27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto: Tutajitoa mhanga

zittoNA MWANDISHI WETU, Dar es Salaam

KIONGOZI wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema Rais John Magufuli amejitoa mhanga kupambana na ufisadi, lakini wapinzani watalazimika kujitoa mhanga kulinda demokrasia inayoelekea kupotezwa na viongozi waliopo madarakani.

Akihutubia mkutano wa hadhara Dar es Salaam jana, Zitto alisema nchi inaweza kuingia katika madhara makubwa kama wapinzania hawatasimama kidete dhidi ya mbinu za kufifisha demokrasia na misingi ya uwajibikaji nchini.

Katika mkutano huo, Zitto vilevile alizungumzia kusimamishwa kazi za Bunge, suala la Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Zanzibar, mwelekeo wa Bajeti na tishio la nchi kuelekea kwenye utawala wa imla wa mtu mmoja.

“Ni imani yetu kuwa ufisadi utapigwa vita kwa ukamilifu siyo kwa kutegemea nia ya mtu mmoja bali kuboresha na kutumia misingi ya demokrasia kwa kujenga taasisi madhubuti zitakazomaliza janga la ufisadi bila ya kutegemea nia ya rais pekee,”alisema Zitto.

Huku akishangiliwa, kiongozi huyo wa ACT alisema baada ya uchaguzi, viongozi wapya wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali nzuri na mbaya zikiwamo kubomoa demokrasia.

“Tumeshuhudia uamuzi mwingine ambao unatia hofu, ingawa tunaona dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi, lakini pia tunaona mbinu za chini chini za kutokomeza demokrasia ya nchi yetu ambayo tumeijenga kwa jasho na damu.

Wabunge kusimamishwa

Alisema Mei 30 mwaka huu, Bunge likiongozwa na Naibu Spika lilipitisha Azimio la kuwasimamisha  wabunge wa upinzani, Esther Bulaya, Tundu Lissu, Halima Mdee, Pauline Gekul, Godbless Lema,  John Heche na yeye  Zitto.

“Mimi binafsi pamoja na wabunge wengine sita hatukufanya fujo yoyote ndani ya Bunge, kosa letu kubwa ni kutaka kuhoji uamuzi wa Serikali kuzuia kuonyeshwa live matangazo ya Bunge.

UDOM:

Alisema wanafunzi 7,800   waliofukuzwa Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) wanasomea programu maalumu ya ualimu wa sayansi ni watoto wa masikini waliokubali kuacha kwenda kidato cha tano na sita ili wakawafundishe watoto wa masikini wenzao.

Alisema wanafunzi hao hawakuanzisha programu hiyo bali Serikali kupitia Baraza la Mawaziri ambalo Rais Magufuli alikuwa mjumbe, kwa mujibu wa kumbukumbu za Baraza la Mawaziri.

“Rais Magufuli hakupinga mpango huu na aliubariki kama wenzao walivyofanya na kuanza kutekelezwa, Tanzania ina uhaba wa walimu wa sayansi 26,000 na tukienda kwa utaratibu wa kawaida tutahitaji miaka 20 kuziba pengo hilo.

“Rais Magufuli anafikia kuita watoto vilaza? Rais huyu anayesema yeye ni Rais wa masikini anaita watoto wa masikini vilaza?

“Rais sifa zimempanda kichwani, hana budi kuwaomba radhi vijana hawa na wazazi wao. Rais ni Mwalimu, anajua madhara ya saikolojia kwa maneno aliyoyasema. Ni sawa na jenerali wa jeshi anayetukana askari wake walio mstari wa mbele. Hata Baba wa Taifa hakuthubutu kamwe kuita wanafunzi vilaza hata kama walimuudhi kiasi gani.

“Rais Magufuli anazungumza  mno… Rais ajue kuweka akiba ya maneno. Yeye ni kiongozi wa wote, wenye akili na vilaza, anapaswa kuwa wa mwisho kuzungumza  ili watu waweze kukata rufaa kwake, sasa akishazungumza  wananchi waende kwa nani?”alihoji Zitto.

ZANZIBAR

Zitto pia alilaani  kauli ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Ali Mohamed Shein kutamka kuwa hamwogopi Maalim Seif kwa sababu hana vifaru na mizinga, akiita ya kutisha.

“Kamwe huwezi kuzima haki za wananchi kwa vifaru na mizinga. Dk. Shein akumbuke kuwa Sultan alikuwa na jeshi, vifaru na mizinga na ulinzi wa dola kubwa kama Uingereza lakini aliangushwa na wananchi wa Zanzibar mwaka 1964.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles