Na. Christina Gauluhanga, Dar es Salaam
Baraza la Taifa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limesema kelele zaidi ya viwango zinasababisha upungufu wa nguvu za kiume pamoja na kuleta athari za akili na afya ya ubongo.
Akizungumza leo Julai 24, katika mkutano wa wamiliki wa baa, kumbi za starehe na sherehe kuhusu kelele zaidi ya viwango vilivyoainishwa katika kanuni za Mwaka 2015 za viwango vya udhibiti wa uchafuzi kelele na mitetemo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Mhandisi Samuel Mafwenga, amesema tangu mwaka 2016 hadi 2019 wamepokea malalamiko 4,790 ambapo kati ya hayo 952 sawa na asilimia 20 ni ya kelele.
Amesema tafiti zinaonyesha kelele zina athari kwa Watoto kiakili, kiafya na kwa wajawazito na wazee pia.
” Tatifiti zinaonyesha kelele zina athari ya faragha pia hivyo kusababisha upungufu wa nguvu za kiume hivyo ni vyema kuzingatia viwango vilivyopendekezwa kulingana na maeneo,”amesema Mafwenga.
Amesema ili kuondoa kero hiyo ndani ya jamii ni vyema wamiliki wakatumia vifaa vya kupunguziwa Kelele ili waweze kupima viwango vyao.
Naye, Mwakilishi wa wauzaji vifaa vya kupunguzia sauti, Gwakisa Mwakyusa amesema kuna vifaa tayari vimeletwa hapa nchini vipo Shirika la Viwango Nchini (TBS), vinafanyiwa uchunguzi.
“ Chombo hicho unaweza kukiweka ukutani na kikakuonyesha kwa kengele kama umezidisha kiwango unachotakiwa kukitunza na kina uwezo wa kutunza kumbukumbu zako, hadi sasa tana vifaa vya aina mbili na tunaendelea kuandaa mikakati ya jinsi ya umiliki na gharama yake itakuwa Kati ya Sh.300,000 hadi 400,000,” amesema Gwakisa.