Mwandishi wetu- Dodoma
SPIKA Job Ndugai, amesema Bunge litashirikiana na Serikali kuhakikisha Mahakama inapata rasilimali za kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kutoa haki kwa wakati.
Akizungumza katika uzinduzi wa wiki ya utoaji elimu ya sheria iliyoambatana na matembezi maalum ya kilomita tano yaliyoanza kwenye viwanja vya Mahakama Kuu Dodoma hadi viwanya vya Nyerere Square, Ndugai aliipongeza Mahakama kwa maonesho mazuri.
‘’Bunge litashirikiana na Serikali kuhakikisha Mahakama inapata rasilimali za kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kutoa haki kwa wakati,’’ alisema Spika.
Aidha Spika Ndugai alitoa wito kwa wakazi wa Dodoma kufika katika viwanja hivyo ili wajue haki zao na kupata elimu ya sheria kwa kuwa Mahakama si sehemu ya kuogopwa.
Ndugai aliipongeza Mahakama kwa kauli mbiu yake ya mwaka huu inayosema ‘Uwekezaji na Biashara: Wajibu wa Mahakama na Wadau kuweka Mazingira wezeshi ya Uwekezaji.’ Kwa kuwa inasaidia kufikisha dhamira ya Serikali ya awamu ya tano kujenga uchumi imara na viwanda.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Bilinith Mahenge, alitoa shukrani kwa Mahakama kujenga majengo ya Mahakama Jumuishi na Ofisi za Makao Makuu jijini Dodoma.
Katika maonesho hayo, Spika pia alizindua vitabu vitatu vya muongozo wa kusikiliza mashauri mahakamani vinavyotumika mahakama za mwanzo, mahakama za wilaya na mkoa na mahakama kuu.
Akizungumzia kuhusu vitabu hivyo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk. Eliezer Feleshi, alisema vitabu vimeshawekwa kwenye tovuti ya Mahakama ya Tanzania.
Wiki ya hiyo imeanza Januari 31, mwaka huu na inatarajia kumalizika Februari 5 ambapo kilele chake cha siku ya sheria nchini kitafanyika Februari 6 jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere. Mgeni rasmi katika kilele hicho, anatarajiwa kuwa Rais wa Dk. John Magufuli.