26.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Ndugai, Mbunge CCM wavaana

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ametangaza kusitisha kwa muda uwakilishi wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), Stephen Masele, akisema sababu ni utovu wa nidhamu wa kiongozi huyo na kugonganisha mihimili.

Akizungumza bungeni jana, Ndugai alisema Masele ambaye ni Mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), amekuwa akipeleka maneno ya uongo kwenye ngazi ya juu ya Serikali na kwamba amekuwa akiitwa tangu Jumatatu arejee nchini kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge lakini amegoma.

Alisema mbali na kamati hiyo ya Bunge, Masele pia anasubiriwa na kamati ya chama chake ambayo nayo ina mambo ya kumuhoji.

Ndugai alisema kutokana na Masele kutorudi, amemwandikia barua Rais wa PAP, Roger Dang kumweleza juu ya kusitisha kwa muda uwakilishi wake katika Bunge hilo ili arudi nyumbani kujibu mambo yanayomuhusu.

Katika mitandao ya kijamii juzi na jana, kilisambaa kipande cha video kikimwonyesha Masele akimtuhumu Rais wa PAP kwamba anamshawishi Spika Ndugai ili amrudishe nyumbani.

Masele alisema amezungumza na Waziri Mkuu ambaye amemtaka kumaliza mambo yake kwanza katika Bunge hilo wakati yale ya nchini yakimalizwa hukuhuku.

“Rais nakuambia huna mamlaka ya kuniondoa hapa, nitaendelea kuwa makamu wa Rais, nilichaguliwa na hawa wajumbe, walinipigia kura,” alisema Masele.

Rais wa Bunge hilo, anakabiliwa na shinikizo kubwa la kung’olewa kwenye kiti chake kutokana na tuhuma mbalimbali ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka na kudhalilisha wanawake.

Hata hivyo, jana Ndugai alisema hawamuiti Masele kwa sababu ya kinachoendelea kwenye Bunge hilo, bali wanataka aje ajibu tuhuma zake za hapa nyumbani.

Kutokana na hali hiyo Spika Ndugai ameitaka Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumjadili Masele.

Akitoa taarifa hiyo jana bungeni kabla ya kuanza kwa kipindi cha maswali na majibu, Spika Ndugai alisema Masele ameonesha utovu wa nidhamu katika Bunge hilo (bila kuutaja).

Alisema kutokana na kuonesha utovu huo wa nidhamu, Bunge limesimamisha uwakilishi wake hadi hapo Kamati ya Maadili itakapomjadili.

“Katika uwakilishi wa Bunge la Afrika, kumetokea matatizo makubwa haswa kwa mheshimiwa Stephen Masele, kuna matatizo makubwa sana ya kinidhamu ambayo nisengependa kuyafafanua leo, muda hautoshi.

“Lakini tumelazimika kumtafuta Mheshimiwa Masele  kumrudisha nyumbani kuanzia Jumatatu, badala yake amekuwa akionyesha kugoma na hata jana (juzi) kwenye Bunge hilo ‘clip’ zimerushwa.

“Baada ya kumwandikia kwamba arudi nyumbani ili aje ahudhurie kwenye Kamati ya Maadili hapa, amekuwa akihutubia lile Bunge na kusema japo ameitwa na Spika, lakini ameambiwa na Waziri Mkuu ‘a-disregard’ (apuuzie) wito wa Spika, endelee tu na mambo yake kule kitu ambacho ni uongo na kutudhalilisha kama nchi.

“Ni kiongozi ambaye amekuwa akifanya mambo ya hovyo hovyo, na ndiyo maana tumemwita kidogo kwenye Kamati ya Maadili atufafanulie, huenda labda yuko sahihi, lakini kwa mtizamo wetu amekuwa akifanya mambo ambayo ni hatari kubwa, ikiwemo kugonganisha mihimili.

“Anapeleka kwenye mhimili wa Serikali juu kabisa maneno mengi ya uongo na ushahidi upo na kulidhalilisha Bunge, ni kiongozi amejisahau, ajui hata anatafuta kitu gani.

“Ukiacha hizo vurugu ambazo hivi sasa zinaendelea kwenye Bunge lake huko, ambazo anaziongoza yeye mwenyewe, ni vurugu kubwa, ila haituhusu sana, tunamuita kwa ajili ya mambo ya hapa nyumbani ya utovu wa nidhamu.

“Sasa kwakuwa tumekuwa tukimuita tangu Jumatatu hataki kurudi, ningependa kulifahamisha Bunge hili kwamba kwa niaba yenu na kwa mamlaka niliyonayo, nimemwandikia barua Rais wa PAP ya kusitisha uwakilishi tuliompatia Mheshimiwa Masele katika Bunge la PAP hadi hapo Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itakapokamilisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake na kukamilisha taarifa yake.

   “Kwa hiyo kwa muda Mheshimiwa Masele hatakuwa Mbunge wa Bunge la Afrika hadi tutakapokuwa tumemalizana naye hapa, na hapa kuna kamati mbili zinamsubiri.

“Kamati ya Bunge ya Maadili, lakini pia Kamati ya Maadili ya chama chake nayo kuna mambo inamuhitaji kuja kuyajibu hapa nyumbani, kwahiyo kuanzia sasa yeye siyo Mbunge wa Bunge hilo tena, hadi tumalize masuala ya hapa nyumbani ndiyo tutaamua wenyewe, mambo haya huwa tunaamua wenyewe tunaendeleaje kuanzia hapa,” alisema Ndugai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles