23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

JAMII IZINGATIE MALEZI YENYE MAADILI

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei akizungumza na mtoto
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei akizungumza na mtoto

Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

SAMAKI mkunje angali mbichi na mtoto umleavyo ndivyo akuavyo ni misemo ambayo imezoeleka sana na imekuwa ikifananishwa na mtoto hasa katika hatua ya makuzi na malezi.

Mtoto anafananishwa na samaki kwa maana kwamba huwezi kumkunja samaki akiwa mkavu bali mbichi, vivyo hivyo katika suala la malezi maadili mema huanza kujengwa kuanzia hatua ya utoto.

Hivyo semi hizi zinatufundisha kwamba watoto wanahitaji mwongozo mzuri angali au tokea wanapokuwa wadogo na wanatakiwa waonyeshwe malezi na njia nzuri wangali bado wabichi.

Hatua hii ya utoto ni muhimu katika makuzi na malezi na isipozingatiwa vizuri huwa ni vigumu mtoto kuweza kuwa na maadili mema na matokeo yake hata akiwa mzima huendelea na kushikilia misingi mibovu.

Hata hivyo katika familia zetu au jamii zetu kuna changamoto kubwa sana katika malezi ya watoto. Kumekuwa na visa mbalimbali vya mmomonyoko wa maadili katika jamii huku sababu kubwa zikielekezwa kwa wazazi na walezi kushindwa kusimamia vyema makuzi ya watoto wao.

Mwenyezi Mungu ametoa jukumu na wajibu kwa wazazi kuwapa watoto malezi bora yatakayowawezesha kuwa watu wema katika jamii.

Malezi ya wazi hayaanzii baada ya kuzaliwa, malezi bora huanzia mtoto anapokuwa tumboni mwa mama mpaka kufikia umri wa kujitegemea.

Malezi ya mtoto yamegawanyika katika sehemu kuu mbili, malezi ya kimwili na malezi ya kiroho.

Malezi ya kimwili ni yale yote anayofanyiwa mtoto ili akue katika afya njema. Malezi haya huanza mara tu mama anapopata ujauzito. Baba ana wajibu wa kumtunza mke kwa kumpatia vyakula maalumu ili mama na mtoto aliyeko tumboni wawe na afya nzuri.

Hata baada ya mtoto kuzaliwa wazazi husika wanapaswa kumlea mtoto kimwili na kimaadili kwa kuwafunza tabia na mwenendo mwema unaomridhisha Mwenyezi Mungu.

Suala hili la malezi ni miongoni mwa mada zitakazojadiliwa wakati wa kongamano maalumu linalohusu masuala ya amani, mshikamano na uwiano wa kidini.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Kituo cha Utamaduni wa Watu wa Iran kwa kushirikiana na wadau mbalimbali linatarajia kufanyika Januari 28 mwakani.

Makala haya yataangazia kwa kina mtazamo wa viongozi wa kidini juu ya suala zima la malezi kwa mtoto.

Pamoja na kuwapo kwa msukumo wa serikali na wadau mbalimbali katika suala zima la maadili, dini pia zina jukumu la kuwawezesha wazazi na walezi kuwalea watoto katika misingi ya imani zao.

Ndiyo maana viongozi mbalimbali wa dini wamekuwa wakihimiza juu ya suala zima la maadili katika jamii ili kuondokana na matatizo yanayowakabili watoto katika miaka ya sasa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Iran, Ayatullah Ali Khamenei, anasema nchi ambayo watu wake wana sifa ya kujali na kuimarisha familia ipasavyo basi huepuka matatizo mengi hususan yale ya kimaadili kutokana na baraka za kuwa na familia bora na imara.

“Ili taifa fulani liweze kufikia kwenye ustawi, utajiri, maendeleo ya kijamii, ushujaa, hekima, uhuru na maisha bora linahitajika kuipa heshima na umuhimu wa hali ya juu suala la malezi sahihi ya watoto,” anasema Khamenei.

Naye Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, anasema hivi sasa kuna matatizo mbalimbali yanayoibuka katika dunia ambapo watoto wa kike na akinamama ndio waathirika zaidi.

Anasema changamoto kubwa inayowakabili wazazi na walezi wengi ni kutokana na pilika pilika za maisha hatua ambayo imesababisha wakati mwingine kukosa nafasi ya kukaa na watoto wao.

“Ili watoto waweze kuwa na malezi pamoja na makuzi bora ni vyema jamii irudi katika mafundisho ya Mwenyezi Mungu ambayo yanaelekeza kuwalea watoto ili waweze kufanikiwa katika maisha ya duniani na akhera,” anasema Alhad Salum.

Naye Mwalimu Salum Mkude, anasema kuwatunza vyema watoto kutasaidia kujenga jamii bora inayofuata maadili.

Anasema hivi sasa wazazi wengi hawana mwamko wa kuzungumza na watoto wao kuhusu maadili na badala yake wameziachia televisheni na mitandao ya kijamii ambayo imekuwa mwalimu wa vijana kujifunza.

“Sisi tunapokuwa na watoto shuleni tunatimiza wajibu wetu kama walimu kwa kuwafundisha tabia njema lakini utashangaa kesho akija shule anakuwa na tabia tofauti, ukichunguza unagundua ameiiga tabia ile kutoka kwa watoto wengine au kwa kutazama mitandao ya kijamii,” anasema Mwalimu Mkude.

Mwalimu huyo anasema wazazi wanatakiwa kutumia muda mwingi kuwafundisha watoto wao maadili mema ili kuepuka kuwa na Taifa lenye watu ambao hawana maadili.

Kwa uapnde wake Naibu Mkuu wa Madrasatul Musbah iliyopo Manispaa ya Ilala, Sheikh Kassim Mzee anasema; “Ni vyema watoto wakaandaliwa katika maadili mema mapema kama ambavyo tunafanya katika madrasa yetu.

Anasema ili kuwa na jamii bora hatuna budi kuwalea watoto katika maadili mazuri hususani ya falsafa ya imani ya dini.

“Tuache ile dhana ya kwenda na wakati na dunia katika malezi ya watoto, na ndio maana watoto wengi wanakuwa hawana hofu ya Mungu. Ukimlea mtoto katika misingi ya kumjua Mungu utabarikiwa pia,” anasema.

Hivyo ni vema wazazi na walezi wakahakikisha kwamba watoto wanakuwa katika misingi ya maadili mazuri, kwa kufanya hivyo itasaidia sana pia kudhibiti wimbi la mmomonyoko wa maadili katika jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles