Na OSCAR ASSENGA, PANGANI
SERIKALI imeombwa kuangalia namna ya kuanza ujenzi wa barabara ya Tanga kuelekea Pangani hadi Saadan Bagamoyo, ili kumaliza tatizo la ukosefu wa usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo.
Ombi hilo lilitolewa juzi na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wilayani hapa.
Katika maelezo yake, Awesu alisema pamoja na kuwapo kwa miradi mingi inayotekelezwa katika maeneo hayo, malalamiko makubwa ya wananchi wa maeneo hayo ni ukosefu wa barabara.
Aweso ambaye pia ni Mbunge wa Pangani kupitia CCM, alisema wakati Rais Dk. John Magufuli akiomba kura kwa wananchi wa maeneo hayo mwaka 2015, aliwaahidi wananchi ujenzi wa barabara hiyo na kwamba ahadi hiyo ilichangia wananchi kumpa kura za ushindi.
“Kwenye mkutano wangu wa leo hii, nipo hapa nyumbani kama mbunge wenu na sikuja kama naibu waziri. Jukumu la mbunge ni kuwasemea wananchi wake ndiyo maana naiomba Serikali ifanye kila linalowezekana kwa kujenga barabara hiyo kwa wananchi wangu,” alisema Aweso.
Pamoja na hayo, alisema kuzorota kwa uchumi na maisha magumu kwa wananchi wa wilaya hiyo, kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na tatizo la kutojengwa barabara ambayo ingesaidia kuwapo kwa mawasiliano na maeneo mengine.
Naye Mkuu wa Mkoa Tanga, Martine Shigella, alisema barabara ya Tanga, Pangani hadi Saadan ni muhimu kwa maendeleo ya Mkoa wa Tanga.
Awali, akizungumzia suala la ujenzi wa barabara hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, alisema wamiliki wa viwanda, wafanyabiashara
wakubwa na wadogo wanatakiwa kulipa kodi ili fedha hizo ziweze kujenga miundombinu ndani ya nchi.