23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

NAMNA YA MTOTO KUJIFINZA -2

watoto-wakicheza-mpiraTUNAENDELEA kujifunza kuhusu hatua mbalimbali za mtoto katika kupambana na kupambanua. Katika safu yetu leo tutaangalia hatua za kujifunza kwa mtoto kuanzia umri wa miezi 0 hadi miaka minane.

 

Kushiriki na wenzake

Mtoto anapata nafasi ya kujifunza mambo mbalimbali toka kwa wenzake na kukuza au kuendeleza ushirikiano. Ushirikiano wa mtoto na kundi rika unamuwezesha kujijengea uwezo wa kutoa mawazo yake kwa kuuliza wenzake maswali na kuiga yale yanayofanywa na wenzake. Hivyo kundi rika lina mchango mkubwa katika kumwezesha mtoto kujifunza.

 

Hatua za kujifunza kwa Mtoto

Kujifunza kwa mtoto kunaanza pindi anapozaliwa. Kujifunza kuko kunatofautiana kulingana na umri, na uwezo wa kuelewa, kufahamu na kupambana na kupambanua mazingira yanayomzunguka. Kujifunza kwake kunategemea pia ukomavu katika makuzi yake kimwili, kiakili, kijamii, kihisia na kimaadili. Ili mtoto aweze kujifunza mzazi au mlezi hana budi kuzingatia mambo anayoweza kutenda mtoto kulingana na umri na uwezo wake.

 

Miezi 0 – 6

Mtoto anatofautisha sura ya mama na watu wengine, anajizoesha kutumia viungo vyake, anajizoesha kujigeuza, kushika, kukaa, anaonyesha hisia tofauti, anatofautisha sauti, ladha ya vitu na harufu. Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake mwonyeshe tabadamu na kuongea naye, mpatie vitu vya kusaidia kufanya mazoezi ya kukaa bila kuanguka, mpatie vifaa vya kuchezea vyenye rangi na milio mbalimbali na weka mazingira katika hali ya usafi.

 

Miezi 7 – 12

Mtoto anainuka na kukaa, anatambaa, anajizoeza kusimama bila kuegemea, anajizoeza kutembea, anasema neno moja au mawili na anaiga matendo rahisi. Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake mpatie mtoto vifaa vikubwa atakavyoweza kushika kwa urahisi, tenga muda wa kucheza na kuzungumza naye, tamka majina ya watu na vitu mbalimbali na mpe vifaa vya michezo.

 

Mwaka 1 – 2

Mtoto anapanga na kujenga vibao, anachora michoro mbalimbali na anaendelea kuiga matendo rahisi. Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake tumia mbinu za miezi 7-12 pamoja na kumuuliza maswali rahisi na kumshirikisha katika shughuli ndogondogo.

 

Miaka 3 – 4

Mtoto anajifunza sehemu mbalimbali za mwili, anaosha mikono, anakula mwenyewe, anaimba, anataja namba na anashirikiana na wenzake. Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake ongea naye, jibu maswali anayouliza kwa usahihi na busara, mpe vifaa vya kuhesabu na kulinganisha maumbo, msimulie hadithi, mfundishe michezo na nyimbo, mwimbie, mzoeze kuvaa, kula chakula, kujisaidia chooni na kufunga vifungo au kamba za viatu.

Miaka 5 – 6

 

Mtoto anadadisi, anauliza maswali, anajifunza stadi mbalimbali kwa mfano kucheza mpira, kuchora, kuandika, kuhesabu na kusikiliza kwa makini. Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake zungumza naye na kujibu maswali anayouliza na kumzoeza mtoto kupanga muda wa shughuli zake.

 

Miaka 7 – 8

Mtoto anakuwa mdadisi, anashiriki michezo mingi na anashiriki katika vikundi na makundi rika. Ili kumchangamsha na kuchochea maendeleo yake mzoeze mtoto kupunguza muda wa michezo na kuweka mkazo katika masuala ya shule, mwelekeze na kumtia moyo wa kujifunza na kudadisi vitu mbalimbali anavyopendelea, msaidie mtoto kujifunza zaidi katika masomo yake na fuatilia maendeleo yake shuleni na katika vikundi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles