25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ni Mapambano

mapambano*Polisi wapambana na wahalifu mapangoni kwa zaidi ya saa 12

*Wakutwa na silaha nzito za vita mapangoni, watatu wauawa

 

Na Fredrick Katulanda, Mwanza

POLISI mkoani Mwanza wakitumia silaha nzito, jana walipambana zaidi ya saa 12 na watu wanaodaiwa kuhusika na mauaji ndani ya Msikiti wa Rahman katika Mtaa wa Utemini, Kata ya Mkolani wilayani Nyamagana, wiki chache zilizopita.

Katika mapambano hayo, polisi waliweza kuwaua  watatu akiwamo Said Hamis Mbuli (48) aliyekuwa akitafutwa na polisi kwa muda mrefu.

Habari zilizopatikana eneo la tukio jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi zilieleza kuwa mapambano hayo yalianza saa 10 jioni juzi hadi usiku wa manane jana.

Katika mapambano hayo, polisi walilazimika kutumia silaha kali yakiwamo makombora ya RPG (Rocket Propelled Grenade ) kushambulia ndani ya mapango ya mawe huku wahalifu hao nao wakiwarushia polisi mabomu ya kutupa kwa mkono.

Habari zinasema, katika mapambano hayo, polisi waliwaua watuhumiwa watatu ambao wawili wametambulika na mmoja hajatambulika.

Kamanda Msangi alisema jana kuwa  Juni 3, mwaka huu polisi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama walimkamata Omary Francis Kitaleti maarufu kwa jina la Kiberiti, ambaye alikiri kuhusika na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kukubali kuwapeleka walipo wenzake.

Alisema mtuhumiwa Omari alikiri kuwa kundi hilo ndilo lililohusika na uvamizi ndani ya Msikiti wa Rahman,  Mtaa wa Utemini Mei 18, mwaka huu na kuwachinja waumini watu watatu  wa dini ya Kiislamu waliokuwa wakiswali.

Omari alisema kundi hilo pia lilihusika na matukio ya wizi katika  maduka ya M-pesa yaliyokuwa yakitokea jijini Mwanza.

“Jana (Juzi) huyu Omari alikubali kuwapeleka askari huko kwenye maficho ya wenzake   kwenye mapango ya Mlima wa Utemini saa 11 jioni.

“Lakini polisi walipofika eneo hilo, ghafla walianza kushambuliwa kwa risasi na wenzake waliokuwa wamejificha ndani ya mapango hayo.

“Katika mapambano hayo ya risasi na   polisi, Omari aliuawa na wenzake na askari wetu mmoja alijeruhiwa mguu wa kulia kwa risasi,” alisema.

Alisema    polisi waliweza kumuua mtuhumiwa mmoja ambaye hajafahamika jina lakini anakadiriwa kuwa na umri kati  ya miaka 20 hadi 25 ambaye alikua akiwashambulia polisi kwa   bastola.

Mtuhumiwa alikuwa akitumia bastola  ya Chinese   namba M.20-06436 iliyokuwa na risasi tatu ndani ya magazine, huku wengine waliokuwapo kwenye mapango hayo wakiendelea kushambulia kwa risasi.

Kamanda alisema baada ya kuona mapambano ni makubwa, polisi waliongeza nguvu na kuyazingira maeneo hayo ya mapango hadi alfajiri ya kuamkia jana, ingawa usiku kucha mapambano ya risasi yaliendelea.

“Alfajiri watu hao baada ya kuona wamezidiwa nguvu na kumekaribia kupambazuka   waliamua kuondoka ndani ya mapango hayo kwa kurusha bomu moja la kutupa kwa mkono huku wakizidisha mashambulio ya risasi na baadhi yao walifanikiwa kutoroka.

“Hata hivyo watatu walitoroka kwa kukodi pikipiki na wengine teksi kukimbilia mtaa wa Nyasaka lakini wakati wakitoroka katika mapango hayo,   dereva wa bodaboda aliyembeba mtuhumiwa mmoja alimtilia shaka akawajulisha polisi.

“Aliwaeleza kuwa alikodiwa na mmoja wa watuhumiwa na kumpeleka eneo la Kiseke Wilaya ya Ilemela,” alisema.

Kamanda alisema kwa  taarifa hizo,  polisi wengine walifuatilia eneo la Kiseke na mtaa wa Nyasaka ambako walimuona mtuhumiwa mmoja.

Alisema mtuhumiwa huyo  baada ya kuona anafuatiliwa na polisi, alitoa bunduki lakini wakati akitaka kuwashambulia,  askari walimuwahi kwa kumfyatulia risasi   na   kumuua papo hapo.

Mtuhumiwa aliyekimbilia Kiseke pia alikamatwa na kurejeshwa Utemini ambako alikufa  baadaye kutokana na majeraha aliyokuwa nayo.

Kamanda Msangi alisema mtuhumiwa Said Khamis Mbuli  (48) ambaye ni mmoja wa waliouawa, alikuwa akitafutwa kwa kuhusika na uporaji katika  maduka ya M-Pesa  na   tukio la mauaji msikitini.

“Huyu Mbuli   alipatikana na bunduki  ya SMG  namba 307039 iliyokuwa na risasi nane na kisu kimoja.

“Wenzake wawili walitoroka ila msako wetu  unaendelea na tutahakikisha tunawakamata wote,” alisisitiza Kamanda.

RC Mongella

Jana asubuhi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella, alitembela eneo la tukioMtaa wa Utemini  na kuzungumza na wananchi.

Pamoja na kuwapongeza kwa kutoa taarifa za siri,  aliwaeleza kuwa wanao wajibu wa kujilinda kwa kuendelea kutoa taarifa zaidi.

Alitoa pongezi za pekee kwa dereva wa bodaboda ambaye alitoa taarifa nzuri zilizofanikisha kukamatwa  mmoja wa watuhumiwa aliyetoroka mapangoni hapo na kukimbilia Kiseke wilayani Ilemela.

“Kwa namna ya pekee   nampongeza huyu mwendesha bodaboda ambaye aliwabeba lakini kutokana na hali fulani aliwashtukia na kuamua kutoa taarifa zao polisi.

“Hata alipoitwa baada ya polisi kufika na kukwama alirudi tena na kuwaonyesha kwa ukamilifu eneo husika…nampongeza sana,” alisema.

Akiwa eneo hilo la tukio, Mongella ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalamaya Mkoa, aliliomba Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na polisi, kuanza kukagua mapango yote katika Mkoa wa Mwanza ambayo yanadaiwa kuwa maficho ya wahalifu ili kudhibiti uhalifu.

Maoni ya wakazi wa Utemini

Wakizungumza kwa nyakati tofauti eneo la tukio, baadhi ya wananchi ambao hawakupenda kuandikwa majina yao gazetini, walisema eneo hilo la mapango limekuwa likishikiliwa na vikundi vya uhalifu kwa muda mrefu tangu  mwaka 2012 na mara zote wananchi wamekuwa wakitoa taarifa polisi.

“Eneo hili kuanzia usawa ule wa Misikiti wa Rahman kuna mapango mengi, yanaweza kuwa zaidi ya manne, lakini polisi walikuwa wakipambana na watu hawa kwenye pango moja tu.

“Mapango mengine yalikuwa yakitumiwa na waumini wa msikiti   mmoja kwa mazoezi ya judo na karate,” alisema mmoja wa wakazi hao.

Saidi Juma anasema tukio hili siyola  ujambazi kwa kuwa wahusika wanafahamika na   wamekuwa wakifanya mazoezi ya kupigana na matumizi ya silaha kwa muda mrefu katika mapango hayo kwa mwamvuli wa dini.

“Baada ya kuchinjwa waumini wenzetu msikitini, ndipo polisi walikuja juu na sasa wameanza kubaini kuwa eneo hilo ni hatari, lakini tulitoa taarifa   za kuwapo hawa maharamia,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles