Na Ramadhan Hassan,Dodoma
SPIKA wa Bunge Job Ndugai amezitaka asasi za kirai zisikubali kutumika na watu wasio na mapenzi na Nchi huku akidai Bunge limetunga Sheria kwa lengo la kuwabana watu wenye nia tofauti na malengo ya Serikali ili kuweza kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa shughuli zinazofanywa na AZAKI.
Spika Ndugai ametoa kauli hiyo leo Oktoba 23, 2021 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa wiki ya Azaki ambapo amedai Asasi za Kiraia zina mchango mkubwa katika kutekeleza mipango ya Serikali ikiwemo kufanya utafiti ili kuweza kutoa majawabu mbalimbali ya changamoto za jamii.
Amesisitiza asasi hizo zisikubali kutumika na watu wasio na mapenzi na nchi yetu, huku akiwataka kujitahidi kuipenda nchi pamoja na kufanya kazi kwa Maslahi ya Nchi yetu.
Ndugai ambaye ni Mbunge wa Kongwa amesema Bunge limetunga Sheria kwa lengo la kuwabana watu wenye nia tofauti na malengo ya Serikali ili kuweza kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa shughuli zinazofanywa na AZAKI.
Amesema Asasi za Kiraia zina mchango mkubwa katika kutekeleza mipango ya Serikali ikiwemo kufanya utafiti ili kuweza kutoa majibu mbalimbali ya changamoto za jamii.
Kwa upande wake,Mkurugenzi Msaidizi wa Idara Uratibu wa NGOs Mussa Sang’anya amezitaka asasi hizo kuendelea kuandaa midahalo na majukwaa ili kuendelea kujadiliana masuala mbalimbali na kutatua changamoto zinazojitokeza.
Aidha ametoa wito kwa Wadau wote kuhakikisha wanafuata Sheria, Kanuni na miongozo iliyowekwa na Wizara ipo tayari kushirikiana nao kwa kila hali ili kutimiza malengo kwa maslahi ya Taifa.
Pia amezitaka asasi hizo kutokuwa na mashaka kuhusu mabadiliko ya Sheria namba 3/2019 inayoweka ukomo wa miaka 10 kwa vyeti vya Usajili wa NGOs.
“Lengo la Serikali ni kuweka ukomo kuhuisha taarifa na kusaidia kutambua mchango wa Mashirika katika kufikia Maendeleo ya wananchi,”amesema.