M23 waibuka mafichoni

0
1058

Mtanzania Juni 29, 2014Na Ratifa Baranyikwa

BAADA ya kimya cha muda mrefu, kundi la waasi wa M23 waliokuwa wakipigana Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kabla ya kuondoshwa rasmi na vikosi  vinavyoundwa na Umoja wa Mataifa (Monusco), limeibuka na kusema kuwa linatarajia kuanika mikakati yake.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na  MTANZANIA Jumapili kutoka nchini Uganda, kiongozi wa kisiasa wa kundi hilo, Bertrand Bisiimwa, alisema baada ya kimya cha muda  mrefu, wakati wowote kuanzia kesho wataweka wazi kile wanachofikiria na walichopanga kufanya.

Bisiimwa, ambaye alisema yuko nchini Uganda tangu Oktoba mwaka jana, ametoa kauli hiyo wakati mazungumzo kati ya kundi lake na Serikali ya Kongo yakiwa bado hayajamalizika.

Alisema tangu waondoshwe Kongo mwaka jana, sasa ni takribani miezi minane wako Uganda wanaendelea  na maisha wakati wakisubiri kupatikana kwa muafaka.

“Wakati wowote kuanzia kesho tutasema kila kitu, tumefanya evaluation (tathimini) tutazungumzia ile declaration (maazimio) ya Nairobi, ili ulimwengu ukuje ujue tuko  wapi tunafikiria nini na tumepanga nini,” alisema Bisiimwa kwa Kiswahili cha tabu kidogo.

Alisema kile ambacho watakizungumza watakifikisha kwenye vyombo vya habari ili viweze kuchapisha na ulimwengu uweze kujua.

Desemba 12 mwaka jana, mmoja wa viongozi wa kundi hilo, Jenerali Sultan Makenga pamoja na Jeshi la Kongo walisaini maazimio nchini Kenya ambayo yamekuwa yakijulikana  kama maazimio ya Nairobi.

Kilichomo hasa ndani ya maazimio hayo hakikuweza kujulikana wakati huo na M23 walisikika wakisema kuwa hayapingani na mkataba wa Kampala.

Mkataba huo wa Uganda pamoja na mambo mengine uliitaka M23 kukomesha uasi na kukubali kujibadilisha kuwa chama cha siasa, msamaha kwa wanachama wa M23 tu na  kusambaratisha kundi la zamani.

Pia Serikali ya DRC isaidie katika mchakato wa kuwahamisha na kuwanyang’anya silaha waasi hao, ambako pia kutahusisha sehemu fulani ya msamaha.

Pia ilijumuisha makubaliano ya kutolewa kwa yote yaliyosababishwa na vita hivyo ama uasi na kurudishwa kwa waliokosa makazi kutokana na mapigano.

Mengine ni kuwepo kamati ya kushughulikia mali na ardhi zilizoibwa, kupokonywa ama kuharibiwa kutokana na vita hiyo.

Akizungumza kuhusu maazimio hayo, Bisiimwa alisema bado hawajafikia muafaka na upande wa Serikali ya Kongo.

“Bado hatujamaliza panga mambo yote na watu wa government (serikali),” alisema Bisiimwa.

Alipoulizwa mambo hayo ni mambo gani, Bisiimwa alikataa kuweka wazi akiahidi kufanya hivyo kwenye mkutano wao huo.

Kuhusu ukimya wao, Bisiimwa alisema ilikuwa ni muhimu kwao wabaki kimya ili mambo ya Kongo yaende, lakini pia watu wengine wapate nafasi ya kujipigia debe kuwa wamefanya jambo muhimu.

Alipoulizwa ni watu gani, Bisiimwa alisema kuwa ni wale waliowaondosha katika eneo la Mashariki ya Kongo.

Mwishoni mwa mwaka jana vikosi vya Serikali ya Kongo kwa kusaidiwa na vile vya Umoja wa Mataifa vilivyopewa uwezo wa kupigana, wakiongozwa na JWTZ wa Tanzania walifanikiwa kuwaondoa waasi wa kundi la M23 waliokuwa wakikalia maeneo mengi ya mashariki ya nchi hiyo.

Inaelezwa kuwa M23 ambao wanadaiwa kuungwa mkono na nchi ya Rwanda, walipata kipigo kikali, kilichomlazimisha kiongozi wake wa kisiasa, Bertrand Bisiimwa kuweka silaha chini na kurudi Uganda kwa ajili ya mazungumzo ya amani.

Kipigo hicho ni wazi kilituma ujumbe wa kitisho kwa vikundi vingine karibu 10 vinavyoendesha mapambano yao katika eneo hilo, jambo ambalo limetoa matumaini ya kuleta amani ambayo imetoweka kwa miongo miwili sasa katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.

M23 linatajwa kama kundi pekee lilikokuwa na nguvu katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo.

Hata hivyo Stephanie Wolters, ambaye anafundisha katika Chuo Kikuu kinachofundisha masomo ya usalama nchini Afrika Kusini, aliwahi kusema kuwa kipigo hicho cha M23 hakimaanishi kwamba Kongo kutakuwa na amani ya kudumu.

Alisema ili kujua kwamba matumaini hayo ya kuleta amani ni hafifu, ni vizuri tukaangalia jinsi kundi hilo la M23 lilivyoundwa na baadhi ya wanajeshi kutoka Jeshi la Serikali ya Kongo, ambalo linajulikana kwa utovu wa nidhamu, rushwa na kutokuwa na uwezo.

Wakati M23 lilipochukua udhibiti wa mji wa Goma, ambao una watu karibu milioni moja Novemba mwaka 2012, liliisumbua Serikali ya Kongo na kuishinikiza Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua dhidi ya vitendo vilivyojitokeza vya uvunjifu wa haki za binadamu.

Rais Joseph Kabila amefanya mabadiliko ya kiuongozi ndani ya jeshi pamoja na vikosi ambavyo vinapambana katika eneo hilo la mashariki.

Katika ishara ambayo inaonyesha mabadiliko yameanza, hakuna ripoti yoyote ya hivi karibuni iliyotolewa dhidi ya uvunjifu wa haki za binadamu, kama ambavyo ilikuwa ikitokea katika operesheni nyingine zilizotangulia.

Machi mwaka jana, Umoja wa Mataifa ulithibitisha askari 3000 wa Afrika, wakiwemo wanajeshi wa Tanzania waliopewa mamlaka ya kutumia silaha kupambana na waasi.

Pamoja na usaidizi wa operesheni nyingine za kikosi cha Monusco, kikosi hicho kipya kimekuwa kikitumia  helikopta kwa ajili ya kuwalenga waasi na kuliruhusu jeshi kusonga mstari wa mbele.

UN tayari ilikwishaanza kutumia ndege zisizo na rubani kukamilisha operesheni hiyo, zoezi ambalo linatoa nafasi ya kufuatilia mienendo ya waasi na usambazaji wa silaha.

Wachunguzi wa UN wamekuwa wakizishutumu nchi za Rwanda na Uganda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, ingawa nchi zote mbili zimepinga madai hayo.

Katika kile ambacho kinaweza kuelezwa kuwa ni dhamira ya kweli kwamba inataka kufikia muafaka juu ya mgogoro huo, Uganda imekuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani kati ya Kongo na M23.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here