33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

NIYONZIMA, OKWI WAMPASUA KICHWA OMOG

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

MASHABIKI wa Simba wanajivunia kumiliki kikosi kipana chenye wachezaji mahiri wenye vipaji vya hali ya juu, baada ya kufanya usajili wa uhakika kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Baadhi ya nyota waliotua Simba kwenye dirisha la usajili la msimu ujao ni mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo raia wa Uganda, Emmanuel Okwi na aliyekuwa kiungo wa Yanga, Mnyarwanda Haruna Niyonzima.

Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, amekiri kuwa sasa ana wachezaji wenye ubora wa juu lakini ana kazi moja ngumu ya kufanya ambayo ni kuwaunganisha nyota wake hao ili msimu ujao mashabiki wa timu hiyo waweze kulia kimvulini, yaani kushangilia matokeo mazuri.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Omog alisema hadi sasa hajui wachezaji gani watatengeneza kikosi chake cha kwanza, lakini ameahidi kukamilisha kazi hiyo wiki ya kwanza baada ya uzinduzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.

“Kupitia mechi za kirafiki tulizocheza nimeona kikosi kimeanza kuimarika, lakini tatizo lililopo kwa sasa ni muunganiko kwa wachezaji ambao naamini kabla ligi haijaanza tutakuwa tumeshakaa vizuri,” alisema.

Alisema kwa sasa anaendelea na maandalizi ya mwisho kabla ya kukutana na Yanga wiki ijayo, huku akiahidi  kikosi chake kitapambana kuhakikisha kinapata matokeo mazuri.

Omog alisema ili kujiweka fiti zaidi kikosi chake leo kitacheza mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya Mlandege FC, ambao pia walikipiga na Yanga na kuchapwa mabao 2-0.

Wakati huo huo, Okwi amesema kikosi cha timu hiyo bado hakijaiva sawa sawa licha ya kushinda mechi mbili za kirafiki.

Simba imecheza mechi mbili za kirafiki tangu iliporejea nchini kutoka Afrika Kusini ilikopiga kambi ya wiki mbili kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii na Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wekundu hao walicheza mchezo wa kwanza dhidi ya mabingwa wa Rwanda, Rayon Sports, katika tamasha maalumu la siku ya klabu hiyo ‘Simba day’ na kushinda bao 1-0 kabla ya juzi kuibuka na ushindi kama huo dhidi ya Mtibwa Sugar. Bao la Simba kwenye mchezo huo lilifungwa na Okwi.

“Kadiri tunavyofanya mazoezi pamoja naamini tutaelewana na kuzidisha ushindani.

“Wajibu wetu ni kumsikiliza kocha kwa makini na kufanyia kazi maelekezo yake ili kuepuka kurudia makosa yale yale, naamini kadiri muda unavyokwenda tutakuwa sawa.”

Okwi amerejea katika klabu hiyo ya Msimbazi baada ya kusajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili akitokea SC Villa ya Uganda, ambayo alijiunga nayo akitokea Sonderjyske ya nchini Denmark.

Mshambuliaji huyo alijiunga na  Sonderjyske mwaka 2015 akitokea Simba, lakini alijikuta kwenye wakati mgumu wa kusoteshwa benchi hatua iliyomfanya aamue kuvunja mkataba wake na kurejea SC Villa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles