NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KAIMU kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Zimbabwe, Kalisto Pasuwa, ametajwa kutua katika klabu ya Simba na huenda uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi, leo ukamtangaza kocha huyo.
Awali Waserbia wawili Milovan Cirkovic na Goran Kopunovic ambao waliwahi kuifundisha Simba, walihusishwa mmoja wao kurejea kuifundisha klabu hiyo licha ya uamuzi huo kuwagawa viongozi.
Simba ilimuondoka aliyekuwa kocha Mkuu wa timu hiyo, Dylan Kerr kutokana na kutofanya vyema katika michuano ya Kombe la Mapinduzi na timu kukabidhiwa Mganda Jackson Mayanja.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa Simba imekuwa makini kufuatilia wasifu wa makocha mbalimbali ili kumpata atakayeisaidia klabu hiyo kurudisha hadhi yake.
Kiungo Mzimbabwe Justice Majabvi ametajwa kuunganisha uongozi wa Simba na kocha huyo na ametoa ushirikiano mzuri juu ya kocha huyo.
“Majabvi amekuwa msaada mkubwa kuunganisha kocha huyo kufanya mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo ya Simba, kwa sasa wanafanya siri kubwa kuanzia usajili pia hili la kocha ni kweli kesho (leo) wanatangaza kocha, ila si Milovan wala Goran, bali anatoka Zimbabwe tena anafundisha timu ya taifa ya nchi hiyo,” alisema.
MTANZANIA liliwasiliana na chanzo cha kuaminika nchini Zimbabwe, ambapo ilipatikana taarifa kuwa kocha huyo anaendelea na majukumu yake katika timu ya Taifa ya Zimbabwe inayotarajia kucheza mchezo wa kirafiki na Uganda The Cranes leo.
“Taarifa kama hizo bado hatujazisikia na Kalisto Pasuwa anaendelea na majukumu yake kuandaa timu kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Uganda The Cranes.
“Kwakuwa kocha yupo bize na timu, tutajua hili baada ya kumalizika mchezo huu wa kirafiki, kama kweli anakuja Simba lazima ataaga na kujiunga na timu hiyo,” kilisema chanzo cha habari nchini Zimbabwe.