25.9 C
Dar es Salaam
Friday, December 13, 2024

Contact us: [email protected]

Ushuru wa magari chakavu juu, vinywaji baridi chini

Saada Mkuya Salum
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum

Na Khamis Mkotya, Dodoma

WAZIRI wa Fedha, Saada Salum Mkuya, juzi aliwasilisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2014, ambao umefanya marekebisho ya viwango vya kodi, ushuru, ada na tozo katika maeneo mbalimbali.

Katika mabadiliko hayo, ushuru wa bidhaa katika magari yasiyokuwa ya uzalishaji (Non-Utility Motor Vehicles) yenye umri wa miaka 10 na zaidi umeongezeka, kwa sasa yatatozwa asilimia 30 ya uchakavu badala ya asilimia 25.

Serikali imefanya marekebisho hayo kutokana na wabunge wengi kulalamikia umri wa magari kushushwa kutoka miaka kumi hadi minane, kwa maelezo kuwa wananchi wengi hawana uwezo wa kununua magari mapya.

Aidha magari yenye umri wa miaka minane hadi tisa yatatozwa ushuru wa bidhaa wa asilimia 15 badala ya asilimia 25 kama ilivyotangazwa Juni 12, katika bajeti kuu ya serikali.

Akiwasilisha muswada huo, Mkuya alisema Serikali imepandisha ushuru huo ili kutoa hamasa kwa watu kuagiza magari yasiyochakavu.

“Lengo la hatua hii ni kupunguza wimbi la uagizaji wa magari chakavu ambayo yanasababisha ajali, vifo na kusababisha gharama ya kutumia fedha za kigeni kuagiza vipuri mara kwa mara na kulinda mazingira,” alisema.

Ushuru katika vinywaji baridi (soda) umepunguzwa kutoka Sh 91 hadi Sh 55 kwa lita, awali serikali iliongeza ushuru wa bidhaa hiyo kutoka Sh 91 hadi Sh 100 kwa lita.

Ushuru wa vinywaji vikali umeongezeka kutoka Sh 2,631 hadi Sh 3,157 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 526, ambapo awali ushuru wa bidhaa hiyo ulitoka Sh 2,631 hadi Sh 2,894 kwa lita, ikiwa ni ongezeko la Sh 178 kwa lita.

Ngozi ghafi

Serikali imefanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Mauzo ya Nje ili kupunguza kiwango cha ushuru wa mauzo ya nje unaotozwa katika ngozi ghafi zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi kutoka asilimia 90 au Sh 900 na kuwa asilimia 60 au Sh 600 kwa kilo moja ya ngozi.

Waziri Mkuya alisema marekebisho hayo yanalenga kuzuia biashara ya magendo ya ngozi ghafi, ambapo baadhi ya wafanyabiashara wanatumia njia hiyo haramu na matokeo yake Tanzania inaonekana haiuzi ngozi ghafi katika soko la dunia.

Mtaji wa uwekezaji

Serikali imefanya marekebisho ya Sheria ya Uwekezaji Tanzania sura ya 38 kwa kupandisha kiwango cha chini cha mtaji wa uwekezaji kutoka kiwango cha sasa cha Dola za Marekani 300,000 hadi Dola za Marekani 500,000 kwa wawekezaji wa nje.

Mtaji wa uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani unabaki kuwa Dola za Marekani 100, 000 kama ilivyo sasa.

Serikali pia ilipendekeza kiwango cha chini cha mtaji kwa wawekezaji mahiri cha Dola za Marekani milioni 20 kwa wawekezaji wa ndani, ambapo kwa upande wa wawekezaji wa nje ni Dola za Marekani milioni 50.

Kamari yarejeshewa msamaha

Serikali imefanya marekebisho kwa kurejesha msamaha wa kodi ya mapato yatokanayo na michezo ya kubahatisha, ambayo hivi sasa inatozwa kupitia Gaming Tax.

Awali miongoni mwa maeneo ambayo yalifutiwa msamaha wa kodi ni pamoja na michezo hiyo, kwa mujibu wa Mkuya, Serikali imefanya marekebisho hayo baada ya kuzingatia ushauri wa wabunge.

Hata hivyo, wakati muswada huo ukijadiliwa, baadhi ya wabunge walipinga hatua hiyo ya Serikali ya kurejesha msamaha katika michezo hiyo kwa maelezo kuwa haina faida kwa jamii zaidi ya kuwafaidisha watu wachache.

“Mimi sioni sababu hasa ya msamaha huu kurejeshwa, kwa kurejesha msamaha huu wananchi wanafaidikaje? Wanaokwenda kucheza kamari kwenye makasino ni watu wenye fedha, wanakwenda kwa starehe zao, sioni sababu ya kutoa unafuu huu,” alisema Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage.

Ukodishaji ndege

Waziri Mkuya alisema msamaha wa kodi ya mapato yatokanayo na ukodishaji wa ndege nje ya nchi umefutwa, ili kupunguza misamaha isiyokuwa na tija.

“Marekebisho haya yanalenga kutoza kodi ya mapato yatokanayo na ukodishaji ndege nje ya nchi, badala ya kumsamehe kodi mlipakodi asiye mkazi,” alisema.

Bunge lilipitisha Muswada huo pamoja na marekebisho yake, baadaye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alitoa hoja ya kuahirishwa kwa mkutano huo wa kumi na tano wa Bunge hadi Novemba 4, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles