Na Upendo Mosha, Hai
JESHI la polisi mkoani Kilimanjaro, linamshikilia mwanamume mmoja Severini Elius(57), mkazi wa Kijiji cha Mabogini wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka minne.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Koka Moita, alisema tukio hilo lilitokea Desemba Mosi mwaka huu saa 10 jioni, katika Kijiji cha Mabogini kata ya Mabogini wilayani humo.
Alisema mtuhumiwa huyo ambaye ni mfugaji anadaiwa kumbaka mtoto huyo na kumsababishia maumivu makali katika sehemu zake za siri ambapo tukio hilo lilibainiwa na dada wa mtoto huyo.
“Beatrice George (17) mwanafunzi na mkazi wa mabogini alibaini kubakwa kwa mdogo wake ambapo mzee huyo alimkuta mtoto akiwa nyumbani kwao peke yake akamvamia na kumvutia chumbani na kisha kuanza kumbaka kwa nguvu.
“Baada ya dada yake kurejea nyumbani alimkuta mdogo wake akiwa analia huku akilalamika kwamba ana maumivu makali sehemu zake za siri huku akiwa anamtaja mzee huyo ambapo baada ya yeye kumchunguza alibaini kuwa amebakwa na kuja kutoa taarifa polisi,” alisema.