29.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

Bunge lachambua hesabu za CAG

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

SPIKA wa Bunge Job Ndugai, amesema taarifa ya Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imekamilika na ameipeleka katika Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) ili iipitie na kuichambua.

Akitoa taarifa hiyo jana bungeni kabla ya kuanza kipindi cha maswali na majibu, Spika Ndugai alisema kwa mujibu wa kifungu cha 46, kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ya ukaguzi wa umma, hesabu za CAG zinapaswa kukaguliwa angalau mara moja kwa mwaka.

“Kwa mujibu wa kifungu 46, kifungu kidogo cha kwanza cha sheria ya ukaguzi wa umma, sheria namba 11 ya mwaka 2008, hesabu za CAG yaani za Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi zinapaswa kukaguliwa angalau mara moja kwa mwaka na kwamba Bunge kupitia Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali ya PAC  ina jukumu la kuteua mkaguzi wa kukagua hesabu za ofisi hiyo.

“Kwa maneno rahisi, Bunge ndio tunatafuta mkaguzi wa nje ambaye ndiye anayekagua hesabu za CAG, kwa hiyo ukaguzi ulishafanyika huko nyuma na Kampuni ya Eki Mangesho iliishakupatikana na imefanya kazi hiyo ya ukaguzi na imetuletea taarifa ya hesabu zilizokaguliwa za ofisi hiyo.

“Nimeona niwajulisheni ili muweze kufahamu katika hesabu zilizowekwa mezani wakati ule, hesabu za ofisi ya CAG hazikuwekwa mezani,” alisema Spika Ndugai.

Spika Ndugai alisema ameipokea taarifa hiyo, lakini kiutaratibu wanaipeleka PAC ili ipitiwe na kuchambuliwa.

“Nimeishapokea taarifa hiyo na nimeisha ipitia lakini utaratibu ni kwamba tunapeleka kwenye kamati ya PAC, kwa kuzingatia sheria ya ukaguzi naipeleka taarifa hiyo PAC ili ipitie na kuichambua.

“Na mara itakapomaliza itawasilisha uchambuzi huo kwangu na mambo mengine yatakayofuatia ni yale ambayo yatakuwa ya wakati huo, katika masuala ya ukaguzi hakuna anayebaki na hakuna anayejikagua mwenyewe kila watu wanaangalia wenzao,” alisema.

Ndugai alitoa kauli hiyo wakati huu ambapo Bunge limetangaza kutofanya kazi na CAG, Profesa Mussa Assad, kutokana na kauli yake aliyosema kuwa yawezekana Bunge halifanyii kazi ipasavyo ripoti zake kwa sababu ya udhaifu wake.

Januari 20, mwaka huu Profesa Assad aliitwa mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambako alihojiwa kwa zaidi ya saa tatu.

Kamati hiyo ilimwita Profesa Assad baada ya Januari 7, Spika Ndugai kumtaka msomi huyo kufika kwenye kamati hiyo kutokana na kauli yake ya kuliita Bunge ni dhaifu vinginevyo atapelekwa akiwa amefungwa pingu.

Kauli ya Profesa Assad juu ya udhaifu wa Bunge aliitoa alipokuwa akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa alipoulizwa juu ya ripoti zake za kila mwaka ambazo baadhi ya watu wanaona kama hazifanyiwi kazi.

CAG akijibu swali hilo alisema; “Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.

“Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.

“Sitaki kuwa labda nasema hili kwa sababu linahusisha watu fulani, lakini ninachotaka kusema ni kuwa Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata huu udhaifu unaoonekana utapungua.”

Baada ya Profesa Assad kuhojiwa na Kamati ya Bunge, Ndugai aliliambia Bunge kuwa msomi huyo hakuomba msamaha bali alisema atazidi kutumia neno dhaifu kwakuwa ni lugha ya kawaida kwenye kazi zao za ukaguzi.

Kutokana na hali hiyo, alitangaza Bunge kutofanya kazi na Profesa Assad, huku akimtaka ajiuzulu nafasi yake jambo ambalo msomi huyo hakulikubali.

Kutokana na mvutano huo, ripoti za CAG mwaka huu ziliwasilishwa bungeni bila Profesa Assad kuhudhuria kama ilivyo desturi.

Pia Profesa Assad aliitisha mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake na kutoa muhtasari wa ripoti zake jambo ambalo ni tofauti na ilivyozoeleka. Awali alikuwa akitumia ofisi za Bunge.

Pia viongozi wa PAC na wale wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), hawakuhudhuria jambo ambalo si kawaida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles