21.4 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

Niyonzima aomba msamaha Yanga

haruna-niyonzima_nnl3mn7ndsd11fsiur0nx4723NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

KIUNGO mchezeshaji wa Yanga, Haruna Niyonzima, ameomba msamaha kwa klabu yake kutokana na adhabu aliyopewa ya kufukuzwa kuichezea timu hiyo kwa kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu.

Niyonzima ambaye aliongezewa mkataba wa miaka miwili Mei mwaka jana, alitimuliwa na klabu hiyo na kutakiwa kulipa faini ya dola za Kimarekani 71,175 (sawa Sh milioni 154 za Tanzania) kutokana na kuvunjwa kwa mkataba wake.

Kitendo cha kuchelewa mara kwa mara kambini kwa kiungo huyo raia wa Rwanda anayechezea timu yake ya Taifa ‘Amavubi’, kilichukuliwa kuwa ni utovu wa nidhamu jambo lililoifanya klabu yake kufikia uamuzi wa kusitisha mkataba wake Desemba 28, mwaka jana.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Niyonzima alisema amefanya uamuzi huo baada ya kujitathmini hivyo amekutana na uongozi wa klabu yake ili waweze kufikia mwafaka katika suala hilo.

“Yanga walikuwa na haki ya kunipa adhabu kutokana na kutokuwepo kwa mawasiliano mazuri wakati nikiwa nchini kwetu Rwanda.

“Ninaomba msamaha kwa uongozi na wapenzi wote wa klabu ya Yanga, maana naamini tukisameheana tutaanza kufikiria mambo yajayo kwa maendeleo ya timu,” alisema Niyonzima.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Jerry Muro, alisema wamepokea ombi la mchezaji huyo na uongozi utatoa tamko juu ya suala hilo.

“Tutajibu ombi la Niyonzima kwa barua kama tulivyofanya siku ya kuvunja mkataba wake, Yanga tunafuata utaratibu wa kimataifa kwa kuwa yeye si mchezaji wa mchangani,” alisema.

Aidha, Muro alisema kiungo huyo haruhusiwi kujiunga na wachezaji wengine wa timu hiyo hadi uongozi utakapofanya uamuzi juu ya ombi lake.

Ikiwa uongozi wa Yanga utafikia uamuzi wa kumsamehe Niyonzima ambaye kiwango chake bado kinakubalika kwa Wanajangwani hao, huenda akarejea dimbani Alhamisi hii kuivaa Majimaji FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles