NA JESSCA NANGAWE
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, jana aliongoza mamia ya waombolezaji katika kuuaga mwili wa aliyekuwa mwandishi wa habari za michezo na burudani, Amina Athuman, jijini Dar es Salaam.
Amina alikuwa mwandishi wa Kampuni ya Uhuru Publication wanaochapisha magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani.
Mwili wa marehemu Amina, aliyefariki katika Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo visiwani Zanzibar alipokwenda kuripoti mashindano ya Kombe la Mapinduzi kutokana na matatizo ya uzazi, unatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwao Tanga.
Akizungumza baada ya mwili huo kuwasili, Nnauye alisema tasnia ya michezo imempoteza mmoja wa waandishi wachapakazi, aliyekuwa akifanya kazi zake kwa umakini mkubwa huku akiitaka familia yake kuwa na moyo wa subira kufuatia kifo hicho.
“Alikua ni moja ya waandishi wenye kujituma sana katika kazi yake, tulifahamu uwezo wake, kikubwa ni kumwombea makazi mema huko alipo, yeye ametangulia na sisi tupo nyuma yake, tunawapa pole wanafamilia kutokana na msiba huu mzito,” alisema Nnauye.
Marehemu Amina ameacha mume na mtoto mmoja wa kike, Yusra.