27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Jeshi kuwa la kisasa zaidi – Dk. Mwinyi

Na ARODIA PETER-DODOMA

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussen Mwinyi, amesema katika mwaka ujao wa fedha 2019/20, watalipa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vifaa na zana bora za kisasa.

Alisema sambamba na hilo, watatoa mafunzo kwa wanajeshi ili kuliongezea jeshi hilo uwezo na weledi wa kiutendaji, kiulinzi na kivita.

Akiwasilisha hotuba ya wizara hiyo bungeni jana, Dk. Mwinyi alisema pia wamepanga kuboresha mazingira ya kazi, kuimarisha upatikanaji wa huduma stahiki na mahitaji ya msingi kwa wanajeshi na watumishi wa umma.

Pia, kuwapatia vijana wa Tanzania mafunzo ya ukakamavu, umoja wa kitaifa, uzalendo na stadi za kazi.

Aidha waziri huyo alieleza kuwa wizara itaendeleza tafiti na uhaulishwaji wa teknolojia kwa kuimarisha na kuanzisha viwanda kwa madhumuni ya kuzalisha bidhaa na huduma kwa matumizi ya kijeshi na kiraia.

Pia kuimarisha ushirikiano wa jumuiya za kimataifa, kikanda na nchi moja moja katika nyanja za kijeshi na kiulinzi.

Nyingine ni kufanya upimaji, uthamini na ulipaji fidia ya ardhi katika maeneo yaliyotwaliwa kwa matumizi ya jeshi.

Dk. Mwinyi aliongeza kuwa wataendelea kushirikiana na mamlaka za kiraia katika kukabiliana na majanga na dharura pale inapohitajika.

“Kulipa stahili mbalimbali za maafisa, askari, vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa na watumishi wa umma.

“Kukamilisha sera ya ulinzi wa taifa, mwongozo wa viwanda jeshini na mpango wa maendeleo wa miaka 10, yaani 2018/29-2027/28 wa kuliimarisha Shirika la Nyumbu,” alisema.

Dk. Mwinyi pia alizungumzia hali ya usalama wa mipaka ya Tanzania kuwa ipo shwari licha ya kuwapo tishio kutoka kwenye vikundi vya kigaidi katika baadhi ya nchi jirani.

UFINYU BAJETI

Mbali na hilo, waziri alisema kuna changamoto mbalimbali, kubwa ikiwa ni ufinyu wa ukomo wa bajeti kwani kiasi cha fedha kilichoidhinishwa na Bunge kwa mwaka 2018/19 Sh trilioni 1.9 hakikidhi mahitaji halisi.

Alisema katika kipindi cha Julai 2018 hadi Aprili 2019, hakuna matukio yaliyoripotiwa baina ya Tanzania na nchi inazopakana nazo.

Hata hivyo, alisema zipo changamoto katika baadhi ya maeneo ya mipaka yanayohitaji kushughulikiwa ili kuboresha udhibiti na kuimarisha usalama wa nchi.

Katika hotuba hiyo, Dk. Mwinyi pia alizungumzia hali ya mipaka na changamoto kadhaa zinazokabili baadhi ya mipaka ya nchi.

Alitolea mfano mpaka wa magharibi mwa Tanzania katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo kuendelea kukumbwa na matukio ya uvunjifu wa amani kutokana na mapigano na mauaji.

“Kwa upande wa kusini changamoto zilizopo ni ujenzi holela wa makazi, matukio ya uhalifu yenye mwelekeo wa kigaidi, hususan kaskazini mwa Msumbiji.

“Kundi la kigaidi Al Sunnah wal Jamaah linaendelea kufanya uhalifu nchini Msumbiji katika Wilaya ya Nangane, Jimbo la Cabo Delgado.

“Changamoto nyingine ipo katika mpaka wa Ziwa Nyasa ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambayo inaendelea kutumia njia za kidiplomasia kulipatia ufumbuzi wa kudumu,” alisema.

Kuhusu ufinyu wa bajeti ya wizara yake, Dk. Mwinyi alisema fedha za maendeleo zilizotolewa kwa kiasi kikubwa zimetumika kulipia mikataba michache ya ununuzi wa zana na utekelezaji wa miradi mingine.

Alisema hali hiyo imesababisha wizara kutoweza kutekeleza mipango yote iliyojiwekea katika mwaka 2018/2019.

“Aidha katika kutekeleza azma ya viwanda vipya jeshini, kuna changamoto za uchakavu wa miundombinu ikiwamo karakana, maabara, mitambo na majengo huku karakana nyingine zikitumia teknolojia zilizopitwa na wakati sambamba na upungufu wa wataalamu wa kuendesha mitambo katika mashirika ya Mzinga na Nyumbu.

“Katika kukabiliana na changamoto hizo, wizara imekutana na wazabuni ili kuweka utaratibu wa kulipa madeni hayo,” alisema Dk. Mwinyi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles