26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, November 2, 2024

Contact us: [email protected]

Nini kimejificha nyuma ya IPTL?

Benki Kuu ya Tanzania
Benki Kuu ya Tanzania

Na Waandishi Wetu

VITA ya maneno inayoendelea kupiganwa na wanasiasa kwa upande mmoja na serikali kwa upande mwingine, msingi wake ukiwa ni uuzwaji wa mitambo ya IPTL uliokwenda sambamba na uchotwaji wa fedha kwenye akaunti ya ESCROW, ina kila dalili zinazoonyesha kwamba kuna siri nzito ambayo imejificha nyuma ya sakata hilo.

Kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na watendaji wa serikali zenye mwelekeo wa kushambulia huku baadhi ya wabunge waliolishikia bango suala hilo wakidai kuwa kuna ukweli unafichwa wakati ambako Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) zikiwa bado hazijakamilisha uchunguzi wake, ndiyo iliyoibua hisia za namna hiyo miongoni mwa jamii.

Tukio la hivi karibuni kabisa la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi kutoa maneno ya kejeli na kuponda nyaraka ambazo zimekuwa zikitolewa na wabunge kama ushahidi dhidi ya kile walichokiita ‘mchezo mchafu kuhusu sakata la IPTL’, likiwa limetanguliwa na kauli nyingine kadhaa za aina hiyo, ikiwamo ile iliyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, ndilo linaloonekana kulizamisha suala hilo kwenye makandokando kwamba huenda kuna yaliyojificha katika suala hilo.

Hilo linaweza kupata nguvu kutokana na kauli ya Maswi wakati akizungumzia mgogoro huo juzi, ambapo aliziponda kauli za wabunge wa upinzani pamoja na kukejeli nyaraka walizozitoa bungeni kama ushahidi kuhusu utata wa sakata zima la IPTL.

Maswi alisema kuwa wabunge hao wa Kigoma Kaskazini (Chadema) Zitto Kabwe na David Kafulila wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) ni washenzi na kwamba njaa zinawasumbua kwa kulilia fedha za IPTL.

Katikati ya wiki hii, Kafulila alijikuta katika mgogoro mkali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Werema ndani na nje ya Bunge, baada ya mbunge huyo kuigomea taarifa ya AG kuhusu sakata la Kampuni ya Escrow.

Werema aliliambia Bunge kuwa fedha zinazodaiwa na Kafulila pamoja na wabunge wenzake wa kambi ya upinzani kuwa zilichotwa katika mazingira ya kutatanisha, zilichukuliwa na mwekezaji mpya wa IPTL ambaye ni Pan Africa Power Solution Limited (PAP).

Ni maelezo hayo ambayo Kafulila aliyapinga, akidai kuwa fedha hizo, takribani Sh bilioni 200 zilizowekwa kwenye akaunti hiyo ya Tanesco, ziligawanywa miongoni mwa watendaji wa Serikali, AG alijikuta akimwita mbunge huyo tumbili huku naye akimwita mwizi na hivyo kuibuka mgogoro mkubwa ndani na nje ya Bunge.

Wasiwasi wa Kafulila na majibizano hayo yameibuka katika kipindi ambacho kuna mwelekeo wa kila upande kuanza kuandaa mazingira ya kutaka kuwa wa kwanza kuiona ripoti ya uchunguzi inayotarajiwa kuwasilishwa na CAG pamoja na Takukuru.

Tayari Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amekwishatamka bayana kwamba ripoti ya uchunguzi ikikamilika ikabidhiwe ofisini kwake.

Wakati huo huo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) inayoongozwa na Zitto nayo inataka kuona ripoti hiyo ikifikishwa kwake kama ambavyo iliagiza.

Kamati hiyo ya PAC, Machi mwaka huu ilimuagiza CAG kufanya ukaguzi  maalumu katika uuzaji wa IPTL na utoaji wa fedha katika akaunti ya Escrow, kabla Waziri Mkuu Pinda naye hajaagiza kufanywa kwa uchunguzi kama huo bungeni mapema mwezi huu.

Zitto kwa upande wake tayari amekwisha ijibu kauli ya Maswi, akieleza kuwa kama wanadhani ni msafi, basi hana budi kusubiri ripoti ya CAG na Takukuru.

Alipoulizwa kwanini anahoji suala hili wakati tayari kuna vyombo vinachunguza, kwa upande wake Kafulila alisema Bunge halijawahi kupitisha azimio la kupeleka suala la IPTL kuchunguzwa na CAG na kwamba uamuzi huo ni wa Spika Anne Makinda pamoja Waziri Mkuu Pinda.

Alisema kiutaratibu jambo lolote linalojadiliwa ndani ya Bunge kabla halijapelekwa kwa CAG lazima wabunge waafikiane kwanza.

“Hili suala bado tunaliongelea kwa sababu maamuzi ya kulipeleka kwa CAG yalitolewa na Spika na Waziri Mkuu wakati kwa ratiba ya kawaida ilipaswa lijadiliwe kwanza ndio lipelekwe,” alisema Kafulila.

Pamoja na hilo, pia alisema hana imani suala hilo kupelekwa kwa CAG kwa sababu ripoti zake zimekuwa zikiwapendelea viongozi wa Serikali wanaotuhumiwa kama alivyofanya wakati wa sakata la EPA.

“Suala la Jairo CAG alimbeba kabisa, pia wakati Dk. Slaa  anaiongelea EPA alionekana si mzalendo kwa suala ambalo lipo,” alisema Kafulila.

Katika hilo, alisema serikali inapaswa kutafuta kampuni ya kimataifa ili kuchunguza suala hilo, kwani viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini wamekuwa wakitumia ujanja ujanja kukwepa sakata hilo, hivyo kusababisha jamii kukosa majibu.

Pia alisema anashangaa kuona wabunge wanaozungumzia sakata la IPTL wakihusishwa na rushwa, jambo ambalo halina ukweli.

“Huyu Maswi na Muhongo ni wababe wa uongo, kila siku wanataja watu wanasema wanatupa hela mara Standard Chartered, mara wanamtaja Mengi, nasema hiyo siyo issue (suala) iliyopo mezani, suala lililopo mezani ni fedha za IPTL waseme zipo wapi, mimi siwezi kusumbuka na uongo wao.

“Nakuhakikishia katika hili suala Maswi atakwenda jela kuungana na Mramba, maneno yote yanamtoka kwa sababu ya woga wa kwenda mahakamani, majungu yake katika suala lenye ukweli hayatamsaidia,” alisema Kafulila.

Alisema yeye binafsi anao ushahidi jinsi fedha hizo zilivyohamishwa kutoka Benki Kuu na kwamba anachokizungumza hajakurupuka.

“Hawa kama wanalijua hili suala vizuri mbona walikimbia mjadala kuhusu Escrow ulioitishwa na sauti ya Ujerumani, Radio Deutsche Welle katika kipindi cha Meza ya Duara, kipindi tulialikwa mimi na Zitto na watu wengine, mtangazaji alisema Waziri Muhongo kamwambia hawezi kushiriki kwa sababu mjadala huo hauna tija kwa taifa, kama hawajaiba wanaogopa nini?” alihoji Kafulila.

“Kwa taarifa yao sasa kama wanajiamini na wana uwezo waitishe mjadala kuhusu suala hili, nitawaruhusu waje wizara nzima na maofisa wote wanaowategemea mimi niwe peke yangu tuongelee IPTL waone kama hawajakimbia kwa aibu,” alisisitiza Kafulila.

Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Ludovick Utoh ambaye pia alizungumza na gazeti hili kuhusu nini anachokiona kuhusu mwenendo wa sasa, yeye alisema hafanyi kazi kwa kutumia mawazo binafsi ya watu.

“Kwenye ‘issue’ ya IPTL, naomba niseme kuna mawazo mengi na kauli nyingi zinazotolewa na watu mbalimbali, ofisi yangu na ile ya PCCB tunatafuta ukweli wa jambo hili, lakini hatuwezi kutumia mawazo ya watu katika uchunguzi,” alisema Utouh.

Kuhusu atakakokabidhi ripoti, CAG alisema; “Mimi sifanyi kazi kwa utaratibu huo, nikimaliza uchunguzi ripoti naitoa kwa wahusika na sio kuwaonyesha viongozi kwa sababu zao binafsi”.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah, alipotafutwa na gazeti hili kwa njia ya simu jana ili kujua iwapo ofisi yake inazifanyia kazi tuhuma zilizotolewa dhidi ya wabunge watatu kupeana rushwa, alijibu kupitia ujumbe mfupi kuwa wanachokifanya hivi sasa ni kutekeleza agizo la Bunge.

“Bunge limeelekeza na tunayafanyia kazi, azimio la Bunge. Mengine kama yapo yaletwe rasmi ofisini yatashughulikiwa,” alisema Dk. Hoseah.

Maswi alipozungumza na MTANZANIA Jumapili kuhusu kilicho nyuma ya sakata la IPTL, alisema haoni haja ya kuzungumzia suala hilo kwa sababu liko chini ya TAKUKURU na CAG.

“Mimi naomba hilo suala tuachane nalo, siwezi kuliongelea kwa sasa, kama ni kweli tuliiba tusubiri majibu ya TAKUKURU na CAG yatasema,” alisema Maswi.

Kufunguliwa kwa akaunti ya Escrow Benki Kuu ya Tanzania (BoT), msingi wake ni mkataba unaodaiwa kuwa ni wa kifisadi wa IPTL uliosainiwa mwaka 1995 kutokana na tatizo la umeme mwaka 1994, ambapo taifa lilihitaji umeme wa dharura.

Ni wakati huo IPTL ikasaini mkataba wa miaka 20 (1995-2015) na wamiliki wa kampuni hiyo ya IPTL walikuwa Mechmar ya Malaysia mwenye asilimia 70 na VIP ya Tanzania yenye asilimia 30 kabla ya kuiuza kwa PAP.

Mwenyekiti Mtendaji wa PAP, Harbinder Singh Sethi, anadaiwa kuwa na rekodi mbaya na ya ufisadi tangu nchini Kenya anakotuhumiwa kushiriki ufisadi mkubwa mwaka 2002 wa Goldenberg – kashfa iliyokiangusha chama cha KANU chini ya Rais Daniel arap Moi.

Singh pia anadaiwa hana rekodi yoyote ya uwekezaji katika masuala ya umeme, jambo ambalo limezidisha wingu la mashaka kama ni mwekezaji anayeaminika kwa kazi.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. MASWI NAYE ANAUWEZO MDOGO SANA WA KUFIKIRI NA KUVIANGALIA VITU KWA MAWANDA MAPANA. ANGEKUWA NI MWENYE ANGALAU HATA CHEMBE YA UFAHAMU, ASINGE SEMA KUWA wabunge wa kigoma ni washenzi na kwamba njaa zinawasumbua kwa kulilia fedha za IPTL. JE NI NJAA IPI WALIYO NAYO WABUNGE HAWA KAMA SIYO MASLAHI YA TAIFA? THINK TWICE BEFORE YOU ACT ONCE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles