Christina Gauluhanga -Dar es salaam
CHAMA cha NCCR Mageuzi kimesema hadi sasa kimepokea wanachama wapya 59,680 waliojiunga wakitoka katika mikoa mbalimbali wakiwamo vigogo wa ACT Wazalendo.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Anjelina Mutahiwa, alisema NCCR inaendelea na shughuli za kisiasa katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kujiimarisha zaidi.
Alisema wakati wanaendelea na shughuli za chama, wapo wananchi ambao wanaelewa sera za chama na kuamua kujiunga nao wakiwamo wanachama 9,540 Mkoa wa Mbeya, Shinyanga 20,645 na Kigoma 29,495.
“Mkutano Mkuu wa Taifa ulitoa maagizo kwa Halmashauri Kuu ya Taifa kuandaa mpango kazi kwa mwaka 2020 na ulipitishwa na tunaendelea kufanya shughuli za kukijenga chama,” alisema Anjelina.
Alisema katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi vya siasa wa mwaka 1985 walifanikiwa kupata wabunge 19, lakini kwa sababu ya udhaifu wa uendeshaji chama, uchaguzi wa mwaka 2000 wabunge wote 19 hakuna hata mmoja aliyeweza kurejea bungeni.
Anjelina alisema chama hicho kinaaamini kuwa kufanya kosa sio kosa bali kurudia kosa, kwa kipindi cha miaka 20 sasa wamejifunza mambo mengi wakiongozwa na itikadi ya utu ambayo ndiyo itikadi bora pekee duniani.
“Tunaomba Watanzania wawapuuze wanaoeneza taarifa ambazo si sahihi kwani chama chetu kinaongozwa na misingi ya itikadi ambayo ni udugu, maadili, usawa, haki, imani, mabadiliko, uhuru, wajibu, asili, kazi na endelezo,” alisema Anjelina.