi ya sukari kupita kiasi haukusaidia kukata hamu ya sukari niliyokuwa nayo. Nilijua kuwa matumizi makubwa ya sukari ndiyo yanayochangia kuongeza uzito wa mwili nami sikupenda kuwa na uzito unaozidi kiwango. Hata hivyo, kila niliposhika kikombe cha chai nilijikuta natumia sukari bila kujua imekuwaje.
Wakati mwingine nilijinyima sukari kwa siku kadhaa, lakini nilipojikuta katika mazingira fulani  fulani –kama wakati wa kufanya kazi za usiku –ubavu wa kujinyima uliniishia. Mchanganyiko wa njaa na uchovu wa ubongo ulinishawishi kutumia vijiko kadhaa vya sukari kama namna ya kukusanya nguvu upya.
Nikajifunza kuwa kuna namna fulani akili yangu inaratibu kiu ya sukari bila mimi kuelewa kinachoendelea. Nilihitaji kuwa na nguvu ya utashi itakayoiamuru akili kuamini vinginevyo. Ndivyo akili zetu zinavyofanya kazi. Kile ambacho akili zetu zinaamini tunakitaka, ndicho tunachokifanya bila hata kufikiri. Kwa hiyo, niliazimia kuiaminisha akili kuwa sihitaji tena kutumia sukari. Nikaanza kujisemea maneno yanayosisitiza kuwa sina mpango wa kutumia tena sukari. Hatua kwa hatua ufahamu wangu ulianza kubadilika na kuamini kuwa hicho ndicho ninachokitaka. Mazoea mapya yakajengeka na ikaanza kuwa rahisi kusimamia kile ninachokitaka kitokee.
Jambo la pili nililojifunza ni umuhimu wa kuweka mazingira yanayonihamasisha kusimamia msimamo wangu. Mbali na kuiaminisha akili kuwa suala la kuacha sukari halikuwa utani, niligundua kuwa ninahitaji watu watakaonifanya nisirudi nyuma. Kwa hiyo ilibidi niwaeleze watu wangu wa karibu kuwa ninaacha sukari. Kufanya hivi kuliniongezea msukumo wa kusimamia nilichokuwa nimekiamini.
Nafikiri unaweza kutumia utaratibu huu hata kwa tabia nyingine unazotaka kuziacha. Usifanye uamuzi uwe siri yako. Unapowaambia watu kusudio lako unajitengenezea mazingira ya kulazimika kusimamia kile ulichokiamini hata pale unapojisikia kuahirisha mpango wako. Ukiwa na watu sahihi wanaounga mkono uamuzi wako, itakuwa rahisi zaidi kusimamia mpango wako.
Huwezi, kwa mfano, kuacha pombe katika mazingira ambayo umezungukwa na watu mliozoea kunywa nao. Ukiendelea kuwa na watu wa namna hii utajisikia mnyonge kuwa tofauti. Katika mazingira kama haya inaweza kuwa vigumu kuacha. Nafikiri mbali na kuwaambia ‘wanywaji’ wenzako kuwa unaacha pombe, ni muhimu kutengeneza mtandao mpya wa watu watakaokusaidia kuona thamani ya maamuzi uliyoyafanya. Unahitaji watu watakaokufanya ujisikie kupungukiwa ukiendelea kunywa.
Jambo la tatu nililojifunza ni kuifanya tabia usiyoipenda iwe ngumu. Nakumbuka wakati ninapambana kuachana na usumbufu wa mitandao ya kijamii kama WhatsApp, ilibidi kuifuta kwenye simu yangu. Hatua hii ilikuwa ngumu kuichukua lakini ililenga kuweka ugumu wa kurudi kule kule nisikokupenda. Unaweza kufanya hivyo kwa karibu kila tabia usiyoipenda.
Kama wewe ni mtumiaji mbaya wa fedha, unahitaji kujiwekea mazingira magumu ya kuchukua fedha benki. Fanya iwe vigumu kutoa fedha kwenye akaunti yako. Kwa mfano, badala ya kujiunga na huduma za kibenki zinazopatikana kwenye mitandao ya simu lazimika kwenda benki au mashine ya kutolea fedha (ATM) ili kuchukua fedha. Kama mazingira yako yanaruhusu, akaunti ya pamoja na mume/mke wako inaweza kukusaidia. Ule usumbufu wa kumtafuta mwenzako asaini hati ya kuchukua fedha inaweza kukusaidia kujidhibiti.
INAENDELEA
Christian Bwaya ni mnasihi na mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0754870815 au barua pepe [email protected] kwa msaada zaidi.