27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Msako wasiopeleka watoto shule kufanyika nyumba kwa nyumba

Allan Vicent- Igunga

MKUU wa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, John Mwaipopo, ameagiza wazazi na walezi wa watoto wote waliofaulu darasa la saba mwaka jana kuhakikisha wanaripoti shuleni kabla ya kuanza kwa msako wa nyumba kwa nyumba.

Akizungumza katika kikao cha kawaida cha baraza la madiwani kilichofanyika jana mjini hapa, alisema baadhi ya wazazi na walezi hasa wa vijijini, wamekuwa na tabia ya kuzuia watoto wao wasiendelee na masomo ya sekondari wanapofaulu darasa la saba jambo ambalo halikubaliki.

Alisema baadhi yao walikuwa hata wakidiriki kuwashawishi watoto wao waandike majibu ya uongo kwenye mitihani ya mwisho ili wasifaulu na kuchaguliwa kuendelea sekondari.

Mwaipopo alibainisha kuwa elimu ni ufunguo wa maisha hivyo watoto wakipata elimu watakuwa msaada mkubwa sana kwa wazazi, walezi na taifa kwa ujumla, hivyo akaagiza kila mzazi au mlezi ambaye mtoto wake kafaulu ampeleke shule.

“Madiwani, maofisa elimu kata na watendaji wa vijiji na kata zote wapeni taarifa wananchi, kuanzia mwezi huu wa pili tunaanza msako wa nyumba kwa nyumba ili kubaini wazazi na walezi ambao hawajapeleka watoto wao shule’, alisema.

Alisema Serikali ya awamu ya tano imeboresha sekta ya elimu kwa kiasi kikubwa ikiwemo kuanza kutoa elimu bure kwa watoto wote kuanzia shule ya awali hadi kidato cha nne na kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Alisema maboresho ya shule hizo yamewezesha shule za sekondari za kata kuwa miongoni mwa zinazofanya vizuri ikiwemo baadhi ya wanafunzi wake kupata daraja la kwanza au kuongoza kitaifa.

“Mzazi yeyote ambaye mtoto wake hajaripoti hadi sasa katika shule aliyopangiwa atoe taarifa haraka iwezekanavyo katika shule husika au kwa ofisa elimu na aeleze kwa nini hajaripoti kabla hatua kali hazijachukuliwa”, alisema.

Aidha aliwataka waliopeleka watoto wao katika shule binafsi kutoa taarifa ili ijulikane mtoto yuko wapi huku akisisitiza kuwa haina haja ya kulipa gharama kubwa wakati shule za Serikali zikiwemo za kata zinafanya vizuri sana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles